Hizbullah: Kukimbia Israel kusini mwa Lebanon ni ishara ya udhaifu wa Wazayuni

Msemaji wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kukimbia wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika maeneo ya kusini mwa Lebanon ni ushahidi tosha wa udhaifu, kufeli na kushindwa wanajeshi hao na Muqawama wa Kiislamu.

Mohammad Afif alisema hayo jana (Jumatatu) mbele ya waandishi wa habari waliotaka kujua hali ilivyo hivi sasa katika mapambano ya kusini mwa Lebanon na kuongeza kuwa, Hizbullah iko imara na inaendelea na mapambano ya kishujaa ya kulilinda taifa la Lebanon na kuwaunga mkono Wapalestina na kwamba ushahidi wa hilo ni jinsi wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni walivyokimbia kwa madhila na kutoka kwenye ardhi za kusini mwa Lebanon.

Akijibu swali la mwandishi wa shirika la habari la Tasnim mjini Beirut, Afif amesema kuwa utawala wa Kizayuni umeongeza mashambulizi yake ya anga dhidi ya maeneo ya Lebanon lakini wakati huo huo majeshi yake mawili yamekimbia kusini mwa Lebanon na huu ni ushahidi wa wazi wa udhaifu, kufeli na kushindwa jeshi la Israel hasa katika mistari ya mbele ya vita vya ardhini. 

Amesema, wanamapambano wa Kiislamu wanaendelea kutoa vipigo vikali kwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni ambao wameshindwa kuiteka na kuikalia hata sehemu ndogo tu ya ardhi ya Lebanon licha ya majigambo makubwa wanayotoa mbele ya vyombo vya habari.

Ameongeza kuwa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameamua kushadidisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya Lebanon hasa kusini mwa Beirut, ili kuficha fedheha ya kushindwa kwao vibaya kusini mwa Lebanon.