Hizbullah yaishambulia tena Tel Aviv kwa makombora, droni zake zawa jinamizi kwa jeshi la Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, imezishambulia tena kwa makombora ngome na vituo vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Tel Aviv.

Ripoti zinasema, sambamba na kutua katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv ndege iliyobeba wanasoka wa timu ya Maccabi ya Israel, sauti za miripuko mikubwa ilisikika mjini humo, ving’ora vya tahadhari ya hali ya hatari vikalia na uwanja huo wa ndege ukafungwa.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, ving’ora vya hali ya hatari vilisikika katika mji wa Tel Aviv na maeneo mengi ya kaskazini na katikati mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel, yakiwemo ya Acre, Wadi Areh, Nahariya na Al-Jalil.

Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Kiebrania vimekiri kuwa ndege zisizo na rubani za Hizbullah zinapenya katika maeneo hayo na kuripoti kuwa jeshi la Kizayuni limeshindwa kukabiliana na ndege hizo zisizo zinazorushwa kutokea Lebanon.

Kuhusiana na hilo, Hizbullah ya Lebanon imetoa taarifa ikieleza kuwa, imeshambulia eneo walipowekwa askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni mashariki mwa kijiji cha Maroon al-Ras.

Itakumbukwa kuwa Jumatatu ya tarehe 23 Septemba 2024, jeshi la Kizayuni lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon, ambayo yangali yanaendelea hadi sasa.

Hizbullah ya Lebanon haijanyamazia hujuma na mashambulio hayo ya kinyama ya jeshi la Israel yanayowalenga raia wa nchi hiyo; na kuanzia wakati huo imekuwa ikifanya operesheni nyingi za mashambulio dhidi ya ngome na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, mbali na kuzilenga kwa mamia ya makombora ngome za jeshi la utawala wa Kizayuni…/