Hivi ndivyo diaspora wameguswa kwenye Sera ya Mambo ya Nje

Hivi ndivyo diaspora wameguswa kwenye Sera ya Mambo ya Nje

Dar es Salaam. Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) wamepewa nafasi ya kipekee katika toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2024, licha ya suala la utoaji wa hadhi hiyo maalumu kuahirishwa mara kadhaa.

Jana, Mei 19, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua sera hiyo huku akiwakaribisha diaspora kuja kuwekeza kwenye sekta za kiuchumi na kijamii, akisema Serikali inawatambua kama wabia muhimu wa maendeleo.

Sera hiyo ni maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 iliyozinduliwa Ngorongoro, Aprili 30, 2001. Maboresho hayo yamefanyika ikiwa imepita miaka 24, kipindi ambacho ulimwengu umeshuhudia mabadiliko mengi yaliyoathiri uhusiano wa mataifa.

Kanuni kuu za Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kulinda mamlaka kamili, mipaka ya eneo na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulinda uhuru na haki, haki za binadamu, usawa, uwiano na demokrasia, kuhimiza ujirani mwema na kuhimiza Umoja wa Afrika.

Pia, kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo, kuwezesha utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote na ushirikiano na ulimwengu wa Kusini.

Kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika juhudi zake za kuleta maendeleo ya kiuchumi kimataifa, amani na usalama; na kuhifadhi maadili ya kijamii na tamaduni za watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Malengo ya kimkakati ya sera hiyo yatajikita katika diplomasia ya kiuchumi, amani, usalama na utulivu wa kisiasa, mikataba, itifaki na makubaliano ya kimataifa, uhusiano wa nchi mbili, ushirikiano wa kikanda na uhusiano wa kimataifa.

Vilevile, kukuza lugha ya Kiswahili, uhamasishaji wa rasilimali, uchumi wa buluu, ushiriki wa diaspora, haki za binadamu na masuala mtambuka (hususan mabadiliko ya tabianchi, jinsia na vijana).

Diaspora walivyomulikwa

Kama sehemu ya wadau, Sera ya mambo ya Nje imewajumuisha pia diaspora ikilenga kuwezesha utekelezaji wa Hadhi Maalumu—mpango wa kutoa haki na upendeleo kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.

Lengo hili la kimkakati litatekelezwa kupitia marekebisho ya sheria mbili muhimu, ambazo ni Sheria ya Ardhi Sura ya 113 ili kuwezesha umiliki wa ardhi na Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 ili kurahisisha kuingia na kutoka kwa uhuru katika Jamhuri ya Muungano;

Mchakato wa kufanya marekebisho mengine mbalimbali unaendelea kupitia taratibu zilizowekwa ndani ya Bunge.

Hata hivyo, Januari 29, 2025, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliondoa marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji, Sura 54, katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2024, uliolenga kutoa utaratibu wa hadhi maalumu (Diaspora Tanzanite Card) kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.

Pia, Dk Tulia aliondoa marekebisho ya Sheria ya Ardhi, Sura 113, katika muswada huo, ambayo ilikuwa ikielezea utaratibu wa upatikanaji wa ardhi kwa watakaopewa hadhi maalumu.

Marekebisho hayo yaliondolewa bungeni kwa mara ya pili, baada ya kuondolewa na Serikali Septemba 4, 2024, kwa kile kilichoelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari kuwa ni kutoa nafasi ya kuendelea kufanyia kazi zaidi hoja hiyo.

Hata hivyo, Novemba 8, 2024, Serikali ilirudisha marekebisho hayo ndani ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4, Mwaka 2024, ambapo ulipelekwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.

Mambo mapya kwenye sera

Toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje limezingatia mambo kadhaa yenye masilahi kwa diaspora, miongoni mwayo ni kuhakikisha mahitaji yao yanatekelezwa, ikiwa ni pamoja na kutoa hati maalumu kwa diaspora wasio raia wa Tanzania.

Pia, sera inalenga kuratibu na kuweka utaratibu rasmi wa kushirikisha diaspora katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya taifa.

Kadhalika, sera inalenga kuhakikisha Watanzania wanapata fursa za ajira katika masoko ya kimataifa pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye ubora za idadi ya diaspora.

Mchango wa diaspora

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, fedha zinazotumwa na diaspora zimeendelea kuongezeka kwa kasi. Kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, wastani wa mapato ya mwaka kutoka kwa diaspora ulikuwa zaidi ya Dola za Marekani 762.5 milioni, (Sh1.982 trilioni), fedha ambazo husaidia familia na kugharamia elimu, huduma za afya na ujasiriamali.

Ili kuongeza mchango wa fedha hizo katika maendeleo, Serikali imeshirikiana na benki kupunguza gharama za uhamishaji na kutoa bidhaa maalumu za kifedha—kama vile akaunti za akiba kwa diaspora, mifuko ya uwekezaji, na akaunti za fedha za kigeni.

Aidha, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka kwa diaspora umeongezeka. Kupitia mifumo kama Mfuko wa Uwekezaji wa UTT na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Watanzania wanaoishi nje wamewekeza zaidi ya Sh10 bilioni katika miradi ya maendeleo ya taifa. Taarifa ya wizara inaeleza kuwa wengi wao wamepata nyumba katika miji kama Dar es Salaam, Dodoma na Arusha—jambo ambalo linachangia kupunguza uhaba wa makazi na wakati huohuo kuongeza ajira.

Bado wataka uraia

Akizungumzia kuhusu sera mpya ya Mambo ya Nje, Mkurugenzi wa Tanzania Diaspora Foundation, Kelvin Nyamori amesema Watanzania waishio nje ya nchi hawatanufaika na sera hiyo kama hawatatambuliwa kuwa ni raia wa Tanzania.

Amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiimba kuhusu Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine kutambuliwa kama Watanzania, hata hivyo jitihada hizo hazijazaa matunda, badala yake wameanzisha kitu kipya (hadhi maalumu).

“Diaspora wanakujaje kuwekeza kama nchi haiwatambui? Hicho ndiyo kitu tunachokipigia kelele siku zote. Wizara ya Mambo ya Nje hawapendi hata kujifunza kwa nchi zilizofanya vizuri, kwa hiyo Tanzania tunakuwa kama tuko kwenye kisiwa.

“Hata hizo sera za Mambo ya Nje tunakuwa tuko kivyetu vyetu, kwa sababu ili uweze kuendelea, huwezi kuacha wananchi wako, wenye asili ya nchi yako, sijui uoga wetu nini,” amehoji mkurugenzi huyo wakati akizungumza na Mwananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *