Hizi hapa faida, hasara za kula miguu ya kuku

Dar es Salaam. Kwa Tanzania, hususan jijini hapa, ulaji wa miguu ya kuku ni maarufu zaidi maeneo ya pembezoni, wengi wakipenda kuila na chachandu au kachumbari.

Kiungo hiki mara nyingi, kama zilivyo firigisi, vichwa, utumbo pamoja na shingo, huuzwa tofauti na nyama ya kuku.

Si kwamba vijijini au mikoa mingine hawali miguu ya kuku, la hasha, huko pia inaliwa lakini si kwa kiasi kikubwa kama ilivyo jijini hapa ambapo kuna biashara kubwa ya kuku wa kisasa.

Ingawa wapo wenye kipato cha kati na cha juu ambao wanakula miguu hiyo, ila kitoweo hiki ni kimbilio zaidi kwa watu wa hali ya chini.

Umewahi kujiuliza faida na hasara za miguu ya kuku? Kama ilivyo kwa vyakula vingine mlo huu umefanyiwa utafiti za kisayansi ulioainisha faida na hasara zake kwa mwili wa binadamu.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Taiwan na kutolewa Septemba 2022, ulibaini kwamba miguu ya kuku ni chanzo kizuri cha ‘collagen’.

‘Collagen’ ni protini inayopatikana kwa wingi katika mwili, mojawapo ya kazi ya yake ni kusaidia ngozi kuwa imara, laini na uzalishaji wa ‘collagen’ unapopungua husababisha dalili mikunjo ya mwili na ukavu.

Hivyo, kula vyakula vyenye ‘collagen’ ikiwemo miguu ya kuku kunaweza kusaidia ngozi kuwa angavu na kupunguza kasi ya ngozi kuzeeka na kuharakisha uponyaji wa vidonda.

Kwa mujibu wa utafiti huo kiwango cha ‘collagen’ kilichomo katika miguu ya kuku kinaweza kuongeza unyevu wa ngozi na kupunguza kuonekana kwa mikunjo, inayosababishwa na athari ya mionzi ya ‘ultraviolet B’.

‘Collagen’ pia husaidia kudhibiti maumivu na ugumu katika viungo na husaidia kupunguza athari za kupasuka kwa mifupa.

Mbali na kudhibiti maumivu ya mifupa pia inaweza kuchochea urejesho wa tishu na kumuondoa mtu kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa viungo, unaosababisha mifupa kugusana na kusababisha maumivu na uvimbe.

“Kula ‘collagen’ kunasaidia kudhibiti dalili kama ugumu, mkao mbaya na maumivu ya mgongo kwa kuongeza nguvu ya mifupa dhidi ya kuvunjika. Mbali na kuboresha unyevu wa ngozi yako, ‘collagen’ iliyomo katika miguu ya kuku inaweza pia kuboresha ukali, ustahimilivu na msongamano wa ngozi yako,” umeeleza utafiti huo.

Hakuna jema lisilo na baya, mtaalamu wa lishe kutoka taasisi UM Surabaya nchini Indonesia, Tri Kurniawati ametahadharisha kuwa ulaji uliopitiliza wa miguu ya kuku unaweza kusababisha athari za kiafya kwa mlaji.

Amesema gramu 100 za miguu ya kuku sawa na miguu mitatu hadi minne zina gramu 5.5 za mafuta hatari kwa mwili, ambayo ni asilimia 60 ya mahitaji ya kila siku ya mtu mzima.

Pia kiwango hicho hicho cha gramu 100, kina cholestro miligramu 84, ambayo ni asilimia 20 ya mahitaji ya kila siku ya mtu mzima.

“Kama utakula miguu ya kuku kwa wingi au mara kwa mara, inaweza kusababisha ongezeko la cholestro, na ikiwa hilo litaendelea, linaweza kusababisha uchovu wa mwili na mwishowe inaweza kusababisha moyo ushindwe kufanya kazi au kiharusi,” anasema Tri.

Madhara ya ulaji wa miguu ya kuku kupita kiasi yanaelezwa pia na daktari wa magonjwa ya binadamu Sadick Sizya ambaye pia ni muasisi wa jukwaa la Sauti ya Afya (VOH) lililopo Tanzania.

Dk Sizya amesema ulaji wa mara kwa mara wa miguu ya kuku huweza kumsababishia mtu kupata unene kupita kiasi kutokana na mafuta yaliyo kwenye ngozi ya miguu hiyo.

“Kwa kawaida ngozi ya kuku ina mafuta, ni aghalabu kukuta mtu anakula miguu ya kuku akakumbuka kutoa ngozi, ataila kama ilivyo. Na bahati mbaya wengi hula zaidi ya mguu mmoja, sasa kama mtu huyu atakuwa anakula miguu mingi mara kwa mara mafuta yote hayo yatakuwa mwilini.

“Kingine ambacho si kizuri kukila kwa kuku ni shingo, kwenye shingo kuna tezi ambayo kazi yake ni kumlinda dhidi ya bakteria, sasa kuna uwezekano hao bakteria wakawepo kwenye shingo au wakaacha sumu inayoweza kusababisha magonjwa kwa mlaji,”amesema.

Daktari huyo amesema wakati mwingine hata vifo vya ghafla ya vijana vinatokana na ulaji wa vitu visivyofaa, ambavyo madhara yake hayaonekani ndani ya muda mfupi.