
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amefikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, akidaiwa kutenda makosa ya uhaini na kusambaza taarifa za uongo.
Lissu anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma jana Jumatano Aprili 9, 2025 muda mchache baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mbinga mkoani Ruvuma.
Taarifa za Lissu kudaiwa kutuhumiwa kwa uhaini na kusambaza taarifa za uongozi zimeelezwa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Aman Golugwa aliyezungumza na Mwananchi Digital kwa simu muda mfupi baada ya kuonana na Lissu leo Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
Lissu amefikishwa kituoni hapo leo asubuhi akitokea mkoani Ruvuma alikokamatwa muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbinga.
“Nimetoka kuonana naye na maofisa wa polisi wanaeleza kuwa kwa hatua za awali wanamtuhumu kosa la uhaini na kusambaza taarifa za uongo na wanakusudia kumpeleka mahakamani,” amedai Golugwa na kuongeza;
“Kwa sasa bado hawajampeleka mahakamani yupo Central, lakini jalada lake limepelekwa kwa mwendesha mashtaka wa Serikali. Katika hatua za awali polisi walivyomkamata wamemtuhumu kwa uhaini.”
Mpaka saa 8 mchana huu, Mwananchi imeelezwa kuwa Lissu alikuwa bado yupo Kituo Kikuu cha Polisi akiendelea kuhojiwa.
Alichokisema wakili
Akizungumza na Mwananchi Digital, Wakili Jebra Kambole amesema kosa la uhaini limeanishwa katika kifungu cha 39 cha Sheria ya Makosa ya Jinai au Kanuni ya Adhabu.
Kambole amefafanua kuwa katika sheria hiyo, imeeleza kosa la uhaini litatendwa na mtu yeyote ambaye ana kiapo cha utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye atafanya mauaji au kujaribu kumua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Au ataanzisha vita, huyo mtu akikutwa na hayo makosa anahukumiwa kunyongwa hadi kufa. Lakini kuna watu wengine wanaweza kutenda kosa la uhaini, lakini lazima awe chini ya kiapo cha utii ambaye atasaidia kushauri wenzake au kundi la watu kufanya mipango ya mauaji ya Rais.”
“Mbali na hilo mtu yeyote ambaye atachukua njia zozote za kutaka kuiondoa Serikali iliyoko madarakani au kuitishia Jamhuri, Bunge au mahakama atakuwa ametenda kosa la uhaini,”amesema Kambole.
Kambole amesema hata kama mtu una kiapo cha utii lakini ukaanza mipango ya kusaidia majeshi ya nchi kwa kutuma taarifa ili kuivamia Tanzania, utakuwa umetenda kosa la uhaini huku akikazia kuwa uhaini ni kosa lisilokuwa na dhamana endapo utakamatwa.
Katika hatua nyingine, Golugwa amesema chama chao kinakemea hila zinazofanywa ili kukififisha chama hicho, wakitaka mambo ya siasa yaachwe kwa vyama vya siasa vipambane kwenye majukwaa kwa hoja.
“Wasifanye hujuma kwa lengo la kukibeba chama tawala. Siasa kuna lugha zake ambazo Jeshi la Polisi wanapaswa kukaa pembeni. Watuache wanasiasa, wasitupangie maneno ya kuzungumza na wasiingilie mambo yasiyowahusu,” amesema.
Mawakili 240 waandaliwa kumtetea Lissu
Katika kuhakikisha haki inapatikana kwa mwenyekiti wa chama hicho, Golugwa amesema timu ya mawakili zaidi ya 200 wameandaliwa kwa ajili ya kumtetea Lissu katika makosa anayodaiwa kuyatenda.
Amesema timu hiyo itawahusisha mawakili wa ndani na nje ya nchi akiwamo, Wakili Robert Amsterdam na wengine watakaoongozwa na Dk Nshala Rugemeleza ambaye ni mkurugenzi wa sheria wa chama hicho.