Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amefanikisha kutatua mgogoro wa usajili wa kanisa moja la Kipentekoste uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusababisha mvutano mkali miongoni mwa waumini wake.
Mgogoro huo ulihusisha kanisa lililosajiliwa kwa majina mawili tofauti, “Free Pentecostal Church” na “Ebenezer Wave of God Worldwide,” hali iliyosababisha sintofahamu kuhusu uhalali wa umiliki wake.
Kutokana na hali hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa, alilifunga kanisa hilo Machi 2024 ili kupisha uchunguzi.
Hatua hiyo ilisababisha huzuni kwa waumini wa “Ebenezer Wave of God Worldwide,” ambao walidai kuwa wao ndio waasisi wa kanisa hilo, wakikumbushia mchango wao wa kujenga jengo hilo tangu miaka ya 1990, kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2023.

Hata hivyo, leo Jumapili, Machi 30, 2025, Mkuu wa Wilaya Mkude ametangaza kufunguliwa kwa kanisa hilo, akiruhusu waumini wake kurejea kusali, hali iliyoibua furaha kubwa na shukrani kutoka kwa waumini hao.
Akizungumza ndani ya ibada ya kwanza baada ya kufunguliwa kwa kanisa hilo, Mkude amewaomba radhi waumini kwa kuchelewa kutatuliwa kwa mgogoro huo, hali iliyowalazimu kusali nje kwa muda mrefu.
“Nilipopokea jukumu hili mwezi wa pili, nilikumbana na mgogoro huu moja kwa moja. Nilimuomba Mungu hekima ya kushughulikia suala hili kwa haraka, na baada ya kupitia maelezo yote, ukweli umebainika kuwa nyie ndio wamiliki halali wa kanisa hili. Kwa hiyo, leo nimefika hapa kulifungua rasmi,” amesema Mkude.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wake, hataruhusu tena migogoro ya kidini kuchukua muda mrefu bila suluhu na kusisitiza kuwa mizozo inapaswa kutatuliwa kwa amani na haraka.
Kwa upande wake, Askofu Yona Sumary wa kanisa la “Ebenezer Wave of God Worldwide” ameishukuru Serikali kwa kuingilia kati na kufanikisha suluhisho la mgogoro huo.
“Tulifikia mahali tulihisi kama si sehemu ya nchi hii kutokana na hali tuliyopitia, lakini sasa tumeona haki imetendeka. Mkuu wetu wa wilaya ametuletea faraja na amani kwa kuruhusu tuendelee kuabudu katika jengo letu wenyewe,” amesema Askofu Sumary.
Waumini wa kanisa hilo waliufananisha mchakato huo na safari ya uchungu ya mjamzito, wakisema hatimaye wamepata faraja baada ya kipindi kirefu cha mateso.
Diwani wa Baraa, Jacob Junior, amesema kuwa mgogoro huo umewasumbua kwa muda mrefu, lakini wanashukuru kuona hatimaye umetatuliwa kwa amani.
Akitumia fursa hiyo, alimwomba mkuu wa wilaya kuwa mlezi wa kanisa hilo na kusaidia harakati za kukamilisha ujenzi wake, ikiwemo kurekebisha maeneo yaliyoharibika.
Mkuu wa Wilaya, Joseph Mkude, alikubali kuwa mlezi wa kanisa hilo na akaongoza harambee fupi iliyowezesha kupatikana kwa Sh4.247 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi.
Historia ya mgogoro
Mgogoro huo ulianza mwaka 2023 kati ya mwanzilishi wa kanisa hilo, Askofu Yona Sumary, na Mchungaji Godson Mollel, aliyesajili kanisa hilo kwa jina tofauti la “Free Pentecostal Church.”
Kila mmoja alidai kuwa ndiye mmiliki halali wa kanisa, akionesha nyaraka zake na kuwashawishi waumini kumuunga mkono.
Mmoja wa waumini, Saruni Marco, ameiambia Mwananchi kuwa mgogoro huo ulifikia kiwango cha kila kiongozi kuhubiri kwa upande wake ndani ya ibada moja, hali iliyowachanganya waumini.
“Ilifika mahali mmoja anakuja anakaa mbele na kuhubiri, wakati huohuo mwingine yuko nyuma naye anahubiri. Waumini wakawa wanagawanyika; wengine wanamsikiliza huyu, wengine wanamsikiliza yule,” amesema Marco.
Alipotafutwa kutoa maoni yake, Mchungaji Mollel alijibu kwa kifupi kuwa hana cha kusema kwa sasa.