
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefanya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel, ikilenga maeneo ya ndani kabisa ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Katika mojawapo ya operesheni zake usiku wa kuamkia leo, Hizbullah imelenga Kituo cha Navel huko Haifa kwa mamia ya makombora. Mashambulizi hayo yametajwa kuwa ni ya aina yake tangu kuanza kwa uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon.
Kambi nyingine kadhaa za Israel zikiwemo Mishar, Shraga na Doviv pia zimepigwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani za Hizbullah.
Hizbullah pia imeharibu vifaru sita vya Israel aina ya Merkava katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na huko Deir Mimas na Bayyada.
Mikusanyiko kadhaa ya wanajeshi wa Israel pia imepigwa kwa silaha za Hizbullah.
Vyombo vya habari vya Israel vimeyataja mashambulizi hayo mapya ya Hizbuullah kuwa hayajawahi kutokea tangu Oktoba mwaka jana.
Vyombo vya habari vya Israel pia vimeripoti kuwa milipuko ilisikika katikati mwa Tel Aviv kutokana na kutua kwa makombora yaliyorushwa kutoka Lebanon.