Mbeya. Miezi sita tangu Mwananchi kiripoti uhaba na uchakavu wa vyoo katika Stendi Kuu ya Mbeya, Halmashauri ya Jiji hilo limeboresha miundombinu hiyo huku wananchi wakipongeza hatua ya utekelezaji wa haraka.
Julai 24, 2024 Mwananchi lilieleza changamoto wanazopitia wananchi wakiwamo wasafiri, wahudumu na watumiaji kwa ujumla wa stendi hiyo wanavyohangaika kupata huduma ya choo.
Hata hivyo, katika uchunguzi wa habari hiyo, ilibaini baadhi ya wafanyabiashara hususani wa baa kutumia ndoo kujisaidia kwa wateja wao, huku wengine wakitumia mifuko kumaliza haja zao na kuleta sintofahamu kwa watumiaji wa eneo hilo.
Mwananchi ilifika tena katika stendi hiyo na kuona mazingira ya vyoo hivyo na kujiridhisha ubora wake kwa kujengwa katika ustadi na vifaa vyote vikiwamo ndoo za maji nje na sabuni.

Muonekano wa awali wa vyoo vya Stendi Kuu ya mabasi Mbeya kabla ya maboresho kufanyika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Jumatano, Februari 12, 2025 baadhi ya watumiaji wa stendi hiyo wamepongeza hatua zilizochukuliwa haraka kwa mamlaka za serikali wakiomba kuwapo utekelezaji wa miradi mingine ya kijamii.
Mmoja wa wahudumu katika stendi hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema kwa sasa wanafanya shughuli zao kwa amani baada ya kupitia kipindi kigumu cha harufu mbaya katika eneo hilo akieleza kuwa hatua hizo zinaongeza ufanisi kwa viongozi kwa wananchi wao.
“Hakuna ambaye hakuona hali ya vyoo ilivyokuwa awali, matundu yalikuwa machache lakini hadhi yake ilikuwa duni sana hadi kutumia ilikuwa ni tatizo sana, tunapongeza utekelezaji huu wa haraka,” amesema.
“Kuna muda tunalipa Sh200 za choo, lakini inategemea kuna nani hiyo, kuna siku tukikuta tunayemfahamu hatulipi kwa kuwa tunajuana vinginevyo tunalipia kila tukitaka huduma,” amesema mjasiriamali huyo aliyeomba kutotajwa jina.
Naye Yusuph Bena amesema kutokana na utekelezaji huo wa haraka, wanaomba kuwapo ufanisi katika miradi mingine huku akiomba kuangalia upya suala la gharama za kuingia stendi kuu na huduma za vyoo.
Amesema tofauti na maeneo mengine, Halmashauri ya Jiji la Mbeya lingeweka utaratibu wa kiwango cha kuingilia stendi kuu kikawa moja kwa moja kwa huduma za choo.

“Mtu kuingia stendi kuu ni Sh200, gharama ya choo Sh200 hadi Sh300 sasa mfumo ungesoma kitu kimoja halafu mwananchi akaondokana na usumbufu wa kuwa na tiketi zaidi ya moja kwenye eneo moja,” amesema Bena.
Naye Dickson Exaveli amesema pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya choo, lakini wahudumu wa stendi hiyo wanaotumia maduka ya stendi hiyo wangeondolewa kwenye gharama za choo.
“Watu wamepanga kwa shughuli zao, nadhani wangetazamwa katika gharama za huduma ya choo, japokuwa tunapongeza uboreshaji wa vyoo hivi na kwa sasa hali imetulia,” amesema Exaveli.
Mtoa huduma ya tiketi katika stendi hiyo upande wa vyoo, amesema kuwapo malipo ya kuingia stendi kuu na gharama za huduma ya choo ni kutokana na wazabuni kuwa wawili tofauti japokuwa mfumo ni mmoja.
“Kila eneo lina gharama zake kwa kuwa wazabuni ni wawili na wanatofautiana ila mfumo ni mmoja, kwa hiyo hatuwezi kuzungumzia zaidi lakini wananchi wanajua,” amesema mhudumu huyo.

Mtoa huduma ya getini, amesema wapiga debe katika eneo hilo hawalipi kiingilio na wanawafahamu na hakuna sura mpya inayoweza kuingia bila kufuata utaratibu.
“Wote wana utaratibu na wengi tunawafahamu, hivyo kusema mtu aingie hivi hivi haiwezekani, kimsingi hakuna kinachopotea,” amesema mtoa huduma hiyo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, John Nchimbi kuelezea changamoto hizo na hatua za haraka zilizochukuliwa kuboresha miundombinu ya vyoo, amesema kuwa hana kauli yoyote.
“Kwa ufupi sina kauli yoyote kati ya hayo mambo yako matatu uliyosema,” amesema kwa kifupi mkurugenzi huyo wa Jiji la Mbeya.