
Katika mambo ambayo mashabiki wa soka wanapenda kuyaona kwenye Kariakoo Dabi Jumamosi hii, basi nyavu kutikiswa tena ikiwezekana kwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa Novemba 5, 2023 Yanga iliposhinda 5-1 dhidi ya Simba.
Kumbuka kuna msemo unasema ‘raha ya mechi bao’ unaosindikiza matamanio hayo ya mashabiki.
Sasa basi, Kariakoo Dabi ambayo inakwenda kuwakutanisha Yanga na Simba Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, kila mmoja amekuwa akizungumza lake huku asilimia kubwa wakitabiri itakuwa ya mabao.
Yanga inajivunia rekodi ya kuitambia Simba katika mechi nne mfululizo zilizopita huku ikitaka kuendeleza ubabe wake na kujitanua zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi na pointi zake 58 wakati Simba ina 54.
Ukiangalia dabi zao mbili za mwisho ambazo zote Yanga imeshinda, haikuwa na mabao mengi na matokeo yalifanana yakiwa ni 1-0, lakini namna safu za ushambuliaji za timu hizo zilivyo kwa sasa ndiyo sababu ya kutajwa kuna uwezekano wa mabao mengi kupatikana.
Yanga iliyofunga mabao 58, Clement Mzize na Prince Dube kila mmoja amefunga 10 na wanaongoza kwenye chati ya ufungaji.
Upande wa Simba yenye mabao 46, Jean Charles Ahoua ndiye kinara wao akiwa na 10, Leonel Ateba na Steven Mukwala kila mmoja ana manane.
Takwimu zinaonyesha, Kariakoo Dabi 10 zilizopita, yalipatikana mabao 16 huku Yanga ikifaidika kuwa na 11 wakati Simba ni matano pekee.
Katika mabao hayo 11 ya Yanga, kuna moja ambalo beki wa Simba, Kelvin Kijili alijifunga ikiwa ni mchezo wa mwisho walipokutana Oktoba 19, 2024 katika Ligi Kuu Bara Yanga ikishinda 1-0.
Mabao mengine ya Yanga yamefungwa na nyota sita tofauti huku Maxi Nzengeli na Aziz Ki wakiongoza kila mmoja akifunga matatu, Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua, Joseph Guede na Zawadi Mauya wana mojamoja.
Katika dabi hii, Maxi, Aziz Ki, Musonda na Pacome, kila mmoja ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao huku Guede na Mauya kwa sasa hawapo Yanga.
Upande wa Simba, mabao yao matano katika dabi 10 zilizopita yamefungwa na wachezaji wanne tofauti huku mmoja pekee akiendelea kusalia hadi sasa ambaye ni Kibu Denis mwenye mawili. Freddy Michael Koublan, Henock Inonga na Augustine Okrah hawapo.
DAKIKA ZA MABAO
Ukiyachukua mabao hayo 16 yaliyopatikana kwenye mechi zao 10 zilizopita, 10 yamefungwa kipindi cha kwanza na yaliyobaki sita yakipatikana kipindi cha pili.
Hii inaashiria kipindi cha kwanza ndicho kimekuwa na pilika nyingi za kusaka mabao.
Hata hivyo, Yanga pia inaendelea kuwa ndiyo timu tishio zaidi kipindi cha kwanza kutokana na kufunga mabao mengi ambayo ni sita na matano cha pili. Simba kipindi cha kwanza imefunga mabao manne na moja cha pili.
Ukiachana na kipindi cha kwanza kuwa na mabao mengi, takwimu zinaonyesha dakika 15 za kwanza ndizo zina mabao mengi yakifungwa matano, kisha zile 15 za mwisho kwenda mapumziko, yamefungwa manne.
Kipindi cha dakika 15 za kwanza baada ya kuanza kipindi cha pili, hakuna bao lililofungwa na hata zile dakika za nyongeza baada ya tisini napo hakuna bao.
Kuanzia dakika ya 61 hadi 75 na 76 hadi 90, hapo kila kipindi yamefungwa mabao matatu wakati kuanzia dakika ya 16 hadi 30 likipatikana bao moja pekee.
Akizungumzia mchezo huo, Edibily Lunyamila ambaye amewahi kucheza Yanga na Simba, alisema kwake anaiona dabi ya Jumamosi haina mwenyewe kutokana na namna mara nyingi haitabiriki huku ikijaa presha kubwa.
“Unapozungumzia dabi ni mechi ambayo haitabiriki, hata Jumamosi inaweza kuwa hivyo kwani unaweza kuwa bora na ukafungwa, kwa sisi ambao tumewahi kucheza mechi hii kunakuwa na presha inaanzia nje ya uwanja kwa mashabiki hadi viongozi, sasa presha hiyo inaweza kuwaingia wachezaji na kujikuta hata kama upo vizuri unacheza vibaya,” alisema Lunyamila.