Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah imesema utawala wa Kizayuni wa Israel umemimina “makombora yaliyosheheni mabomu ya vishada” kwenye vitongoji vya kusini mwa Lebanon.
Mabomu ya vishada yamepigwa marufuku duniani kote kwa sababu yanasababisha madhara ya papo kwa papo na ya muda mrefu kwa raia.
Harakati ya Hizbullah imeeleza katika taarifa kwamba jeshi la utawala wa Kizayuni limeshambulia maeneo ya Hanin na Tiri, katika wilaya ya kusini mwa Lebanon ya Bint Jbeil, kwa makombora yaliyosheheni mabomu ya vishada.
Taarifa ya Hizbullah imeendelea kueleza: “hatushangazwi hata kidogo na jinai hii mpya ya kinyama, ambayo imeongezwa kwenye rekodi ya uhalifu wa Israel dhidi ya watu wa Lebanon na Palestina.”

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, hii si mara ya kwanza kwa jeshi la utawala wa Kizayuni kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku dhidi ya raia wa Lebanon. Mnamo mwaka 2006, utawala huo haramu ulitumia mabomu ya vishada yaliyovurumishwa kwa kutumia makombora ya mizinga katika maeneo yenye watu wengi nchini humo wakati wa vita vyake vya siku 33 dhidi ya Lebanon.
Kwa mujibu wa mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, mwezi Oktoba mwaka jana pia, vikosi vya jeshi la utawala ghasibu wa Israel vilitumia mabomu yenye fosforasi nyeupe viliyopatiwa na Marekani katika mashambulizi yao dhidi ya Ghaza na Lebanon.
Katika uchunguzi wake, Human Rights Watch pia ilithibitisha kutumiwa mabomu hayo na jeshi la Israel katika manispaa zisizopungua 17 kusini mwa Lebanon tangu Oktoba 2023, wakati lilipoanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Tangu vilipoanza vita hivyo, Marekani imekuwa ikiisaidia Israel kikamilifu katika masuala ya silaha na mabomu…/