Historia yaibeba Yanga nyumbani dhidi ya Waethiopia

Kumbukumbu ya mechi za nyuma zinaipa Yanga hali nzuri kisaikolojia kupata matokeo mazuri dhidi ya CBE ya Ethiopia leo kwenye mechi ya nyumbani ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa leo kuanzia saa 2:30 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika mchezo huo wa leo, Yanga inahitaji matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote mbele ya Waethiopia hao ili iweze kutinga hatua ya makundi ya Lig ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ugenini huko Ethiopia, Jumamosi iliyopita.

Yanga imekuwa na historia ya kufanya vizuri katika mechi za hapa nyumbani za mashindano ya klabu Afrika dhidi ya timu za Ethiopia kwani katika mara nne ambazo imewahi kucheza, haijawahi kupoteza mechi yoyote huku ikishinda tatu na kutoka sare moja.

Mwaka 1968, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya St. George na mwaka 1998 ikapata ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Coffee ya huko.

Sare ya Yanga nyumbani dhidi ya timu kutoka Ethiopia ilikuwa ni 2011 pale ilipolazimishwa sare ya mabao 4-4 dhidi ya Dedebit na 2018 ikaitoa Welayta Dicha ya huko.

Yanga inaingia katika mechi hiyo ikijivunia viwango bora na endelevu vya wachezaji wake wa kila idara ambavyo vimekuwa chachu ya timu hiyo kufanya vizuri katika mechi za mashindano tofauti ambayo imekuwa ikishiriki kwa miaka ya hivi karibuni.

Safu ya ulinzi imekuwa bora katika kuhakikisha wapinzani hawalioni lango lao kirahisi lakini kuichezesha timu kuanzia nyuma huku ile ya kiungo ikiwa ni kama uti wa mgongo wa kujenga mashambulizi ya Yanga na kuipa muelekeo wa kiuchezaji wakati safu ya ushambuliaji imekuwa vizuri katika kufumania nyavu.

Hilo linaweza kuthibitishwa na matokeo ambayo Yanga imeyapata msimu huu katika mechi za mashindano tofauti ambayo imecheza ambapo imeonyesha ubora mkubwa katika kujilinda, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Timu hiyo imecheza mechi sita msimu za mashindano tofauti, ikishinda zote huku ikifunga mabao 18 sawa na wastani wa mabao matatu kwa mchezo na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu ikiwa ni wastani wa bao 0.2 kwa mechi.

Ubora huo wa Yanga unaenda sambamba na muendelezo wa matokeo ya kuvutia ambayo imekuwa ikiyapata pindi inapocheza nyumbani katika mechi za kimataifa kama hii ya leo.

Matokeo ya mechi 10 zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Yanga imecheza nyumbani yanaweza kuwa shahidi wa hilo ambapo imepata ushindi katika mechi sita, kutoka sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.

Mambo ni tofauti kwa wageni wao CBE ambao wamekuwa hawana historia nzuri na mechi za ugenini na kudhihirisha hilo, katika mechi nne za mashindano ya klabu Afrika walizocheza ugenini kwa miaka tofauti, wamepata ushindi mara moja tu huku wakipoteza michezo mitatu.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo wa leo.

“Hali ya wachezaji wangu ni nzuri, tumejiandaa vizuri sana na tumepata muda wa kujiandaa. Nina wachezaji wakubwa sana ambao wanaweza kufanya jambo bora kuliko wapinzani wetu, najua wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa kufuzu hatua ya makundi,” alisema Gamondi.