Wapiganaji wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon wameiangusha ndege ya kivita isiyo na rubani ya jeshi katili la Israel kusini mwa Lebanon sambamba na kuvurumisha makombora katika maeneo ya kijeshi ya Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ili kulipiza kisasi jinai zinazoendelea za utawala wa Tel Aviv dhidi ya Ukanda wa Gaza na Lebanon.
Hizbullah imesema katika taarifa fupi siku ya Jumanne kwamba wapiganaji wake katika kitengo cha ulinzi wa anga walitungua ndege kubwa ya kivita isiyo na rubani ya Israel ijulikanayo kama Elbit Hermes 450.
Imebainisha kuwa operesheni hiyo ya Jumanne ilifanywa kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina walio na msimamo thabiti katika Ukanda wa Gaza pamoja na makundi shujaa na yenye heshima ya muqawama huko, na kwa ajili ya kuilinda Lebanon na watu wake.
Kundi hilo la muqawama la Lebanon pia limesema wapiganaji wake walilenga mjumuiko wa wanajeshi wa Israel karibu na kituo cha kijeshi cha al-Marj kwa msururu wa maroketi.
Katika wiki za hivi karibuni, Israel imeendeleza mashambulizi yake ya anga ya umwagaji damu huko Lebanon, na kusababisha kuhama angalau watu milioni 1.3, zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu wa nchi hiyo.

Kulingana na Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon, takriban watu 2,309 wameuawa na wengine 10,782 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Lebanon tangu mapema Oktoba 2023.
Katika kipindi hicho utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na kuua Wapalestina wasiopungua 42,344 na wengine 99,013 kujeruhiwaw ,engi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Hizbullah imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya ngome za Israel na kuapa kuendelea kupigana hadi utawala huo utakapomaliza uchokozi wake dhidi ya Lebanon na Gaza.