Hizbullah yavitwanga kwa makombora viwanda vya kijeshi vya Israel huko Haifa

Hizbullah ya Lebanon imeendelea kutoa vipigo kwa utawala pandikizi wa Kizayuni na imevipiga kwa makombora viwanda vya kijeshi vya Israel kaskazini mwa mji wa Haifa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, jana Jumapili, Hizbullah ya Lebanon ilitangaza kuwa, imeitwanga tena kwa makombora kambi Zofolon yenye viwanda vya kijeshi vya Israel, kaskazini mwa mji wa Haifa.

Katika taarifa yake ya Sita, Hizbullah imesema kuwa, ikiwa ni muondelezo wa kuliunga mkono taifa imara la Palestina huko Ghaza na kuusaidia muqawama wa kupigiwa mfano wa wananchi mashujaa wa Palestina pamoja na kulinda ardhi Lebanon na usalama wa watu wake, wanamapambano wa Muqawama wa Kiislamu mchana wa jana Jumapili tarehe 27 Oktoba 2024 waliipiga kwa makombora kadhaa kambi ya Zofolon ya jeshi la Israel kaskazini mwa mji wa Haifa.

Mapema jana asubuhi pia, Hizbullah ya Lebanon ilifanya mashambulo kwa kulipiga kwa droni shirika la kijeshi la Israel kusini mashariki mwa Acre.

Redio ya utawala wa Kizayuni imethibitisha habari ya kushambuliwa shirika hilo la kijeshi la Israel na kusema kuwa limefanyika kwa umakini mkubwa na limepelekea wanajeshi wasiopungua wanne wa Israel kujeruhiwa.