Historia ya Clara yawaliza waombolezaji msibani

Moshi. Mamia ya waombolezaji walioshiriki mazishi ya mwanafunzi wa Chuo cha Utalii na Ufundi Marangu, Clara Kimati (21) wamejikuta wakiwa katika majonzi mazito na kububujikwa na machozi wakati historia yake ikisomwa kwenye maziko hayo.

Clara ambaye alikuwa ni mtoto wa kwanza wa familia ya Kimati, aliachiwa wadogo zake wawili  baada ya wazazi wake wote kufariki dunia mwaka 2019 na 2020, ambapo yeye ndiye aliyekuwa tegemeo la familia yake na badala yake historia imebadilika na kuwa ni pigo tena kwa familia hiyo.

Hivyo, ni kama wadogo zake wamekosa tumaini tena kutokana na kifo cha dada yao huyo ambaye walikuwa wakimtegemea kuwa mkombozi wao wa baadaye.

Clara ambaye amezikwa leo Alhamisi, Machi 6, 2025 pembezoni mwa kaburi la baba na mama yake, mtaa wa Msufini, kata ya Makuyuni, Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, alifariki dunia Februari 25, 2025 baada ya kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha utumbo kutoka nje na kulazwa hospitali ya KCMC Desemba 5 mwaka jana hadi alipofariki dunia.

Hata hivyo, vilio na simanzi vimetawala msibani hapo, huku baadhi ya waombolezaji wakishindwa kujizuia na kuzimia.

Akitoa mahubiri katika ibada ya mazishi ya mwanafunzi huyo, Padre David Mwahiri wa Parokia ya Rauya Himo, amelaani vikali mauaji hayo na kusema hakuna mwenye haki ya kutoa uhai wa mtu mwingine na kila mtu ana haki ya kuishi.

“Clara amekufa akitetea utu wake, baada ya kumkataa muhalifu, tunamshukuru Mungu kwa ujasiri wake, ametetea utu wake ndipo akapoteza maisha baada ya kupata  majeraha yaliyopelekea kifo chake,” amesema Padre Mwahiri.

Amesema Clara alitarajiwa kuwa mtu wa kusaidia familia yake baada ya wazazi wake wote kufariki lakini haikuwa hivyo, akawataka waombolezaji waendelee kuwaombea wadogo zake waliobaki.

“Tunaiomba familia mpokee msiba huu kwa matumaini, huyo Mungu aliyewapa Clara atawajalia tena zawadi nyingine, hakika msiba huu unaumiza.”

“Tunaiombea amani familia hii lakini hatutaki haki ya mtu ipotee, wadogo zake Clara tunawaombea msiba wa dada yenu usiwapelekee kuyumba, simameni imara katika imani,” amesema Padre Mwahiri.

Historia ya Clara

Akisoma historia ya marehemu, Theresia Mtui, amesema mtoto wao amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa visu sehemu za tumboni, mgongoni na sehemu mbalimbali za mwili wake hivyo kusababisha kifo chake.

“Tunawashukuru ndugu jamaa na marafiki waliomsaidia Clara tangu alipoondokewa na wazazi wake hadi leo, Mungu awabariki sana,” amesema Theresia huku baadhi ya waombolezaji wakionekana kububujikwa machozi.

Akitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Chuo cha Ufundi na Utalii Marangu, Paul Joseph amesema kifo cha Clara kimewaumiza kwa kuwa alikuwa katika hatua ya mwisho ya kumaliza masomo yake.

“Kifo cha Clara kimetuumiza sana kwa namna kilivyotokea, kama chuo tumeumia kwa sababu siku hiyo alimaliza mitihani yake ya nadharia saa saba mchana na alikuwa  akijiandaa na mtihani wa vitendo,”amasema mkuu huyo wa chuo.

“Sasa jioni yake ndio tulipata hizi taarifa kwamba kushambuliwa, kwa kweli hizi taarifa zilitusikitisha mno, tulienda hospitali kumuona lakini hatukuweza kuongeza naye kutokana na hali yake ilivyokuwa,” amesema Joseph.

Akimzungumzia Clara, Winfrida Lyimo ambaye ni rafiki na mwanafunzi mwenzake, amesema Clara alikuwa na upendo na kila mtu na mwenye hekima.

“Clara nilizoeana naye hata kabla sijaanza chuo, alikuwa ni mtu wa watu na tumefanya mambo mengi sana, sijui ni kwa nini huyu mtu ameamua kumfanyia ukatili wa namna hii, alikuwa mwenye hekima kwa kila mmoja,” amesema Winfrida.

Ameiomba Serikali kuingilia kati mauaji hayo ya kikatili na kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa.

“Tunaomba Serikali iingilie kati jambo hili ili haki ya Clara ipatikane, aliyetenda hili kosa tunaomba ahukumiwe kwa haki, wasifiche haki ya Clara popote pale,”amesema huku akibubujikwa na machozi.

Emmanuel Mosha, mwanafunzi mwenzake na Clara amesema:”Clara alikuwa mwenzetu, mchapakazi, mcheshi na alikuwa hana ugomvi na mtu alikuwa na upendo na kila mtu, tukio hili limetuumiza sana, tunaomba vyombo vya sheria vichukue hatua kwa aliyefanya tukio hili.”