HRW: Wakimbizi wa Sudan hatarini kutokana na mapigano

Mapigano kati ya vikosi vya shirikisho vya Ethiopia na wanamgambo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo yamewaweka katika hatari kubwa wakimbizi wa vita kutoka Sudan.

Hayo yameelezwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, lenye makao yake mjini New York, Marekani.

Naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika Laetitia Bader amesema kuwa, wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia wamekuwa wakidhalilishwa na makundi tofauti ya wanamgambo waliojihami kwa zaidi ya mwaka sasa.

Katika ripoti yake, shirika hilo limesema kwamba, watu waliojihami wamefanya mauaji, uporaji, utekaji nyara na kudai kulipwa pesa ili kuwaachia huru, na kuwafanyisha wakimbizi kazi za lazima karibu na kambi mbili.

Shirika hilo limesema limetuma matokeo yake ya awali ya ripoti hiyo kwa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Ethiopia lililokiri kwamba, kambi ziko karibu na maeneo yenye machafuko ila likadai kuna usalama wa kutosha.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba.

Hivi karibuni Justin Brady, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini Sudan alisema, “leo, Sudan ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.