Historia ya safari ya muziki ya King Kikii

Leo asubuhi Ijumaa Novemba 15, 2024 tasnia ya muziki wa dansi Tanzania na Afrika kwa ujumla imeamka na simanzi ya kumpoteza mwanamuziki mkongwe, Boniface Kikumbi maarufu ‘King Kikii’.

King Kikii amefariki dunia usiku wa kuamkia leo. Miaka 10 iliyopita—Jumamosi Oktoba 11, 2014 jabali hili la muziki wa dansi lilipata wasaa wa kusimulia safari yake ya muziki katika mahojiano maalumu na Mwananchi, endelea nayo…..

Alishawishika kuingia kwenye muziki akiwa na miaka sita, baada ya kumwona mwanamama Miriamu Makeba.

“Inawezekana kung’aa kwangu katika muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa Januari Mosi, saa 11 alfajiri.” Hayo ni maneno ya mwanamuziki Boniface Kikumbi Mwanza Mpango maarufu King Kikii.

Katika makala haya mwanamuziki huyo atatufahamisha kwa undani historia ya maisha yake, ikiwamo ya muziki, mafanikio na njia alizopitia hadi kufikia hapo alipo.

Kikii alianza kueleza kuwa alizaliwa mwaka 1947 katika Jiji la Lubumbashi lililopo kwenye Mkoa wa Katanga, eneo maarufu huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alisema wakati anakua alikuwa na kaka yake Koroumba Joseph aliyekuwa akipenda muziki kiasi kwamba anapokuwa anafanya kazi zake za kawaida lazima, aimbe wimbo fulani au anapoingia nyumbani kutoka matembezini ilikuwa rahisi kufahamu kama ni yeye kwa kuwa alikuwa akiimba.

Kama bahati nzuri alikuwa akimpenda sana, hivyo muda mwingi alikuwa anaongozana naye, kwenye dansi hasa mwishoni mwa wiki.

Miriamu Makeba, anaamsha roho ya kupenda muziki

Alisema katika kipindi hicho akiwa na umri wa miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952 kundi la muziki kutoka nchini Afrika Kusini ambapo mwanamuziki mahiri Miriamu Makeba alikuwa akifanya kazi nao likafanya ziara ya muziki nchini humo.

Alieleza kuwa ikatokea bahati kama kawaida kaka yake akamchukua na kwenda naye, anasema licha ya miaka mingi kupita hajasahau kiongozi wa kundi hilo alikuwa anaitwa Dambuza Mulele, akiwa na wanamuziki kama Sekena Kolaye, Tigizi Kwankwa, Dolira Jebe na mwenyewe nguli Miriamu Makeba.

Alisema majina hayo hakuwahi kuyaandika wala kuyasoma mahali popote zaidi ya siku hiyo yalipotambulishwa hadi leo anayakumbuka kwa ufasaha kabisa.

“Nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki na nimeona shoo nyingi za kimataifa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile nilichokiona siku hiyo, waliimba kwa ustadi mkubwa, walicheza kama hawana mifupa kwenye miguu na mwili kwa ujumla, Makeba alikuwa ni kinara wa kuimba.

“Kiongozi wao Dambuza Mulele, alikuwa na sauti nzito hivyo alikuwa anachomekea maneno walipokuwa wakiimba kama anavyofanya Koffi Olomide katika baadhi ya nyimbo zake, nilikuwa nasogea mbele kila baada ya muda na sikuwa nafikiri kama nipo katika Mji wa Likasi tulipokuwa tunaishi wakati huo nilijiona kama nipo katika dunia ya wanamuziki watupu,” alisema King Kikii.

Alisema wakati Makeba anaimba alikuwa anaona kama jina hilo hakustahili kuitwa akawa anawaza angepewa nafasi ya kumtafutia jina linaloendana na jinsi anavyoporomosha muziki, lakini kwa bahati nzuri akiwaza hayo akasikia kiongozi wa bendi hiyo akisema anapenda kumwita mwanamama huyo ‘Chocolate Girl’.

“Kwa kuwa nilikuwa na hayo mawazo, na nilikuwa mdogo aliposema hivyo niliruka kwa furaha kiasi cha kusemwa kidogo na kaka yangu, najaribu kukueleza nilivyokuwa najisikia siku hiyo lakini kunielewa ni ngumu, kwa kweli nilikuwa naelea katika dunia ya wapenda muziki,” alisema Kikii.

Aliendelea kueleza kuwa hapo mwanzo kabla ya siku hiyo alikuwa anamshangaa kaka yake kupoteza muda kwenda kwenye majumba ya starehe na kuchelewa kulala, lakini siku hiyo alifahamu kwa nini huwa anakesha huko.

Alisema huku akicheka kwa nguvu kuanzia siku hiyo ndiyo alianza rasmi kuupenda muziki.

Alieleza kuwa alipofika darasa la nne baba yake ambaye alikuwa ni mfanyakazi katika kampuni ya madini inayotambulika kwa jina Gecamiou Athenee Royale kwa sasa, wakati huo ilikuwa ikijulikana Union Miniere Du Hut Katanga alipata uhamisho na kuhamia katika mji wa tatu kutoka Likwasi . Akiwa anapenda kuimba imba mwalimu wake akaliona hilo na kumjumuisha katika vikundi vya ngoma na muziki shuleni hapo.

Alisema wakati huo kaka yake aliyekuwa anakwenda naye dansini mwaka 1953 alipata safari ya kwenda nchini Afrika Kusini, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuja Miriamu Makeba na kundi lake, mwaka 1958 akarudi na kuanzisha kikundi cha muziki alichokiita Bantu Negro ambacho kilikuwa kinapiga muziki wa Afrika Kusini.

Alisimulia kuwa kuwapo kwa bendi ya kaka yake kulizidisha hamu yake ya muziki, anakumbuka aliwazoea sana wanamuziki waliokuwa wakifanya kazi na kaka yake huyo ambao ni Zapta Mfana, Kumaro Kadima, Andre Kaka na Joseph Kolomba.

“Naweza kusema hawa walinipa ujuzi mkubwa kwani nilijifunza kupiga vyombo pamoja nao, na hapo ndipo nilipopenda kucheza, sikuwa mnene kama nilivyo sasa ungeniona ungefurahi,” alisema Kikii kwa kujiamini na akicheka kuonyesha anamaanisha anachokisema.

Alisema akawa anachukua utaalamu wa kucheza kutoka katika bendi hiyo na kuupeleka shuleni ambapo alitafuta wanafunzi wenzake watatu na kuanzisha kikundi cha muziki wa dansi wakiwa darasa la tano.

Alisimulia, walimu waliupenda muziki waliokuwa wanaimba na kucheza, hivyo kila sherehe za shule ni wao na sifa za umahiri wao zikavuma kwa kuwa walikuwa vijana wadogo wanafanya mambo makubwa.

“Haikuishia hapo, kwani hata katika sherehe za watu wa karibu na shule, wanafunzi waliokuwa na sherehe majumbani mwao, walikuwa wanatualika na tunakwenda kuimba na kucheza bure,” alisema King Kikii.

Alisema kuwa mbali na kupenda muziki alikuwa ni mahiri katika masomo na hakuwahi kuwa mtu wa tatu kila anapofanya mtihani akifeli sana wa pili.