
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameshauri njia mbalimbali za kumsaidia mgonjwa wa usonji, ikiwa ni pamoja na kumpeleka kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini na kutibu tatizo hilo.
Usonji, au Autism Spectrum Disorder (ASD) ni hali ya ukuaji wa ubongo inayojumuisha changamoto katika maeneo ya mwingiliano wa kijamii, mawasiliano na tabia zinazojirudia.
Hali hii inahitaji uangalizi maalumu na msaada kutoka kwa wataalamu ili kusaidia watu wenye ugonjwa huu kufikia uwezo wao kamili.
Usonji ni ugonjwa unaojulikana mara nyingi katika umri wa miaka miwili hadi mitatu, ambapo dalili za awali huanza kujitokeza.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), takriban mtoto mmoja kati ya 100 duniani kote anapatwa na ugonjwa huu.
Ili kumtambua mtoto mwenye usonji, kuna dalili maalum zinazoweza kuonekana, ambapo miongoni mwa tabia kuu ni pamoja na ugumu katika kuelewa na kutafsiri hisia za watu wengine, hali inayoweza kuathiri ufanisi wao katika mwingiliano wa kijamii.
Mtoto mwenye usonji anaweza kuwa na changamoto katika kutambua na kuelewa hali ya kukasirika inayojitokeza kwa watu wengine.
Hali hii mara nyingi inaweza kumfanya mtoto huyo kuonekana kama anayeonyesha dharau, mtukutu, au kutokuwa na huruma kwa wengine.
Aidha, watoto wenye usonji mara nyingi hupendelea kucheza peke yao na kuepuka kushirikiana na watoto wenzake.
Hata wanaposhirikiana na wenzao, uwezo wao wa kuhusiana na kucheza kwa pamoja unakuwa wa kiwango cha chini na mara nyingi hawawezi kuruhusu watoto wengine kutumia au kuchezea vitu vyake.
Mabadiliko haya yanaongeza ufanisi katika kuelezea tabia za mtoto mwenye usonji na kuzingatia mtindo wa maelezo wazi na wa kiufasaha.
Hali kama hii, ndiyo mara nyingi huwafanya watu wamchukulie kuwa ni mchoyo.
Hayo yanabainishwa wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Uelewa wa Usonji Duniani kupitia Umoja wa Mataifa (UN) Aprili 2, kila mwaka.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu Daktari bingwa wa Magonjwa ya Ubongo na Mfumo wa Fahamu kwa watoto, Edward Kija anasema pili unaweza kuangalia yupo kwenye hatua gani ya usonji.
“Kutokana na level ya mtoto ambayo yupo ndiyo itaainisha mahitaji yake. Kutokana na level ya mtoto aliyopo anaweza akahitaji tiba ya kumsaidia kufanya mazoezi tiba ya mawasiliano, (Speech Therapy).
“Kuna baadhi ya watoto wanakuwa na tabia isiyisawa hivyo akahitaji tiba ya namna ya mazoezi. Pia, kila mtoto atakuwa anahitaji tiba ya mazoezi kulingana na mahitaji yake,” anabainisha Dk Kija.
Akitaja viashiria vya hatari vinavyopelekea mtoto akazaliwa na usonji, Dk Kija anasema watoto wanaouzaliwa kabla ya wakati (Njiti) wanauwezekano wa kupata;
“Huwezi ukagundua mtoto kama ana usonji akiwa tumboni kwa hiyo watoto wanaozaliwa kwenye familia ambazo kuna mtu anatatizo hilo basi anakuwa kweye hatari zaidi,” anabainisha.
Dk Kija anasema hakuna kitu ambacho mama mjamzito akakifanya kikapelekea mtoto wake akapata kuzaliwa na usonji.
Akitaja athari anasema usonji unaathiri uwezo wa kuwasiliana, kujifunza na wakati mwingine unaweza ukageuza mtu akalala mchana badala ya usiku ukaathiri saa za kulala yaani mtu akalala wakati usio sahihi.
“Akiwa shuleni anashindwa kuuliza maswali kwakuwa anashindwa kuwasiliana na walimu ingawa haiathiri uwezo wa akili. Pia, hisia za mwili anaweza akawa anakula chakula cha aina moja tu,” amesema Dk Kija.
Anasema kutokana na athari hizo zinaweza kumfanya akawa tegemezi maisha yake yote.
Hata hivyo, ingawa dalili za usonji zinaweza kuonekana mapema utotoni, mara nyingi utambuzi hufanyika baadaye. WHO inasema ugunduzi wa mapema na kuwahi matibabu kunaweza kuboresha mawasiliano na uelewa wa kijamii dhidi ya ugonjwa huo, na hivyo kuimarisha ustawi wa watu wenye usonji pamoja na walezi wao.
Inaelezwa kwamba watu wenye usonji wanaweza kupata ugumu wa kuhama kutoka shughuli moja hadi nyingine, kuzingatia maelezo madogo madogo, na kuwa na hisia za kipekee kwa masuala mbalimbali.
Zaidi ya hayo, mara nyingi wanakumbana na hali zingine kama vile, msongo wa mawazo, wasiwasi na matatizo ya usingizi.
WHO inasema utafiti wa kisayansi unaonyesha Usonji husababishwa na mchanganyiko wa sababu za kijenetiki na kimazingira.
Ni muhimu kupinga dhana potofu kuwa chanjo husababisha usonji kwani tafiti zimepinga kabisa uhusiano huo. Chanjo, zikiwemo zile zenye thiomersal au alumini, haziongezi hatari yakupata Usonji.
Katika kuadhimisha siku hii inahitajika ujumuishi na hatua za jamii na Serikali ili kukuza ufikiaji wa watu wenye usonji, kukubalika na msaada kwao pamoja na walezi wao.
Juhudi zinapaswa kuelekezwa katika elimu, fursa za ajira na uhamasishaji wa umma ili kukuza mazingira yenye uelewa na yanayojali.
Hata hivyo WHO inasema unaweza kusaidia watu wenye usonji kupita ujumuishaji, kuchagiza matibabu ya mapema, na kuhimiza uelewa katika jamii yako.