Tanga. Unapotaja maeneo ya kihistoria nchini, huwezi kuliweka kando Jiji la Tanga, kama eneo maarufu na muhimu katika Mkoa wa Tanga.
Nje ya historia ya mkoa, maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Tanga yana simulizi za kuvutia kwa anayezisoma au kusikiliza.
Mwananchi Digital tunakunyofolea baadhi ya maeneo na kukupa kwa ufupi simulizi zake, kama ilivyodokezwa na mwenyeji mmoja aliyezaliwa jijini hapo miaka ya 1960.

Mnara maarufu katika eneo la Mabanda ya Papa jijini Tanga kwenye mzunguko wa barabara ya kwenda Donge,Ngamiani na maeneo mengine.Picha na Rajabu Athumani
Asili ya Ngamiani
Ukifika jijini Tanga basi ni lazima utakanyaga kata ya Ngamiani.
Hapa ndio kuna soko la Tangamano, stendi ndogo ya mabasi na huduma nyingine muhimu za kijamii
Inaelezwa miaka ya zamani eneo hilo kulikuwa mnada wa mifugo hasa ngamia waliokuwa wakipatikana kwa wingi.
Biashara hiyo kwa mujibu mkazi wa jijini hapo, Abubakar Wendo, ilikuwa ikifanywa na wafanyabiashara wa Kiarabu.

Maeneo kuanzia Mabanda ya Papa hadi Ngamiani jijini Tanga kwenye barabara maarufu ya Taifa Road.
Asili ya Kisosora
Wendo anasema awali eneo hilo lilikuwa linaitwa Misufini kutokana na kuwepo miti mingi aina ya Misufi, hivyo wananchi walioanza kujenga hapo walianza kutambulishana kuwa wanajenga Misufini.
“Baadaye alijitokeza mwananchi mmoja na kujenga hapo ambae alikuwa Mnyamwezi aliyeitwa Sosora,na kuanza kutambulisha jina la Kisosora na hatimaye kuzoeleka mpaka sasa,” anasema.
Majani Mapana
Mtaa mwingine ambao jina lake ni maarufu katika Jiji la Tanga, ni Majani Mapana ambao upo kata ya Nguvumali.
Wendo anaeleza kuwa sababu zamani kulikuwa na miti aina ya mitiki, na hakukuwa na watu wengi wakiishi hapo,ila waliokuwapo walizoea kuita miti hiyo kwa jina la majani mapana kutokana na majani ya miti hiyo kwa mapana.
“Kwasababu lilikuwa zao jipya kwao hawakujua kama linaitwa mitiki, hivyo wananchi waliendelea na jina lao kwamba wanakwenda kwenye majani mapana na baadaye ndio kukazaliwa jina la Majani Mapana ukiwa mmoja wa mitaa ya mwanzo kama unaingia jijini Tanga,” anaeleza.

Sanamu lililopo eneo la Kwaminchi, moja ya maeneo maarufu jijini humo, likiwakilisha kilimo cha zao la mkonge mkoani Tanga.Picha na Rajabu Athumani
Ukifika jijini Tanga ukiingia mitaa ya Kwaminchi basi umeshafiki mjini, Wendo anasema enzi hizo eneo hilo lilikuwa linaitwa Mwanzang’ombe.
Kwaminchi anasema limetokana na mzee mmoja wa Kijerumani aliyefahamika kwa jina la Minchi.
“Mzee Minchi alipewa sehemu ya kuishi na mwenyeji wake aliyefahamika kwa jina la Halfan,ila kwa sifa ile ya kusema hapa anakaa mzungu,basi jina la mwenyeji halikuweza kuvuma na badala yake likavuma la mgeni la mgeni wake. Hivyo wenyeji walivumisha jina la Kwaminchi ambalo linatumika mpaka sasa,” anasema.
Mabanda ya Papa
Eneo hili lipo katikati ya jiji na simulizi zinaeleza kuwa lilitokana na uwepo wa soko la samaki hasa aina ya papa ambao ni maarufu kwa wakazi wa jiji hilo.
“Walikuja wafanyabiashara Waarabu kutoka Yemen wakibeba nguo na samaki ambapo walijenga mabanda na kuweka bidhaa zao. Papa ndio ilikuwa bidhaa kubwa kwenye mabanda mengi na watu waliokuwa wanakwenda hapo wakawa wanaita Mabanda ya Papa,” anaeleza.
Anaongeza: “Baadaye biashara hizo zilipokwishwa eneo lilibakia na jina lilele la Mabanda ya Papa ila kwasasa shughuli za biashara zimetanuka kwani hutakuta papa pekee, kuna watu wanafanya biashara zote.”
Chumbageni
Eneo jingine ni Chumbageni ambapo Wendo anasema asili yake zamani, kulijengwa vibanda kwa ajili ya wageni waliokuwa wakifika Ngamiani na Mabanda ya Papa kufanya biashara zao.
“Vibanda hivyo vilikuwa maarufu kama vyumba vya wageni, lakini wafanyabiashara wa Kiarabu walishindwa kutamka, wakawa wanaita chumba geni,” anasema.