Hizbulla yaendelea kutoa vipigo dhidi ya Wazayuni

Kitengo cha habari za kivita cha Hizbullah ya Lebanon kimetangaza kuwa harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu imeendelea kutoa vipigo na kuyatwanga kwa makombora na droni maeneo mbalimbali ya kijeshi ya Israel.

Taarifa ya jana Ijumaa ya Hizbullah imesema kuwa, ikiwa ni kuendelea kuliunga mkono taifa imara la Palestina na kusaidia Muqawama wa kishujaa wa taifa hilo kwenye Ukanda wa Ghaza pamoja na kuendelea kuilinda Lebanon na watu wake, Hizbullah imefanya mashambulizi mengine dhidi ya mkusanyiko wa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kwa kutumia makombora na droni (ndege zisizo na rubani).

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Hizbullah imefanya mashambulizi mapya dhidi ya mikusanyiko ya wanajeshi wa Israel katika eneo la Maroun al-Ras na kwenye kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Sa’sa’ cha kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Wazayuni wanaokimbia ardhi za Palestina inaendelea kuvunja rekodi kutokana na vipigo vya Muqawama

Hayo yanaripotiwa huku idadi ya walowezi wa Kizayuni wanaokimbilia nje ya ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel ikiendelea kuvunja rekodi siku baada ya siku kutokana na vipigo inavyopata Israel kutoka kwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina.

Kwa mfano katika ripoti yake ya karibuni kabisa, gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti kwamba zaidi ya walowezi 10,000 wamekimbilia Canada kutoka katika ardhi za Palestina walizokuwa wanazikalia kwa mabavu kutokana na vipigo vikali wanavyopata kutoka kwa wanamapambano wa kambi ya Muqawama.