Hivi hapa vichocheo vya magonjwa ya figo, gharama tatizo

Dar es Salaam. Licha ya uzito uliozidi, matumizi ya sigara na pombe kali kuwa vichocheo vya magonjwa sugu ya figo, wataalamu wameonya unywaji holela wa dawa hasa zile zisizothibitishwa na mamlaka zinachangia kwa kasi tatizo hilo.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya figo leo Machi 13, 2025, wataalamu wa afya wameeleza hatari zinazoweza kusababisha maradhi ya figo ikiwemo matumizi ya tiba asili, na dawa zinazouzwa kiholela mitandaoni.

Hayo yanaelezwa wakati takwimu za Wizara ya Afya hadi mwaka jana zikionyesha, idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji damu ‘dialysis’ iliongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi 3,231, Desemba mwaka 2023.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Wizara ya Afya, Roida Andusamile amesema wanaofanyiwa kwa sasa mwaka 2025 idadi yao imefikia wagonjwa 3,327.

Mkuu wa kitengo cha figo Hospitali ya Benjamin Mkapa BMH, Dk Kessy Shija amesema matumizi ya dawa holela ambazo hazijathibitishwa na mamlaka, yanaweza kuwa na madhara hivyo wananchi wanapaswa kutumia dawa ambazo zimethibitishwa.

“Tunashauri mtu kutumia dawa ambazo zimethibitishwa, kuna mamlaka za kuthibitisha. Unapotumia dawa kiholela unaziweka figo hatarini,” amesema Dk Shija.

Dk Kessy anasema unywaji holela wa dawa za kupunguza maumivu, zina madhara kwenye figo zikitumika kwa muda mrefu bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

“Ukimeza dawa holela upo uwezekano wa figo zako taratibu kushindwa kufanya kazi, dawa za kisasa na kienyeji, pia dawa za kulevya zina madhara,” anasema.

Aidha, matumizi ya tiba asili yanaweka hatarini figo kutokana na dawa nyingi za asili kutopitia mchakato wa kupimwa viwandani na kutoa majibu ni kiwango gani unapaswa kukitumia kujitibu, ambacho mwili unaweza kumudu au kustahimili ile nguvu ya dawa.

Daktari mbobezi wa magonjwa ya ndani na figo kutoka hospitali ya Saifee, Mercy Mwamunyi amesema tiba asili zinaleta changamoto ya figo kutokana na dawa zilizo nyingi kutopitia mchakato wa upimaji kwenye viwanda, kwani kila dawa inatakiwa iwe na kiwango ambacho mwili utaweza kustahimili.

‘’Kwahiyo kuna dawa zingine pia zinatolewa kwenye mwili kupitia figo, kama hazijapimwa hatujua kiwango gani cha dawa hii inaleta athari kwenye figo.

“Ni vema ukatumia dawa kutoka kwa mtaalamu ambaye amepitishwa na Serikali na Mkemia Mkuu wa Serikali na mamlaka husika, lakini dawa ambazo hazijapimwa ni vema kuziepuka maana hujui kiwango cha ile dawa ina sumu kiasi gani, inaingia kwenye mwili na itakuletea madhara gani hapo baadaye,” amesema Dk Mercy.

Aidha Dk Kessy amesema mtindo wa maisha kwa namna ya kutojali afya unaweza kusababisha hatari kwenye figo.

Amesema visababishi vikuu vya shida kwenye figo ni maradhi ya kisukari na shinikizo la juu la damu (Pressure), na visababishi hivyo vina uhusiano mkubwa na mtindo wa maisha.

Dk Shija amesema hivyo mtu ambaye hafanyi mazoezi, mtu mwenye uzito ulopindukia ana hatari ya kupata shinikizo la juu la damu.

“Mtu mwenye uzito uliopindukia pia inaweza kumletea shida kwenye figo na kupata kisukari. Wengine wanaweza kupata shinikizo la juu la damu  kutokana na madhara ya sigara,” amesema.

Amesema matumizi ya vyakula kama chumvi iliyozidi kiwango ina uhusiano na shinikizo la juu la damu.

“Watu siku hizi wanakula chipsi mishikaki wanaongeza chumvi iliyozidi kiwango, unywaji wa vinywaji vikali kama pombe kali pia nayo inaweza ama kuleta athari moja kwa moja kwenye figo, au kuwa kuwa vihatarishi vya madhara mengine,” amesema Dk Shija.

Mratibu wa tiba na magonjwa yasiyoambukiza Manispaa ya Kinondoni, Dk Omary Mwangaza amesema katika kila watu saba, mmoja ana tatizo la figo.

Akielezea dalili za ugonjwa wa figo, Dk Mercy amesema kwa sababu  magonjwa ya figo hayajulikani dalili zake mapema, vipimo ndivyo hubainisha mapema zaidi.

“Kuna dalili tunazoweza kutambua mapema, mwingine akikojoa mkojo unamuwasha, unamchoma, mwingine mkojo una mapovu au kiwango cha maji alichokunywa na mkojo anaoutoa havilingani, magonjwa ya figo yanakuja kulingana na vile viashiria hatari alivyonavyo mfano sukari na shinikizo la juu la damu.

“Mwingine hajui hali yake ya kisukari, ukimpima unakuta ipo juu unagundua na figo kumbe zilishapata changamoto siku nyingi vivyo hivyo na shinikizo la juu la damu, hivyo ni vema ukatambua figo zako mapema kama ziko salama au vinginevyo, hii itasaidia kuepuka athari mbaya hapo baadaye,” amesema.

Amesema ni muhimu kufanya uchunguzi mara kwa mara angalau mara moja au mbili kwa mwaka, hasa wale waliokutwa na changamoto awali. Dk Mercy amesema vipimo vya awali mara nyingi havina gharama kubwa.

Siku ya Figo Duniani, inayoadhimishwa Machi 13, 2025, hutumika kama ukumbusho wa kimataifa wa umuhimu wa afya ya figo.

Kauli mbiu ya mwaka huu, ‘Je, figo zako ni salama? Tambua mapema, linda afya ya figo’ inasisitiza uwezo wa kutambua matatizo ya figo mapema.

Wakati wataalamu wakitaja mbinu za kuepuka ugonjwa huo, taarifa za ndugu wanaouguza wagonjwa wa figo si nzuri, kwani wengi wamekuwa wakiingia katika umasikini mkubwa hasa wale wanaolipia huduma kutoka mfukoni ‘out of pocket’.

Miongoni mwa changamoto zinazowasibu wagonjwa wenye magonjwa sugu ya figo ni usafishaji damu, huduma ambayo mgonjwa hupatiwa mara tatu kwa wiki, ili aendelee kuishi wakati akisubiri upandikizaji wa figo.

Gharama za usafishaji figo zimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka mpaka kufikia kiasi cha Sh150,000 kwa mzunguko mmoja, hivyo mgonjwa kuhitaji Sh450,000 kwa mzunguko.

“Tunauguza mgonjwa wa figo, anasafishwa damu kupitia mashine mara tatu kwa wiki, tunalipia si chini ya Sh450,000 kwa wiki tangu alipoanza kupata huduma hiyo, awali tulitumia zaidi ya Sh1 milioni kwa wiki. Tumeuza mashamba, viwanja na baadaye tukaanza kuchangishana kama familia.

“Gharama ni kubwa,” amesema Merry Swai ndugu wa mgonjwa.

Ili kukabiliana na gharama kubwa ya huduma ya usafishaji wa damu kwa wenye ugonjwa sugu wa figo, mashine mpya aina ya SWS 6000 ziliingizwa nchini ambazo zilishusha gharama ya tiba hiyo kutoka Sh250,000 mpaka Sh150,000.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025 mashine 113 zimeshapokelewa Bohari ya Dawa (MSD) na tayari mashine 72 zimesambazwa kwa hospitali 14 nchini ikiwa ni nyongeza ya mashine 137 zilizosambazwa awali. Gharama ya mashine moja ni Sh31,761,000 milioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *