Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imeshambulia kwa makombora vitongoji vinne vya walowezi wa Kizayuni vya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu imevipiga kwa makombora vitongoji vinne vya walowezi wa Kizayuni kikiwemo cha Kiryat Shmona huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Vile vile Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa, mashambulizi hayo ya makombora dhidi ya vitongoji hivyo vya walowezi wa Kizayuni yamefanyika ikiwa ni kutekeleza onyo ililolitoa huko nyuma la kuwataka wakaazi wa vitongoji hivyo wahame kwenye maeneo hayo. Huko nyuma Hizbullah ya Lebanon ilikuwa imetoa onyo kuwa itavishambulia vitongoji 25 vya walowezi wa Kizayuni na kuwataka Wazayuni wanaoishi kwenye maeneo hayo wahame haraka iwezekanavyo.

Jumatano ya jana, Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon ulifanya oparesheni 32 za kushambulia vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, vituo vya kijeshi, zana za kijeshi na maeneo mengine muhimu ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni.
Tangu tarehe 23 Septemba, jeshi la Kizayuni limekuwa likifanya mashambulizi makubwa kwentye maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon.
Katika kujibu jinai hizo, Hizbullah ya Lebanon imefanya oparesheni nyingi dhidi ya maeneo na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni hasa maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel na inaendelea kuusababishia hasara kubwa utawala huo pandikizi.