
Wakati wajumbe wa mkutano mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) wakikutana jijini Addis Abba nchini Ethiopia kwa ajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa tume hiyo, matumaini ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ya kupata uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika yameingia shakani.
Hiyo ni kufuatia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuziandikia nchi wanachama 16 ikizikiomba kumuunga mkono Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato kwa mujibu wa BBC.
Nafasi hiyo imekuwa ikishikiliwa na Mousa Faki, raia wa Chad tangu mwaka wa 2017.
Tayari Odinga aliyesindikizwa na Rais William Ruto, ameshafika kwenye mikutano inayondelea jijini Addis Ababa, kwa mujibu wa televisheni ya Nation (NTV) ya Kenya.
Uchaguzi wa AUC umepangwa kufanyika Februari 2025 wakati wa mkutano mkuu wa AU utakaofanyika makao makuu ya umoja huo, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Pamoja na sekretarieti ya SADC kutoa ombo hilo, bado haijabainika kuwa litakubaliwa au la katika upigaji wa kura utrakaofanyika kwa simu.
Angola, Botswana, Comoros Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, South Africa, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Kati ya nchi hizo, Tanzania na DRC pia ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anakotoka Raila.
Umoja wa Afrika umetoa majina ya wagombea wanne wanaowania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Mbali na Raila, wagombea wengine ni Richard James Randriamandrato (Madagascar) na Mahamoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, huku aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius, Anil Kumarsingh Gayan akijitoa katika nyang’anyiro hicho.
Wagombea uenyekiti
Raila Odinga (79) ni kiongozi wa upinzani nchini Kenya na amewahi kuwa Waziri Mkuu wan chi hiyo.
Ameshajaribu kuwania urais wa Kenya na kushindwa mara tano – ya mwisho katika uchaguzi wa 2022 ambapo alishindwa na Rais William Ruto.
Uamuzi wake wa kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa wa Afrika bila shaka utafuatiliwa kwa karibu kote barani.
Odinga ni mwanasiasa mkongwe ambaye anasifika kupigania mageuzi ya kisiasa nchini Kenya, harakati ambazo zilimfanya kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 wakati wa utawala wa rais wa pili wa Kenya Hayati Daniel arap Moi.
Mahmoud Ali Youssouf (58) amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo lakini lenye umuhimu wa kimkakati katika eneo la upembe wa Afrika tangu 2005.
Amekuwa mtumishi wa umma wa muda mrefu, kabla ya kushika wadhifa wa sasa, hivyo kutokuwa na umaarufu mkubwa.
Anajivunia kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha tofauti na ana imani kuwa uwezo huo wa mawasilaino utamwezesha kuwa daraja litakalounganisha maeneo ya kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
Richard James Randriamandrato, ni Waziri wa Mambo ya Nje wa wa zamani wa Madagascar, ambaye alifutwa kazi Oktoba 2022 kwa kulipigia kura azimio la Umoja wa Mataifa lililolaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, wakati nchi yake ikiwa na msimamo wa kutounga mkono upande wowote.
Mbali na wagombea uenyekiti, pia kuna wagombea unaibu mwenyekiti wakitokea nchi za Algeria (wawili), Misri, Livya, Morocco.
Gachagua amwombea kura Raila
Akiandika katika mtandao wa Facebook, aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigath Gachagua amemtakia ushindi Railaa akisema yeye ndiye chaguo bora zaidi kwa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
“Afrika inastahili kilicho bora. Hakuna shaka kuhusu mtazamo wake wa kimataifa na juhudi zake za kuwatetea watu wa Afrika.
“Kama bara, tunahitaji mtu wa haiba kama Raila Odinga ili kuunganisha Afrika ya Anglophone na Francophone kuelekea mustakabali mzuri wa bara letu,” ameandika.