Huhitaji Profesa ili uifahamu biashara

Asante na John ni wajukuu wa mwenyekiti maarufu wa kijiji Ligumbiro. Wakiwa katika mwaka wao wa mwisho wa elimu yao ya chuo kikuu, wakiwa katika vimbwete wanajisomea, John anaacha kusoma na kufunika daftari. Kisha anamtazama Asante, unajua Profesa Mark namwelewa sana, anaongea John. Kwa nini unamwelewa sana? Yaani anavyofundisha kuhusu ujasiriamali, ananihamasisha sana kufanya biashara nikimaliza chuo, John anasisitiza.

Mimi sioni kwa nini unavutiwa na profesa Mark, akaongea Asante. Kwa nini hunielewi? Ina maana wewe hakuvutii? Anauliza John. Umeshawahi kufika kwenye biashara ya profesa Mark? Asante anauliza huku akisimama na kuanza kuondoka. John anasimama na kupita mbele ya Asante na kusimama. Unatambua kabisa profesa muda wote yupo anatufundisha, atapata wapi muda wa kufanya biashara? Anauliza John.

Ndio maana nasema hawezi kunivutia kufanya biashara, anajibu Asante kwa mkato. Una maana gani? Anauliza John. Nawezaje kuvutiwa mambo ya biashara na mtu asiyejua biashara? Anajibu Asante kwa mkato. Mbona profesa anajua sana biashara na kanuni zake zote, ina maana huwa humuelewi? Anauliza John kwa mshangao.

 Unahitaji mfanyabiashara kukufundisha biashara. Kwa nini madaktari wanafunzi wa upasuaji wanafundishwa na madaktari bingwa wapasuaji? Akauliza Asante. Nafikiri kwa kuwa maisha ya watu hayawezi kufanyiwa majaribio, akajibu John kwa wasiwasi. Kwa hiyo mitaji ya watu ndio ya kufanyiwa majaribio? Akauliza tena Asante. John akamtazama Asante bila kujibu kitu.

Kwa nini umtumie profesa wa uchumi kufundisha ujasiriamali wakati yeye sio mjasiriamali? Ukiambiwa huyu ni daktari bingwa ambaye amesomea Ulaya ila hajawahi kufanya upasuaji kwa vitendo utakubali kupasuliwa naye? Akauliza tena Asante. Hapana, akajibu John. Sasa kwa nini ukubali kufundishwa ujasiriamali na Profesa wa uchumi ambaye hajawahi kumiliki japo genge la mbogamboga?

Sasa unafikiri mfanyabiashara gani amesoma mpaka kuwa na shahada ya uzamivu ili afundishe chuo kikuu? Anauliza John. Hapo ndipo kosa lilipo John, anajibu Asante. Huhitaji profesa aliyesoma nadharia kufundisha wanafunzi wanaokwenda kufanya biashara katika dunia halisi, anaelezea Asante.

Kama unavyohitaji daktari wa upasuaji ambaye anashinda chumba cha upasuaji ili awafundishe wanafunzi jinsi ya kupasua, unahitaji mtu anayeshinda sokoni kuwafundisha wanafunzi wanaotaka kufanya biashara sokoni. Vivyo hivyo hatuhitaji profesa aliyesoma kilimo kuwafundisha wakulima watarajiwa bali tunahitaji mtu anayelima na kuwa na kanuni za halisi za kilimo na sio nadharia. Bila kujali aliishia darasa la saba ama kidato cha nne. Kama ameshafanya biashara kwa mafanikio, huyu ndiye profesa tunayemuhitaji afundishe chuo kikuu, akamaliza Asante.