Hivi ndivyo Mwigizaji Fredy alivyopambania uhai wake bila mafanikio

Dar es Salaam. Baba wa Mwigizaji Fredy aeleza mwanaye alivyopambania uhai bila mafanikio

Baba mzazi wa marehemu mwigizaji Fredy Kiluswa, Nahum Kiluswa ameiambia Mwananchi kuwa kwa mara ya kwanza kijana wake alianza kupatwa na maradhi akiwa safarini mwezi mmoja uliopita.

                       

“Mara ya kwanza nilipigiwa simu akiwa anaenda  Ngorongoro alipofika Karatu alienda saluni kisha hapo akawa anajisikia vibaya anatapika wale wenyeji wake  wakamkimbiza hospitali wakagundua kuwa ana kitu kwenye mapafu au  moyo lakini hawana vipimo zaidi wakashauri twende Muhimbili.

 “Alivyoletwa vipimo vya kwanza ikagundulika kuna  na tatizo kwenye mirija ya damu moyoni na tiba yake kuna dawa maalumu anaweza kunywa alafu polepole ikajifungua. Akapewa dawa akanywa kwa wiki tatu ndiyo Ijumaa Novemba 16, 2024 alipozidiwa nikapigiwa simu akapelekwa Muhimbili akawekwa ‘emergency’ pale akawa anapumua  kwa tabu sana presha ipo juu haijashuka kwa muda mrefu’,”

                      

Anasema baada ya kufika saa tisa mchana presha ilishuka ndipo Fredy akahamishiwa Hospitali ya Mloganzila.

“Akalala pale kesho yake nikaenda saa 11 :30 jioni  nilichokikuta huwezi kuamini nilimkuta mwanangu anapambana kuokoa roho yake anapumua kwa tabu kifua kinapanda juu kama anatafuta hewa hapati, nikawa naongea na muuguzi nikageuka nikakuta amekata roho nikamwambia ulinisubiri nije ndio uondoke mbele yangu,”amesema baba wa marehemu.

Aidha amesema mwanaye hajawahi kuwa na historia ya kuumwa magojwa hayo hata alivyokuwa mtoto.

“Nakumbuka mambo mengi alikuwa anapenda usanii tangu mtoto alipomaliza kidato cha nne nikamuuliza anataka kuwa nani akaniambia usanii nikampeleka Bagamoyo,  anapenda wazazi wake anaweza kukupigia simu akakusalimia tu na hata mimi nilikuwa nikimtumia  sms asubuhi ananijibu jibu moja tu Mungu ni mwema.

“Sikujua  ndani ya maneno hayo Mungu ni mwema yalikuwa na maana kubwa sana na sikujua kama siku ya Jumamosi atasubiri mpaka niingie nikiwa mtu wa mwisho ndio aondoke ni pigo kubwa sana,”amesema.

Baba huyo pia  ametoa pole kwa mashabiki waliokuwa wakimfuatilia mwanaye katika kazi zake za sanaa.

                       

“Najua watamkumbuka kama mimi nitavyomkumbuka lakini kazi ya Mungu haina makosa kila mmoja aliyekuja hapa duniani kuna siku yake ataondoka kwa siku Mungu aliyopanga bila kuongeza saa wala kupunguza dakika,” amesema.

Fredy aliyezaliwa mwaka  1992, ameacha mke mmoja aliyekuwa akiishi nae na watoto wawili. Mwili wake utaagwa Jumanne, Novemba 19,2024 katika Viwanja vya Leaders Club na kisha kupumzishwa kwenye makaburi ya Kinondoni.