
Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids ameonyesha matumaini katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Masry.
Davids alikiri timu yake ilifanya makosa yaliyoigharimu, lakini anaamini bado ina nafasi ya kupindua matokeo nyumbani kwa Mkapa huku akitaja njia zitakazowavusha kwenda nusu fainali.
Simba ambayo ilipoteza mchezo huo uliofanyika Jumatano hii kwenye Uwanja wa New Suez, Misri, ina dakika zingine tisini za kujiuliza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, Jumatano ijayo Aprili 9 na inahitaji ushindi wa uwiano mzuri wa mabao ili kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
“Tulianza vizuri lakini hatukuweza kutumia nafasi tulizopata. Tulimiliki mpira kwa asilimia 59, tulipiga mashuti 18 dhidi ya saba yao, lakini ukosefu wa umakini umetugharimu,” alisema kocha huyo.
Licha ya Simba kuwa na takwimu bora kwenye umiliki wa mpira na pasi sahihi kwa asilimia 83, bado walishindwa kuwa na ufanisi katika kumalizia mashambulizi. Al Masry walitumia mbinu zao kwa uangalifu, wakijilinda vyema na kushambulia kwa kushtukiza.
“Tumeona mapungufu yetu. Tulijaribu kupenya ngome yao lakini hatukuwa na maamuzi sahihi kwenye eneo la mwisho. Tunapaswa kurekebisha hili kabla ya mchezo wa marudiano,” aliongeza kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Simba walipata kona tano dhidi ya moja ya Al Masry, wakionyesha dhahiri walikuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo. Hata hivyo, timu hiyo haikutumia mipira ya kona ipasavyo kupata mabao.
Katika mchezo wa marudiano, Davids alisema Simba italazimika kuanza kwa kasi na kuhakikisha wanapata bao la mapema ili kuleta msukumo wa kusawazisha matokeo.
“Hatuhitaji kuanza taratibu, tunapaswa kuwashambulia kwa nguvu tangu mwanzo,” alisema.
Mojawapo ya changamoto kubwa kwa Simba ilikuwa kushindwa kutumia nafasi zao, huku mashuti saba pekee yakilenga lango. Davids alisema wachezaji wake wanapaswa kuwa watulivu zaidi wanapofika mbele ya lango la wapinzani.
“Kama tulitengeneza nafasi nyingi ugenini, inamaanisha tuna uwezo wa kuwafunga. Tunachohitaji ni kuwa na umakini mkubwa, kujiamini na kutumia kila nafasi inayotokea,” alisema kocha huyo.
Kwa mujibu wa takwimu, Al Masry walikuwa na wastani wa matarajio ya kufunga bao 0.84 dhidi ya 0.68 ya Simba, ikionyesha kuwa walikuwa na nafasi bora zaidi za kufunga. Simba wanapaswa kuimarisha ulinzi ili kuepuka makosa yatakayowapa wapinzani nafasi za wazi.
Kwa upande wa nidhamu, Simba walipata kadi za njano tatu dhidi ya moja ya Al Masry, jambo ambalo linaweza kuathiri mbinu zao kwenye marudiano.
“Lazima tucheze kwa nidhamu, tusifanye makosa yasiyo ya lazima ambayo yanaweza kutugharimu tena,” alisisitiza Davids.
“Tunapaswa kuwa na uwiano mzuri wa kushambulia na kujilinda. Hatuwezi kuruhusu bao lingine nyumbani,” alisema.
Simba italazimika kushinda kwa mabao mawili bila majibu ili kulazimisha mikwaju ya penalti au zaidi ya hapo ili kufuzu moja kwa moja. Davids anaamini hilo linawezekana iwapo wachezaji wake watafuata maelekezo kwa umakini.
“Kupoteza ugenini si mwisho wa safari. Tumeshuhudia timu nyingi zikirejea kwenye michuano hii kwa ushindi wa nyumbani. Tunaweza kufanya hivyo pia,” alisema.
Simba inahitaji wachezaji wake hatari Elie Mpanzu, Charles Jean Ahoua na Kibu Denis kuwa katika ubora wao wa juu ili kupata matokeo yanayohitajika.
“Huu ni mpira wa miguu. Chochote kinaweza kutokea. Nawaambia mashabiki waendelee kutuunga mkono. Bado tuna nafasi ya kufanya jambo kubwa,” amehitimisha kocha huyo.