Dodoma. Uhai wa Bunge la Tanzania uko mbioni kutamatika huku wabunge wakiwa matumbo joto wasijue iwapo wananchi watawarejesha katika muhimili huo wa kutunga sheria na kusimamia Serikali au watawekwa kando.
Uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais utafanyika Oktoba 2025.
Tayari homa ya uchaguzi mkuu kwa wabunge imeonekana katika mkutano wa 18 wa Bunge la 12 uliomalizika Ijumaa ya Februari 14, 2025 jijini Dodoma.
Bunge la 12 linaloongozwa na Spika Tulia Ackson litamaliza safari yake ya miaka mitano Juni 27, 2025 kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kulihutubia na kulivunja.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Hotuba ya Rais itatanguliwa na ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Juni 26.
Katika mkutano wa Bunge la 18 lililojadili miswada mbalimbali na taarifa za kamati za Bunge za Februari 2024 hadi Januari 2025, baadhi ya wabunge mbali na kuchangia hoja hizo na maswali waliyokuwa wakiuliza, wengi walianza kuutaja uchaguzi wakitaka utekelezaji wa ahadi na namna wanavyoweza kurudi Bunge la 13.
Katika mkutano huo uliodumu kuanzia Januari 28 hadi Februari 14, 2025, mjadala mkubwa ulikuwa pongezi za wabunge hao kwa mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18-19, 2025 kuwapitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu.
Pia, kumpongea Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Mbali na kuwapongeza, wabunge wenyewe walitumia fursa walizopata kujipigia chapuo kwamba kwa yale waliyoyafanya kwa miaka mitano kwa wananchi wao hawana shaka muda ukifika watawarejesha tena bungeni.
Miongoni mwa wabunge waliotaja bungeni namna wanavyotamani kurejea tena bungeni ni Asia Haramga, Twaha Mpembenwe, Ruben Kwagilwa, Elibariki Kingu, Subira Mgalu, Joseph Kakunda, Josephat Kandege na Stephen Byabato.

Mbunge wa Ikungi (CCM), Elibariki Kingu
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika moja ya wilaya za Mkoa wa Singida ambaye ameomba asitajwe, amesema hofu ya wabunge siyo katika uchaguzi mkuu bali wanahofu kwenye uchaguzi wa kura za maoni.
“Mimi siyo msemaji wa chama, hata hivyo, naweza kukuambia, wale wabunge wetu hawaogopi uchaguzi mkuu ila wanakazi kubwa kwenye kura za maoni ndani ya chama, maana vijana wamejipanga vilivyo ndani ya CCM,” amesema.
Diwani wa siku nyingi, Evelyne Jakobo amesema kauli za wabunge ni kitu cha kawaida kipindi hiki, kwani mwanasiasa hapaswi kuwa mnyonge hata kama atakuwa na hali ngumu.
Evelyne ambaye amedumu kwa miaka 20 akiwakilisha nafasi hiyo kwa viti maalumu, amesema kauli za namna hiyo zinasimama katika maeneo mawili ambayo ni kujiamini na wakati mwingine ni huruma ya kuomba tena.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, wakili Fred Kalonga amesema hakuna dhambi kwa wanasiasa kujisifia na kuwasifu wa juu yao kwani hiyo peke yake ni siasa.
Wakili Kalonga amesema kitendo cha kueleza kama utarejea ni sawa na kumweka kwenye hofu adui yako au akate tamaa lakini pia kuwajengea matumaini wananchi kwamba uko imara na unaweza kuendelea na kazi waliyokutuma.
‘Hofu ya uchaguzi’
Ukiacha wabunge hao, kicheko kilikuwa kwa Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei aliyezungumzia suala la kurejea tena bungeni ikiwa ahadi alizotoa zingetekelezwa kabla ya uchaguzi lakini akaenda mbali zaidi kuwa ‘sijawa mzee.’

Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei
Dk Kimei aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB aliliambia Bunge bado anadaiwa kituo cha afya ambacho alisema kikijengwa katika jimbo lake hapana shaka anarudi tena mjengoni.
“Mimi siyo mzee, bado nina nguvu zaidi na tunachotaka kuwaambia wenzetu ni ile ahadi ya kituo cha afya na barabara kidogo, tukitimiza hayo wale watu wataturudisha tena hapa,” amesema Dk Kimei mwenye miaka 71.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asia Haramga amesema hajuti kuzaliwa Tanzania mahali ambako kuna viongozi wazuri, hivyo anaamini bado atarudi kuendelea kuwatumikia zaidi wananchi.
Kauli ya Asia ilikuja wakati akihitimisha hoja yake kuhusu Azimio la kumpongeza Rais Samia akisema kwa namna ilivyo inampa nguvu kurudi tena bungeni.
Mbunge wa Kibiti (CCM), Twaha Mpembenwe amesema ari ya kuwatumikia wananchi wa jimbo lake ameipata kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na Rais, hivyo ataendelea kuwatumikia akiamini watamrudisha tena bungeni.

Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe
“Mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan yananipa nguvu na ari ya kuwatumikia wananchi, naomba tuendelee kushirikiana tena hata kipindi kinachokuja tukashikamane,” amesema Mpemenwe.
Mbunge wa Handeni, Rubeni Kwagilwa amesema kama ingependeza Watanzania, hakukuwa na sababu za kufanya vinginevyo badala yake wabunge wote (akiwemo yeye) wangerudishwa tena ili waendelee kutekeleza kazi waliyoianza.
Katika hoja hiyo, Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Eribariki Kingu amesema Watanzania wamekielewa Chama cha Mapinduzi na wamewaelewa viongozi wanaotokana na chama hicho, kwani anaamini watafanya kweli Oktoba.
Kwa mujibu wa Kingu, kwenye uchaguzi huo wengine watakuwa wasindikizaji huku akitangaza kuwa Singida Magharibi wamemuelewa na hivyo watakuwa naye.
Mbunge Josephat Kandege wa Kalambo amesema kazi waliyompa wananchi chini ya CCM imekwenda vizuri na kwamba anaamini hana deni kwa wananchi wake.
Hata hivyo, Kandege aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) amezungumzia suala la nyongeza ya fedha ya Serikali kwamba zikitumika bila utaratibu mzuri zitawaumiza wengi.
Amesema fedha za nyongeza hazijapelekwa kwa ajili ya kuzigawana na kutumika vibaya kama wafanyavyo mataifa mengine badala yake wananchi waamini zinasimamiwa vizuri na tija itaonekana chini ya wawakikishi wao waliopo sasa anaoamini watarejesha tena.
Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruholo ameomba gari la zimamoto katika wilaya yake ili kumwezesha arudi tena kwenye kiti chake.

Mbunge wa Handeni Mjini (CCM), Ruben Kwagilwa
Alipojibiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuwa gari litanunuliwa, Mbunge huyo amesema:“Hayo ndiyo majibu sahihi niliyoyangoja, yamekuja kwa wakati muafaka katika kipindi hiki cha muhimu sana.”
Wabunge Stephen Byabato (Bukoba Mjini) na Joseph Kakunda (Sikonge) wao wanataja kete yao ya kuwarudisha tena kwenye nafasi zao ni kazi zilizofanywa na Rais Samia kwamba, watawaambia wapiga kura kuwa wanastahili kurudishwa kwa hilo.
Byabato aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki amesema hadi sasa wananchi wa Bukoba wameshajua anayerudi tena bungeni ni mtu anayeitwa Byabato na hakuna mbadala wake hata watu wanajua hilo.
Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka amehoji kwa nini Serikali isitumie utaratibu wa kuratibu na kutekeleza ahadi za viongozi wakuu nchini ili zisionekane ni za uongo na kwamba zitakwenda kuwasaidia kurejea madarakani.
Mawaziri nao wakatia neno
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Februari 11, 2025 amesema matamanio yake ni kuona wabunge wote waliopo sasa wakirudishwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa.
Mchengerwa amesema kazi nzuri walizozifanya wabunge hawana zawadi nzuri ya kupewa isipokuwa wapiga kura waendelee kuwaamini na kuwapa nafasi tena,“kwani hawa wabunge wamefanya kazi kubwa na nzuri.”
Mchengerwa ambaye pia ni mbunge wa Rufiji amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kupanga ratiba ya uzinduzi wa miradi mbalimbali iliyosalia kwa kushirikisha wabunge waliochangia utekelezaji wake.
“Sasa kwa kuwa tunayo miradi mingi ambayo bado haijafunguliwa, wabunge hawa wamefanya kazi nzuri. Nitumie fursa hii kuwaelekeza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri sasa kuwapangia wabunge hawa miradi yote ambayo haijazinduliwa. Waende mara moja katika majimbo yetu yote 215.”
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba yeye amesema wizara yake imepata ushirikiano mkubwa na kamati pamoja na wabunge hivyo analiona Bunge la 12 ni la maendeleo.
“Tumefanya kazi kwa mashirikiano makubwa kati ya Wizara ya Fedha, Kamati za Bunge na wabunge wote, ningetamani Watanzania wawarudishe wabunge hawa wote ili waje waendelee kuwatumikia Watanzania kwa awamu nyingine,” amesema Dk Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi.