Hospitali Kanda ya Mbeya yaboresha chumba cha upasuaji wa watoto

Mbeya. Katika jitihada za kuboresha huduma bora za afya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya imeboresha miundombinu na kufunga vifaa tiba vya kisasa kwenye chumba maalumu cha upasuaji wa watoto.

Hatua hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma bora za afya na kuleta matumaini mapya kwa watoto wanaohitaji huduma katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Mei 6, 2025, siku moja baada ya kuzindua chumba hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Dk Uwesu Mchepange, amesema kuwa maboresho hayo yataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Ameeleza kuwa maboresho hayo yamewezekana kupitia ushirikiano kati ya hospitali hiyo na Shirika la Kimataifa la Smile Train kutoka Marekani, ambalo linaratibu matibabu ya mdomo wazi kwa watoto, pamoja na Shirika la Kids Operating Room (KidsOR) kutoka Scotland, ambalo limejikita katika kuboresha huduma za afya ya watoto kwa kuwekeza katika miundombinu ya upasuaji.

Dk Mchepange ameongeza kuwa mazingira ya chumba hicho yameundwa kwa namna ya kuondoa hofu kwa watoto kabla na baada ya upasuaji, kwa kuweka michoro ya kuvutia na vifaa vya michezo ya watoto vinavyowaburudisha.

“Chumba hiki kinamwezesha mtoto kuwa na hali ya utulivu, kwa sababu kinatoa mazingira rafiki yanayopunguza hofu na msongo wa mawazo kabla ya upasuaji,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa kimataifa katika kuboresha huduma za afya, hasa kwa watoto wenye changamoto mbalimbali.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa maendeleo kushiriki katika kuboresha sekta ya afya nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya Smile Train nchini Tanzania, Veronica Kimwela, amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Ufunguzi wa chumba hiki ni hatua kubwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya katika kuinua afya ya watoto, hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,” amesema.

Naye Mratibu wa KidsOR, Jenn Perkison, ameushukuru uongozi wa hospitali kwa kushirikiana katika utekelezaji wa mradi huo muhimu.

Daktari Bingwa wa Saratani na Magonjwa ya Damu kwa Watoto, Anna Magembe, amesema uwekezaji huo utasaidia katika utoaji wa huduma bora, hasa kwa watoto wenye matatizo ya upungufu wa damu ambayo huathiri maendeleo yao ya kimwili na kiakili.

Kwa upande mwingine, mkazi wa eneo la Ghana jijini Mbeya, Tusekile Mathias, ametoa wito kwa jamii kuelimishwa juu ya uwekezaji huu ili kuwasaidia watoto wengi zaidi.

“Uwekezaji huu usiishie hapa mjini tu, bali jamii vijijini wapewe elimu ya kutosha ili kusaidia kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *