Hizbullah yawatwanga kwa makombora wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel

Wanamuqawama wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon wamevurumisha makombora katika kambi za kijeshi mahali walipokuwa wamekusanyika wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hizbullah imetangaza katika taarifa yake kuwa: Wanamuqawama wa harakati hiyo wameitwanga kwa makombora sehemu ambayo wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walikuwa wamekusanyika katika kambi ya kijeshi ya Dofif karibu na kijiji cha Maron al Ras ikiwa ni katika kuwatetea wananchi shupavu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na huko Lebanon.  

Vita vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vimeingia katika mwezi wa 13 sasa baada ya kujiri oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa Oktoba 7 mwaka jana. Harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah inatekeleza oparesheni za kijeshi dhidi ya utawala wa Israel kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi na mapambano ya ukombozi dhidi ya maghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.  

Tangu tarehe 23 Septemba mwaka huu jeshi la utawala wa Kizayuni linafanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon.

Katika kujibu hujuma hizo za kikatili za Israel za kuwashambulia raia wa Lebanon, Harakati ya Hizbullah pia haijakaa kimya na imeweka katika ajenda yake ya kazi oparesheni nyingi dhidi ya kambi za kijeshi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.  

Mashambulizi ya Hizbullah kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel)

Hizbullah imesisitiza kuwa, kusitishwa  vita katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kunategemea kusitishwa  vita dhidi ya Ukanda wa Gaza.