Waislamu huwa wanaita chungu. Kitakuwa chungu cha saba Jumamosi jioni. Dakika chache baada ya kugusagusa futari macho na masikio tutayaelekeza pale Lupaso. Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kugusagusa futari ndiyo lugha sahihi zaidi. Hadi kufikia siku hiyo mashabiki wengi watakuwa hawajiwezi kwa hisia. Wengine watashindwa kula. Wengine wameanza kushindwa leo. Mawazo ni mengi. Nani anapigwa mechi hiyo? Ni swali linalosababisha watu washindwe kula vizuri.
Kuna mambo saba ya kufikirika katika pambano. Jambo la kwanza? Hakuna anayepaswa kukubali kichapo na hasa Simba. Matokeo mabovu zaidi kwao yawe sare sio kufungwa. Ndani ya hili kuna mambo mawili.

Akifungwa hii itakuwa mara ya tano mfululizo. Haikubaliki. ‘derby’ itakejeliwa kuliko kiasi na watani zao. Mara tano! Hapana. Kuna jambo lazima lifanyike. Na mbaya zaidi itaonekana kama vile na wao wameungana moja kwa moja na timu ambazo kwa sasa zinajulikana kama matawi ya Yanga.
Mashabiki wa Simba wataruhusiwa kuuliza uongozi kama ni kweli wamemshindwa kijana Injinia Hersi Said na genge lake la watu wa Yanga. Itakuwa mara nyingi zaidi na itawafanya wajisikie wanyonge zaidi.
Lakini hapo hapo haifikiriki Simba kufungwa kwa sababu ukweli ni kwamba endapo watapoteza pambano hili basi Yanga wataawacha nyuma kwa pointi saba, ingawa Simba atakuwa na mechi moja mkononi ambayo akishinda atapunguza pengo hilo.

Tatizo la mpira wetu ni hakuna timu ambazo unazitegemea sana zikufanyie kazi. Zipo chache zinazoweza kukusaidia, lakini hauwezi kuzijua labda bahati tu itokee. Hili litawakuta na Yanga pia wakifungwa. Kama wakifungwa na Simba wakala kiporo chao vizuri basi Simba atasimama juu ya Yanga kwa pointi mbili. Yanga wana uhakika gani kuna mtu atawafanyia kazi ya kumpunguzia Simba pointi tena kama Fountain Gate na Azam walivyofanya hapa karibuni? Haifikiriki sana.
Hii inafanya mechi hii kuwa kama fainali tu. Nadhani katika miaka ya karibuni hawa wakubwa wamekutana katika pambano la pili wakiwa wamekaribiana zaidi katika msimamo wa ligi. Inatoa picha hii ni kama fainali tu.
Jambo la pili mechi hii. kwa mlio karibu na makipa wa Yanga na Simba, Moussa Camara na Djigui Diarra waambieni makosa ya wazi hayaruhusiwi mechi hii. Kila mmoja ana kesi yake mkononi na huenda siku hiyo ikawa hukumu.
Rafiki yetu Camara mashabiki walisimama naye, licha ya kosa la kizembe lililowapa Yanga ushindi wake wa nne mfululizo pambano lililopita.
Kaka yangu, Crescentius Magori alimuita Camara mara tatu wakati alipourudisha ndani mpira wa Clatous Chama ambao ulikuwa unakwenda nje. Maxi Nzingeli akaurudisha ndani, Kelvin Kijili akajifunga kwa bahati mbaya.
Camara hataruhusiwa tena kufanya kosa hilo. Kuanzia pambano hilo hadi Jumamosi atakuwa hajafanya kosa lolote la kizembe. Iweje arudie tena kosa katika mechi ya Yanga. Yatajengwa mawazo fulani ya kufikirika na ninavyojua mimi baada ya hapo maisha yake yatakuwa magumu Tanzania.

Diarra watu wa Yanga wameguna makosa aliyoyafanya hivi karibuni. Msimu huu mashabiki na viongozi wala hawamuelewi, lakini kwa heshima zaidi wameendelea kumweka katika lango lao. Dhidi ya Simba kosa lake halitaeleweka kamwe.
Ajiandae kucheza moja kati ya mechi yenye presha kwake kuliko wakati mwingine wowote. Akifanya makosa ya kipuuzi katika pambano hilo basi fungate lake na mashabiki wa Yanga huenda likafika mwisho. Hawa watu wa Kariakoo usijiamini watakupenda kwa muda wote wa maisha ya soka.
Jambo la tatu. Kibu Dennis ni mchezaji wa mechi kubwa na kwa hilo tayari amekonga mioyo mashabiki wa Simba katika mechi kubwa. Hata hivyo, kuna wengine ambao wanahitajika kusimama wahesabiwa. Itakuwa mechi ya kwanza kwa Ellie Mpanzu na lazima afanye jambo la kusaka ufalme katika dabi.
Kuna Mcongo alikuwa anaitwa Fiston Mayele alishaacha alama kubwa katika mechi hii na zilimjengea heshima kubwa. Ni wakati wa Mpanzu kufuata nyayo za Mayele au Kibu kuweka heshima katika mechi hii. Nitamtazama kwa jicho la karibu.

Katika hili hili jambo la tatu basi kule Yanga kuna Clement Mzize na Prince Dube. Huyu Dube aliinyanyasa Simba akiwa na Azam, lakini amecheza mechi dhidi ya Simba akiwa katika jezi ya Yanga bado hakuweza kuacha alama.
Ni kama Mzize. Anaonekana kukomaa kwa sasa, lakini ukitaka kuwakosha zaidi mashabiki wa Yanga basi afanikiwe kuwafunga Simba. Unaweza kubadilisha maisha yako zaidi na zaidi. Tayari ameyabadilisha kutoka kuendesha bodaboda na sasa anaendesha Crown ya Kijapan. Anaweza kubadilisha zaidi.
Jambo la nne ni mwamuzi. Natamani awe Ahmed Arajiga. Niliandika hapa jana. Hata hivyo, kuna presha inapenyezwa chini kwa chini kwa Arajiga. Simba wanajiona wana nuksi naye. Huwa hawashindi sana mechi zake, ingawa kwa mtazamo wangu anachezesha kwa haki kama alivyofanya mechi iliyopita dhidi ya Azam.
Hata kama Arajiga hatachezesha pambano hilo basi mwamuzi ambaye atachezesha pambano hilo anapaswa kufuata nyayo za Arajiga. Kwenye penalti unaweka penalti. Hata kama ni penalti tatu kwa timu moja unaweka zote.
Kwenye kadi nyekundu unatoa kadi nyekundu hata kama ni dakika ya saba ya mchezo. Hakuna kubalansi. Huwa inanichekesha pale mashabiki wanaposema, “mwamuzi ametoa kadi nyekundu mapema ameharibu mechi. Mechi kubwa hauwezi kutoa kadi nyekundu mapema vile.”. Hapana. Kadi inatolewa kwa mujibu wa sheria na sio kwa mujibu wa dakika.

Jambo la tano ni kwamba tusiende kwa Mkapa tukiwa na matokeo yetu mfukoni. Wala tusilifuatilie hili pambano tukiwa na matokeo yetu. Zaidi ni kujiandaa kukubali matokeo. Idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na matokeo ya mechi hii kubwa inazidi kuongezeka na inasikitisha.
Presha za mashabiki kuanguka baada ya bao kutinga inakuwa kubwa katika siku za karibuni. Tujifariji kwamba huu ni mchezo tu na mashabiki yanapaswa kusonga mbele baada ya mechi hii.