
Ni kawaida inapotokea ajali ya barabarani baadhi kupigwa butwaa wasijue nini cha kufanya, wapo wanaoweza kusaidia, lakini hawana ufahamu na huduma ya kwanza.
Pia wapo ambao hujisikia fahari kuwa wa kwanza kuchukua video ya ajali na kuisambaza badala ya kutoa msaada kwa majeruhi. Wapo pia wasio wasamaria wema hutumia nafasi hiyo kukwapua mali za majeruhi, ikiwamo pesa, simu na vito vya thamani.
Vitendo kama hivyo siyo vya kiungwana na vinachafua nia njema ya wale wasamaria wenye lengo la kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali za barabarani.
Leo nitalenga ufahamu kuhusu huduma ambazo mpitanjia anaweza kusaida ili kuokoa maisha ya majeruhi kwa jeraha la wazi linalovujisha damu.
Kutoa huduma ya awali kwa jeraha linalovuja damu inaokoa maisha na madhara yanayoweza kutokea, kutokana na kupoteza damu nyingi. Vilevile inasaidia majeruhi kuepukana na kuongezewa damu.
Itakumbukwa kuwa Tanzania ni nchi kubwa ambayo bado kuna changamoto za kuzifikia huduma za afya kwa wakati.
Kufanya aina yoyote ya usaidizi kwa majeruhi wakati wa kusubiri huduma za afya au kuwasafirisha kunaongeza nafasi ya kuishi kuliko kutofanya kitu.
Kama uko jirani na ilipotokea ajali na hufahamu lolote kuhusu huduma ya kwanza, basi angalau omba msaada au piga simu ya dharura, ikibidi pia toa ishara kwa vyombo vya moto kwa uangalifu.
Kama unaweza kuishinda hofu na kujiamini, jaribu kumpa msaada, kama ni katika barabara muweke pembeni majeruhi huku ukifanya hivyo kwa uangalifu kwa usalama wako na majeruhi.
Kwa haraka na umakini mkague majeruhi kama njia ya hewa haina mkwamo au kikwazo, tathimini hali ya upumuaji na mzunguko wake wa damu kwa kubinya mshipa wa mkono au shingoni kama unanepa.
Hii inaweza kubaini kama yupo hai, katika koma, amezimia au yuko kawaida, ingawa ni katika huduma za afya pekee ndio wanaoweza kuthibitisha kama majeruhi sio hai.
Kujua hali hizo tatu zinakufanya kupata picha kuhusu huduma anayohitaji mgonjwa, ama ni ya dharura au ya haraka.
Kama yuko kawaida na kuna jeraha la wazi linalovujisha damu tafuta kitambaa safi na weka shinikizo katika jeraha ili damu isiendelee kuvuja. Usiondoe kitu chochote kilichopo au kilichochoma katika jeraha. Kandamiza kwa sehemu inayotoa damu kwa kitambaa safi na salama. Ikiwa damu inaendelea kutoka usikiondoe kitambaa hicho, bali weka juu yake mpaka damu itakapo acha kutoka.
Kama maji na sabuni vipo jirani, unaweza kutumia pia kuosha mikono yako kabla ya kutoa huduma na baada ya kumaliza kuhudumia. Vilevile kuosha mazingira ya jeraha ili kupunguza hatari ya uvamizi wa bakteria. Ondoa vitu vinavyozunguka jeraha, ikiwamo nguo au vifaa kama mkanda au viatu.
Hali ya kutoka damu inapopungua au kuacha, endelea kuomba msaada kwa wengine au kwa kupiga simu ya dharura au mpeleke mgonjwa katika huduma za afya zilizo jirani.
Elimu ya huduma ya kwanza ya msingi ni elimu inayohitaji muendelezo katika jamii kuanzia shule ya msingi na kuendelea.