
Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, tunawasikia baadhi ya viongozi wa kisiasa na viongozi wa dini wakiimba au kuhubiri wimbo wa amani, lakini najiuliza hivi hadi miaka hii hatujui amani ni tunda la haki?
Kwa hiyo haki katika uchaguzi wowote wa kidemokrasia ndio ambao huzaa amani ambayo ni kama yai, likidondoka na kupasuka huwezi kuliunganisha likarudi kama lilivyokuwa na ili uchaguzi uwe wa haki unaanzia kwenye mifumo ya uchaguzi.
Tunapozungumzia mifumo ya uchaguzi tunaanzia kwenye Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni za uchaguzi kama hazifanyi uchaguzi ukawa wa haki, huru na unaokubalika, basi ni wazi huyo mtoto “Amani” tunayemlilia hawezi kuzaliwa.
Ukisoma utangulizi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yam waka 1977 inasema sisi Wananchi wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchiyetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.
Inasema misingi hiyo itatekelezwa tukiwa na Mahakama huru zinazotoa haki bila woga wala upendeleo wowote ili kuhakikisha haki zote za binadamu zinalindwa na zinadumishwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu mkubwa.
Ukisoma pia ibara ya 107A (1) ya Katiba inasema mamlaka ya utoaji haki katika hapa Tanzania itakuwa mikononi mwa mahakama na hakuna chombo cha Seriikali wala cha Bunge kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.
Sasa ukija kwenye Ibara ya 41(7) ya Katiba hiyo hiyo ya Tanzania inasema iwapo mgombea urais ametangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.
Maana yake hata kama uchaguzi wake haukuwa huru na haki na hata kama kuna ushahidi madhubuti (strong evidence) wa wizi wa kura, udanganyifu na kugushi nyaraka zilizompa ushindi, ushindi wake hauwezi kuhojiwa mahakamani.
Huku tunasema mahakama ndio chombo cha mwisho cha utoaji haki katika ardhi ya Tanzania, hapo hapo tunaifunga mikono kusikiliza malalamiko ya uchaguzi katika nafasi ya urais, na bado wanasiasa na viongozi wetu wa dini hawalioni hili.
Lakini ibara yenye maudhui kama hayo unaikuta kwenye Ibara ya 74(12) inayoanzisha Tume ya Uchaguzi ambayo sasa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 2024, inaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi au INEC.
Ibara hiyo ndogo ya (12) ya Katiba yetu inasema hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hiyo.
Unajiuliza, inakuwaje chombo kama INEC ambacho wajibu wake wa msingi ni kutenda haki kwa kuendesha chaguzi huru, haki na zinazoaminika kinawekewa kinga ya aina hii na bado hatuoni tatizo katika mifumo yetu ya uchaguzi.
Hata ile namna ambayo Rais ambaye kwa utamaduni wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiye huyo huyo anakuwa mwenyekiti wa chama, kuteua mwenyekiti na makamu mwenyekiti na watendaji wengine wa tume bado inaleta ukakasi.
Hao wakurugenzi wa miji, manispaa na majiji pamoja ambao hugeuka kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwenye majimbo na watendaji wa kata wanakuwa wasimamizi wa wasaidizi na wapo wanaojulikana kwa majina ni makada wa CCM.
Yaani mwenyekiti wa chama cha siasaa kinachoshindana na vyama vingine vya siasa ndiye anayeteua mtendaji mkuu wa chombo kinachopaswa kusimamia uchaguzi, hii haina tofauti na refa mchezaji kwa maana anaamua kila kitu.
Ndio maana kwa waliosoma Cuba wanaelewa hata ile kauli ya waziri kuwa anayeamua nani ashinde sio sanduku la kura ni anayehesabu na kutangaza matokeo, sio ya bahati mbaya, kwani ni sawa na mlevi anayesema ukweli akilewa.
Kwa hiyo siku zote ukiwa na Katiba yenye vipengele vinavyominya haki kwenye uchaguzi, automatically (moja kwa moja) inakwenda kuzaa Sheria na mifumo ya uchaguzi inayonyima haki na kukinufaisha chama kilichopo madarakani.
Mwandishi wa vitabu, William Scott Downey anasema “Law without justice is a wound without cure”, akimaanisha sheria bila haki ni jeraha lisilo na tiba, kwa hiyo tunapaswa kuililia zaidi haki ili izae amani kwa mustakabali mwema wa taifa letu.
Bahati mbaya sana, sielewi ni kwa kutoelewa au ni makusudi ama ni kwa maslahi, baadhi ya viongozi wa kisiasa na wale wa Dini wanaohubiri amani, kwao neno haki limekuwa ni msamiati mgumu kuuelewa na hata wakielimishwa hawaelewi.
Wamekariri tu “tunataka amani” au “kuna vyama vinataka kuvuruga amani yetu” ama “hatutakubali amani yetu ivurugwe”, wanashindwa kuelewa kuwa bila haki machafuko ni dhambi ya kukandamiza haki katika taifa lolote la kidemokrasia.
Mhariri, mwanasiasa na mwandishi wa vitabu wa Marekani, William Allen White (1868-1944), aliwahi kusema “peace without justice is tyranny”, akimaanisha amani bila bila haki ni udhalimu, hivyo tunapaswa kuhubiri ni haki kwanza.
Ukimuacha huyo lakini Papa Paul VI naye alipata kusema “if you want peace, work for justice”, kwamba kama unataka amani, shughulika na haki kwanza na ndio maana ninawasihi watanzania tupiganie haki katika chaguzi ili tupate amani.
Katika hili, nawasihi sana watanzania, tusikubali kuyumbishwa na propaganda kwani hata kilio cha vyama vya siasa kwa sasa ni juu ya mifumo ya uchaguzi isiyotoa haki kwa vyama vya upinzani, wala havina nia ya kuleta machafuko.
Wala tusijidanganye sana kutumia maguvu kulazimisha kwenda kwenye uchaguzi ambao tayari sheria zinaminya haki kwani nguvu ya umma ikiamua, hakuna Jeshi linaloweza kuzuia na itakuwa ni sawa na kuzuia maji ya mafuriko kwa mikono.
Hata mwaka 1917 huko Urusi, Jeshi lililokuwa na vifaa vya kisasa na wanajeshi wakakamavu lilizidiwa nguvu na nguvu ya umma na mifano ipo pia katika nchi za Tunisia, Misri na Libya, bado majeshi hayakufua damu mbele ya nguvu ya umma.
Leo hii tunaweza kubeza vuguvugu lililoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) la “no reforms no election” kwamba kama hakuna mageuzi katika sheria na mifumo ya uchaguzi hakuna uchaguzi, lakini moto wake ni mbaya.
Kwa sababu somo wanalolieneza kupitia mikutano yao ya hadhara linawaingia wananchi kwa vile wanafahamu nini kilitokea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na Uchaguzi mkuu 2025, kwani wanaona dalili ni zile zile za chaguzi hizo.
Suluhu pekee katika chaguzi zetu ni kuwa na sheria na mifumo ya uchaguzi inayotoa haki na kufanya uchaguzi uwe wa huru, haki na unaoaminika ili amani yetu iendelee kutamalaki, na bado tunao muda wa kurekebisha mapungufu.
Wala CCM isione soni kuongoza mabadiliko ya mifumo kwa sababu kwa kufanya hivyo ni mama Tanzania itashinda kwani nchi yetu itabaki salama, hivyo viongozi wa kisiasa na viongozi wa dini wahubiri haki zaidi ili iweze kuzaa mtoto “Amani”.
Binadamu wana hulka ya kusema “enough is enough”, kwamba sasa imetosha, hivyo tusiwafikishe huko Watanzania kwa sababu waswahili wana msemo kuwa sumu huwa haionjwi, nasi tusijaribu kuonja vurugu na machafuko yanayotokana na uchaguzi.