Hizbullah yalenga Tel Aviv, Haifa; yazindua kombora jipya lenye usahihi mkubwa

Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imeishambulia miji ya Tel Aviv na Haifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya Kamikaze. Aidha Hizbullah imezindua kombora jipya lenye usahihi mkubwa ambalo litatumiwa katika mapambano yake yanayoendelea dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Hizbullah imesema kuwa imetekeleza mashambulizi yaliyofanikiwa ya anga ya kulipiza kisasi dhidi ya kikosi cha ndege zisizo na rubani katika uwanja wa ndege za kivita wa Belo unaotumiwa na kikosi cha askari wa akiba wa kitengo cha 98 cha jeshi la Israel kusini mwa Tel Aviv. Hi ni mara ya kwanza kwa ngome hiyo ya kijeshi kulengwa.

Hizbullah imesema imefanya operesheni hiyo kama sehemu ya mfululizo wa operesheni za Khaybar chini ya kauli mbiu inayosema: “Tuko katika Huduma Yako Ewe Nasrallah,” akimaanisha katibu mkuu wa zamani wa harakati hiyo Sayyed Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa shahidi wakati wa mashambulizi makali ya anga ya Israel dhidi ya Lebanon, mji mkuu Beirut mwishoni mwa Septemba.

Hizbullah imesisitiza kuwa operesheni hizo za kulipiza kisasi ni katika “kuunga mkono watu wetu thabiti wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na kuunga mkono mapambano yao ya kijasiri na ya heshima, na pia ni kwa ajili kuilinda Lebanon na watu wake.”

Hizbullah imefanya mamia ya mashambulizi hayo tangu Oktoba mwaka jana, wakati utawala huo ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza na kuzidisha uchokozi wake mbaya dhidi ya Lebanon.

Mashambulizi hayo ya kikatili hadi sasa yamepelekea Wapalestina 43,391 kupoteza maisha wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, huku mashambulizi dhidi ya Lebanon yakisababisha vifo vya takriban watu 3,050.