Hofu AI kuwafanya Watanzania mazezeta

Akili Mnemba ama Artificial Intelligence (AI) kwa lugha ya kiingereza, ni teknolojia ambayo inazungumzwa sana kwenye vyomba vya habari kwa sasa.

Umaarufu wake kwa sasa unaendelea kupata nguvu, kutokana na uamuzi wa mataifa makubwa kuiweka katika ajenda zao kama moja ya sekta inayotakiwa kutazamwa na kufanyiwa kazi.

Kwa mtu anayefuatilia masuala ya teknolojia au hata mwenye uelewa mdogo tu wa matumizi ya kompyuta, atakubaliana na mimi kuwa hii siyo teknolojia mpya, bali maboresho ya kile ambacho kimekuwepo tangu awali.

Kumekuwepo na Google ambayo imekuwa msaada mkubwa sana kwa wanaotafuta habari mtandaoni au hata mada mbalimbali za masomo.

Tofauti na zamani, kwa sasa teknolojia hii imepewa kipaumbele sana na hasahasa ujio wa kampuni ambazo zinajitanabahisha kujihusisha moja kwa moja na masuala ya akili mnemba.

Kwa sasa kuna kampuni nyingi lakini zilizo maarufu zaidi ni pamoja na ChatGPT, DeepSeek, OpenAI, NVIDIA na nyingine nyingi ambazo malengo yake si tofauti na yaliyokuwa malengo ya kuanzishwa kwa Google.

Kinachoyatofautisha kampuni hizi na Google ni maboresho makubwa yanayoambatana na wingi wa taarifa zinazopatikana ndani ya muda mfupi sana.

Aidha taarifa hizi kupitia kizazi hiki kipya cha Akili Mnemba ni kwamba, inakuletea kile unachokitaka na kwa namna ambayo kinatakiwa kuwa.

Hii ni tofauti kidogo na Google ambayo inakupa taarifa za jumla, hatua ambayo inakulazimisha uendelee kutafuta kile unachokitaka.

Hili la matumizi ya Akili Mnemba yenye kiwango kikubwa cha ufanisi, siyo jambo baya hata kidogo.

Ni zuri na kwa tafsiri rahisi tu kwamba inakusaidia kutatua jambo kwa muda mfupi na pengine kwa ufanisi mkubwa tofauti na ambavyo ingekuwa kama ungetumia muda na akili yako binafsi.

Pengine ni kutokana na ufanisi huu na wepesi wa kupata taarifa, kampuni kubwa Za teknolojia zimesukumwa kuwekeza mabilioni ya fedha katika kuiboresha teknolojia ya kizazi kipya cha Akili Mnemba.

Changamoto za Akili Mnemba

Hata hivyo, kama ilivyo kawaida katika dunia hii kwamba, hakuna jambo lenye mazuri pake yake bila kuwa na changamoto zake. Akili Mnemba inaonekana kupokelewa vyema na watu binafsi, taasisi pamoja na mataifa mengi tu kwa ujumla.

Hapa kwetu Tanzania, nimewahi kusikia kiongozi wa taasisi moja kubwa akisisitiza matumizi ya akili mnemba.

 Aidha kumekuwa na ushauri kwa mawakili juu ya kujikita katika matumizi ya akili mnemba ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.

Pamoja na msisitizo huu wa matumizi ya teknolojia hii, nina shaka kama tunaipokea kama fursa au suluhisho la mikwamo yetu. Kama tunaipokea kwa maana ya fursa ya kuongeza ufanisi na hatimaye kutengeneza fursa zaidi, sina tatizo na mapokeo hayo hata kidogo.

Lakini, kama tunaipokea teknolojia hii kama suluhisho la kuziba udhaifu wetu ya kukosa ufanisi, basi nina shaka kubwa kama  tunaielewa dhana ya ujio wake.

Nichukue mfano mmoja tu wa matumizi ya teknolojia hii kwenye shughuli za uwakili hapa Tanzania.

Pamoja na umahiri mwingine wowote ambao Wakili anatakiwa kuwa nao, umahiri wa uandishi na uandaaji wa nyaraka zenye sura ya kisheria, ni sifa kubwa anayotakiwa kuwa nayo wakili.

Umahiri huu, haupatikani kwa kunakiri maandiko ya wengine, bali unapatikana kwa wewe mwenyewe kujipa kazi ya kuandika hicho unachotakiwa kuandika.

Sasa tunadhani uwepo wa akili mnemba, utaendeleza hii hali ya wakili kutaka kujijengea umahiri kwa kuandaa andiko lake mwenyewe? sidhani.

Maadam anaweza kupata chochote kupitia akili mnemba, sioni kama wakili huyu atajisumbua kukaa na kufikiri kutengeneza mfumo wake mzuri wa kiuandishi; atatumia akili mnemba imletee kisha yeye ataingiza majina na sahihi yake tu. Huku ni kutumia akili za watu wengine.

Tunachotakiwa kufahamu ni kwamba, taarifa tunazozipakia mitandaoni, ndizo hizo hizo ambazo ukiamuru akili mnemba ikuletee taarifa inayofanana na hiyo, basi itaitafuta kwa muda mfupi kokote duniani na kukupatia.

Kimsingi, matumizi ya akili mnemba, ni matumizi ya akili na ubunifu wa watu wengine, na kwa kufanya hivyo, tunakwenda kufifisha kama siyo kuua kabisa uwezo wetu wa kufikiri.

Utafika muda, hatutaweza kuwaza chochote na badala yake tutasubiri kampuni makubwa za teknolojia zituletee majibu kwa maswali ambayo tulitakiwa kuyajibu sisi wenyewe kwa kutumia akili zetu.

Aidha, matumizi ya akili mnemba yanakwenda kuondoa uhitaji wa watoa huduma, hasa za kiuandishi kwa sababu kila kitu kitapatikana kupitia teknolojia hiyo. Taaluma nyingi zitafutika na ukuaji wa fikra na bunifu mpya utazorota kwa kiwango kikubwa.

Tutatengeneza kundi dogo la watu wanaotakiwa kufikiri kwa niaba yetu, huku sisi tukibaki mazezeta wa kumeza kila tunacholetewa.

Pamoja na faida zote za teknolojia hii, mimi ninaiona hatari kubwa mbele hasa kwa mataifa yetu haya ya Afrika ambayo kwa sehemu kubwa yamekuwa walaji wa teknolojia za mataifa yaliyoendelea.

Sina uhakika kama kuna wanaoitazama teknolojia hii kwa namna ninavyoitazama mimi, kama wapo ni jambo la heri.

Tuipokee akili mnemba lakini tujipe tahadhari sisi wenyewe. Tutazame kizazi chetu cha tano kutokea sasa.