Wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon wameshambulia kwa makombora kadhaa viwanja vya ndege vya Ben Gurion na Ramat David katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yaliyopachikwa jina bandia la Israel.
Chaneli ya Sahab imelinukuu shirika la habari la IRNA na kuripoti kuwa, televisheni rasmi ya utawala wa Kizayuni imetangaza leo kuwa, sauti ya mripuko imesikika katika mji wa Tel Aviv na uwanja wa ndege wa Ben-Gurion umefungwa.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti pia kuwa, kombora jengine limelenga uwanja wa ndege wa kijeshi wa Ramat David katika eneo la Maraj Bin Amer mashariki mwa mji wa Haifa, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa televisheni ya CNN waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alichelewa kuondoka Tel Aviv kufuatia kulia ving’ora vya hali ya hatari katika mji huo.
Kufuatia mashambulio hayo, ving’ora vya hali ya hatari vimelia pia katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Masaf Am na Kaffar Giladi katika sehemu ya mashariki ya mpaka wa pamoja na Lebanon.
Milio ya kengele za hatari imesikika pia kwenye kitovu cha Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Tel Aviv.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya kurushwa makombora hayo kuelekea Tel Aviv, Wazayuni wamejawa na hofu kubwa na kukimbilia kwenye maficho yao, ambapo kadhaa miongoni mwao wamejeruhiwa kutokana na msongamano na mrundikano.
Pamoja na kuthibitisha kuwa makombora hayo yamerushwa kutokea Lebanon, duru za Kizayuni zimedai kuwa makombora mawili yaliyorushwa kuelekea Tel Aviv yamenaswa.
Jana Jumanne Hizbullah iliweka rekodi ya kutekeleza operesheni 39 katika muda wa siku moja kulenga ngome, vikosi, shabaha, zana za kivita, vitongoji, na kambi za utawala wa Kizayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) na kusini mwa Lebanon.
Jeshi la Israel lilitangaza katika taarifa liliyotoa Jumanne usiku kwamba Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umerusha ndege zisizo na rubani na makombora 140 kuelekea maeneo ya utawala huo wa Kizayuni.
Septemba 23, jeshi la utawala haramu wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon, ambayo yangali yanaendelea.
Hizbullah ya Lebanon haijanyamazia kimya jinai za utawala wa Kizayuni za kuwalenga raia wa nchi hiyo na tangu wakati huo imeshatekeleza operesheni kadhaa za mashmbulio dhidi ya ngome na vituo vya utawala wa Kizayuni…/