Hospitali ya Haydom yapanuliwa, kugharimu Sh6.5 bilioni

Haydom. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa amezindua jengo jipya la mama na mtoto la hospitali ya rufaa ya Kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara lenye thamani ya Sh6.2 bilioni.

Askofu Malasusa akizindua jengo hilo la mama na mtoto leo Ijumaa Machi 28 mwaka 2025 amesema jengo hilo litakuwa baraka kwa watu wengi watakaohudumiwa.

Amesema wamisionari wa kwanza kutoka Norway walifika Haydom Januari 15 mwaka 1955 na kupokelewa vyema na jamii ya eneo hilo na kuanza kutoa huduma ya afya.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa (katikati) akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo la mama na mtoto kwenye hospitali ya Rufaa ya Kilutheri ya Haydom. Picha na Joseph Lyimo

“Mgonjwa wa kwanza hapa hospitali ya Haydom ni mtu aliyeshambuliwa na chui na alitibiwa akapona tunapoadhimisha miaka 70 ya hospitali hii tuone Mungu alivyotembea nasi kwa jamii ya hapa kuwapokea wamisionari wa kwanza,” amesema Dk Malasusa.

Amesema madaktari wa hospitali ya rufaa ya Kilutheri ya Haydom wanafanya kazi ya kiuchungaji kwa kutibu afya za wagonjwa.

“Huwezi kupeleka rushwa madhabahuni, hapa tunatarajia maadili ya ki Mungu yaongoze na kusiwe na tabia zisizo nzuri tunazozisikia pengine,” amesema Dk Malasusa.

Katika hafla hiyo Mkurugenzi wa huduma za tiba, Dk Vicky Daud amesema hadi kukamilika kwa jengo hilo la mama na mtoto litagharimu Sh6.2 bilioni na sasa limetumia Sh4.7 bilioni.

Dk Vicky amesema vyanzo vya fedha za ujenzi wake ni hospitali ya Haydom asilimia 90 na asilimia 10 ni marafiki kutoka Norway.

Ametaja huduma zitakazotolewa kwenye jengo hilo litakaloweza kuhudumia karibu asilimia 70 ya wagonjwa wa nje ni huduma ya uzazi, huduma ya watoto wachanga, wodi ya watoto na vyumba vya upasuaji.

Ametaja huduma nyingine ni chumba cha wagonjwa mahututi, chumba cha upasuaji, vyumba vya kutakatisha vyombo, stoo kubwa ya dawa na vyumba vya wagonjwa binafsi.

Mkurugenzi wa huduma za tiba hospitali ya kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara, Dk Vicky Daud akisoma taarifa ya jengo la mama na mtoto la hospitali hiyo. Picha na Joseph Lyimo

Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo, Emmanuel Joseph amesema jengo hilo linatarajia kukamilika Aprili 2025.

Joseph amesema jengo hilo lilianza kujengwa Septemba 4 mwaka 2023 na litaanza kutumika kuanzia mwezi ujao wa Aprili mwaka 2025.

Mkazi wa mji mdogo wa Haydom, Elizabeth Elias amesema amefurahia uzinduzi wa jengo hilo la mama na mtoto kwani litaongeza tija kwa wagonjwa wa mikoa mbalimbali.

“Hii hospitali inatoa huduma kwa watu wa mikoa mbalimbali ikiwemo Manyara, Karatu Mkoani Arusha, Kondoa mkoani Dodoma, Mkalama mkoani Singida, Igunga mkoani Tabora na Meatu mkoani Simiyu,” amesema Elizabeth.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *