Hoja kutoridhishwa na usalama wa chakula yaibuka bungeni

Dodoma. Wabunge wameibua hoja tatu za hali mbaya ya usalama wa chakula, kuchelewa kwa utekelezaji wa Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam na mfumo wa elimu kutokuwa na uwezo wa kuzalisha wahitimu wenye weledi na umahiri.

Hoja hizo zimetolewa bungeni leo Alhamisi, Aprili 10, 2025 na wabunge Neema Lugangira, Bonnah Kamoli na Shamsi Vuai Nahodha wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2025/26.

Katika bajeti hiyo ambayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliiwasilishwa bungeni juzi, aliomba Bunge liidhinishe Sh782.08 bilioni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Lugangira  amesema hali ya sasa ya vyakula vinavyouzwa sokoni, kutoka ndani na nje ya nchi, hairidhishi hasa linapokuja suala la usalama wa chakula.

Amesema mwaka 2019 Serikali, iliamua kufuta Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuhamishia jukumu la udhibiti na usalama wa chakula kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

 “Tuseme kwa uwazi, TBS  imeshindwa kuratibu na kudhibiti na usalama wa chakula, hatuwezi kuendelea kuendesha suala la usalama wa chakula kibiashara. 

“Suala la usalama wa chakula ni suala linalohusu uhai na afya za Watanzania, hatuwezi kuweka maisha ya Watanzania kwa sababu ya kusimamia biashara,” amesema Lugangira  .

Amesema wakati umefika sasa chini ya Waziri Mkuu wapate kauli ya Serikali maana tangu mwaka 2021 wamekuwa wakiomba Serikali irejeshe Wizara ya Afya masuala ya udhibiti na usalama wa chakula.

Lugangira amesema Tanzania kuna maeneo mengine wanashindwa kuuza mazao kwa sababu ya changamoto ya kushindwa kukidhi viwango vya usalama wa chakula.

Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah ameomba kuharakishwa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa Bonde la Mto Msimbazi, linalopita katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema imepita muda mrefu tangu mradi huo ulipoanzishwa lakini utekelezaji wake bado haujaenda kwa kasi inayohitajika, jambo linalochelewesha maendeleo ya eneo hilo.

 “Juzi juzi mvua zimeanza kunyesha na watu wameendelea kupata mafuriko na wananchi wanafahamu kuwa bonde liko katika mkakati wa kujengwa. Kwa hiyo tulikuwa tunataka katika majibu ya Waziri Mkuu atakapokuja kutuambia atuambie sasa umefikia wapi,”amesema Bonnah.

Amesema kwa sababu hilo ndilo bonde linaloendelea kuwapa shida katika Mkoa wa Dar es Salaam, shida hiyo ipo katika majimbo mengine.

Juni 26, 2019 aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aliwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Viwango ili kuhamisha majukumu ya kusimamia masuala ya chakula na vipodozi kutoka TBS na TFDA iliyokuwa inasimamia majukumu hayo.

Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Shamsi Vuai amesema bado mfumo wa elimu hautengenezi wahitimu wenye weledi na umahiri mkubwa kwa sababu hauzingatii shauku ya kujifunza kwa wanafunzi lakini pia hauzingatii  vipaji vya wanafunzi.

Amesema mifumo ya elimu Tanzania na malezi inadumaza vipaji, uwezo na karama za wanafunzi kwa sababu inalawazimisha kusoma masomo yasiyoendana na vipaji.

“Uzoefu unaonesha waliofanya vizuri duniani mambo makubwa ni wale waliofanya wanayoyapenda na yanayozingatia vipawa vya asili.  Kuwalazimisha kusoma wasichopenda inaathiri ari na uwezo wao wa kujifunza na ubunifu,”amesema Shamsi Vuai.

Amesema hivi karibuni Serikali ilizundua sera mpya ya elimu na utekelezaji wake unahitaji kiwango kikubwa cha fedha ili kuwaandaa walimu wenye ujuzi, ujenzi wa maabara za kisasa na karakana za mafunzo ili waweze kukabiliana na tatizo hilo.

Shamsi Vuai amependekeza mambo mawili yafanyike ikiwamo Serikali itumie ipasavyo Chuo Kikuu Huria (OUT), kuandaa walimu kwa mafunzo hasa katika mbinu kisasa za kufundishia na kutumia teknolojia ya kisasa katika elimu.

Amependekeza pia walimu kutumia kompyuta kwa njia ya mtandao kuwaonyesha watoto majaribio ya kisayansi ya jinsi mimea inavyotumia nishati na mengine mengi.

“Serikali ihimize matumizi ya mazingira ya shule na sayansi ya nyumbani katika kujifunza. Mfano kuonyesha nishati ya jua inavyotumika katika shughuli za nyumbani na usafi wa mazingira,”amesema Shamsi Vuai.

Amesema elimu inapaswa kujengwa katika misingi ya kujitegemea  kwa kuzingatia sayansi na teknolojia na uvumbuzi.

“Tuna mwanga wa jua,  lakini wataalamu wetu hawawezi kubuni kuvuna mwanga wa jua kutumika kama nishati, tuna wahandisi wengi lakini bado miundombinu mingi yakiwamo  madaraja  na majengo yanajengwa na wageni. Tunaagiza mitungi ya gesi wakati tuna wahandisi wengi,” amesema Shamsi Vuai.

Amesema kuna haja ya kuangalia muundo wa vyuo vikuu vya Tanzania ili kusisitiza zaidi vitendo kuliko nadharia.

Nahodha amependekeza kuwa na vyuo vikuu aina tatu vya utafiti, vyuo vikuu vya mafunzo ya kazi na vya sayansi na teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *