Hizi hapa ahadi za Hamdi kocha mpya Yanga

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Yanga, Miloud Hamdi amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo akitamba kuwa itaendelea kucheza soka la kuvutia, kupata matokeo mazuri na kutwaa mataji ya ndani kama walivyofanya watangulizi wake.

Hamdi aliyejiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars alisema kuwa Yanga inahitaji mataji kwa vile ni timu kubwa na yeye kama kocha atahakikisha hilo linatimia.

“Naifahamu Yanga kwa sababu imeshiriki mara nyingi mashindano ya Kimataifa ni nadra kusikia kocha anasema haifahamu hii timu ambayo tayari imevaa medali ya Caf. Imetwaa mataji mengi ya ndani makocha wengi wameandika rekodi hivyo kwangu presha kubwa ni kuipambania ifikie malengo kimataifa.

“Naheshimu makocha wote waliopita na walichokifanya, hivyo nitafanya muendelezo huku nikisaka rekodi yangu pia kwa kufanya kilicho bora zaidi, kikubwa ninachojivunia ni kuona wachezaji wengi wanacheza aina ya mfumo ninaoupenda,” alisema Hamdi.

Aliongeza kwamba, juzi alikaa na wachezaji kabla ya kuanza mazoezi na kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha hawaachi nafasi kwa wapinzani kufanya vizuri zaidi yao sambamba na kuwaambia makosa wanayopaswa kuyafanyia kazi kutokana na kile alichokishuhudia walipocheza dhidi ya KenGold.

“Nilikuwa na kikao na wachezaji wangu juzi kabla ya mazoezi, nimezungumza nao nini nataka na nimewaambia wapi walikuwa na mapungufu, tumeelewana, kilichobaki ni kufanya kazi vizuri.

“Kwa sasa hakuna muda wa kupoteza kwani ukiangalia ratiba kwa mwezi Februari imebana sana, tuna mechi mfululizo tunazopaswa kucheza.

“Wachezaji wangu wapo timamu hivyo kazi yangu haitakuwa ngumu sana, napambana kuhakikisha nawajenga kiushindani ili kufikia malengo waliyojiwekea mwanzo wa msimu kutetea mataji,” alibainisha kocha huyo.

Alisema anafurahi kuifundisha timu ambayo ipo kwenye ubora mkubwa na aina ya wachezaji waliopo ndani ya timu kwa upande wake anaamini ni muda sahihi kuipata nafasi aliyopewa atapambana kuhakikisha anaendelea kuipaisha timu hiyo kuendelea kuwa bora kwa kushinda mataji.

“Hakuna kinachoshindikana, kama mipango imetimia, Yanga ina wachezaji wengi bora na wenye uzoefu mkubwa, mbinu imara itakuwa chachu ya wao kuisaidia timu kufikia malengo wanayoyatamani muda mrefu, naamini uwekezaji mkubwa na ushirikiano mzuri na viongozi hakuna kitakachoshindikana,” alimaliza Hamdi.

Kwa sasa Yanga ipo kwenye maandalizi chini ya Hamdi ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa kesho Jumatatu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Timu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 45, moja mbele ya Simba inayoshika nafasi ya pili, inapambana kutetea taji lake ililobeba kwa misimu mitatu mfululizo.