HISIA ZANGU: Labda simu moja itairudisha Yanga katika dabi

Mpira  wetu bwana. Watu wanaohangaika ni wale wasiokuwa karibu na mambo. Watu wanaoteseka ni wale wa mikoani. Watu wanaoteseka na kuumia ni wale ambao hawajui mambo mengi yanayoendelea nyuma ya pazia. Usiku wa manane simu huwa zinaita.

Nilipomaliza kusoma taarifa ya Yanga kuhusu kutocheza tena pambano la Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba niliishia kutabasamu tu. Huenda wapo sahihi. Huenda ni msimamo wao wa dhati. Yanga wako hivyo miaka na miaka. Wana nongwa zao na huwa zinakaa vyema zaidi kama wakijiona katika haki.

Kutoka sasa hadi tarehe ambayo pambano hilo litapangwa kupigwa Yanga hawatapeleka timu yao uwanjani. Wakisema jambo wanalisimamia. Kinachoweza kubadilisha misimamo yao ni kama kuna simu moja itatembea usiku wa manane.

Utaambiwa tu kuna simu imepigwa kutoka juu. Juu wapi? Huwa hatufahamu. Ila kama simu haitapigwa basi Yanga hawatacheza mechi na Simba hatapewa pointi tatu. Mpira utavurugika zaidi. FIFA hawapendi haya mambo mawili.

FIFA hawapendi mpira kutochezwa. Na hapo hapo hawapendi mpira uingiliwe kutoka kwa watu wengine nje ya wao wenyewe wenye mpira wao. Tatizo letu Afrika hiki ambacho FIFA hawakipendi huwa kinafanya kazi sana kwa sababu hatupendi kufuata kanuni, lakini mpira huwa unaingiliwa na watu wengine wenye nguvu.

Simba na Yanga zitaendelea kugomea mechi bila ya sababu ya msingi na hakuna mwenye ubavu wa kuzipora pointi zao. kama ambavyo wahusika waligoma kuipa Yanga pointi tatu Jumamosi usiku basi ndivyo watagoma kuipa Simba pointi tatu siku hiyo ambayo pambano litapangwa.

Tegemea kwamba kilichotokea kwa Yanga kuikimbia mechi wakiwa wamepasha misuli moto basi kitaendelea kutokea. Siku ile waliyogeuza gari lao wakarudi Kigamboni. Tegemea walichofanya Simba Jumamosi usiku kitaendelea kutokea.

Hakuna mtu mwenye ubavu wa kuziadhibu. Lakini tegemea kuna simu zisizoruhusiwa na FIFA zinaweza kutembea usiku wa manane na kulazimisha pambano hilo kufanyika. Hiki ndicho kitu pekee ambacho watu wa Bodi wa Ligi wanaombea.

Watu wa Bodi ya Ligi wao wenyewe kwa ubavu wao jambo hili hawaliwezi. Lipo juu yao. Yanga waliwahi kugomea pambano la mshindi wa tatu michuano ya Kombe la Kagame inayoendeshwa na Cecafa dhidi ya Simba na wakafungiwa miaka mitatu na Cecefa ya Nicholas Musonye, kisha Leodegar Tenga akiwa Rais wa TFF aliifungia kucheza kimataifa na kuitumikia kwa miaka miwili.

Baadaye wabunge wakaja juu pale Dodoma na Yanga wakafunguliwa. Tegemea katika uhai wako, utashuhudia tena Yanga au Simba inagoma kuingia uwanjani katika pambano la Dabi. Sio hili linalokuja ambalo Bodi inataka kupanga tarehe upya, hapana, hata jingine la msimu ujao.

Mpira wetu kwa kiasi kikubwa umechanganywa na siasa nyingi. Ukiwa karibu na watu wa Bodi au TFF utagundua namna ambavyo wakati mwingine wamekuwa wakielemewa na simu za usiku wa manane kutoka kwa watu wasiojulikana ambao wamekuwa wakipanga wanachotaka kiwe.

Bahati nzuri kwa watu wasiojulikana ni hawawezi kwenda hadharani kwa sababu wanajua nguvu ya Fifa. Wanajua namna gani ambavyo FIFA hawataki mwingiliano wa mambo. Hata hivyo, kwa nchi zetu hizi maskini hilo ni jambo la kawaida tu.

Kitu ambacho hakiwezi kubadilika ni kuona watu kama Azam TV wakichukia na kutoa taarifa kali au onyo dhidi ya timu hizi. Fikiria namna biashara yao ilivyovurugika. Fikiria hasara ambayo wameingia. Lakini hata wao wenyewe maisha yao yanategemea Simba na Yanga.

Zaidi ya kila kitu ni kwamba hata mashabiki ambao wametumia pesa nyingi kujaribu kufika Temeke wakitokea mikoani nao watarudi tena uwanja wa taifa wakiambiwa kwamba pambano hilo lipo. Hapa ndipo Simba na Yanga wanapodekezwa na mazingira ya mpira wetu.

Angalia taarifa zote zilizotoka tangu sakata hili lianze. Kuna mahala ambapo mashabiki wameombwa radhi?  Hapana. Huwa wanaambiwa tu wawe watulivu. Hakuna anayejali sana gharama zilizotumika kwa sababu hatuna ustaarabu wa kuwajali mashabiki.

Nasubiri kuona ni kitu gani kinaweza kutokea. Kwanza tusubiri kuona Bodi ya Ligi itapanga lini pambano la marudiano. Tuendelee kuona msimamo wa Yanga utakuwa nini. Na wakati tukiendelea kuona msimamo wa Yanga basi tusubiri tu kusiwe na simu za usiku wa manane tuone kama kweli Yanga hawataenda uwanjani. Ninavyojua hawataenda na Simba hawatapewa pointi tatu.

Zitakuwa vurugu nzuri katika soka ambazo zitatufundisha nini kifanyike katika siku za usoni ingawa nafahamu hatutaweza kuiacha hii tabia. Simba na Yanga zinatambua nguvu zao na zinajua namna ya kuzitumia nguvu zao.

Kitu pekee ambacho kinaweza kufanya pambano lisifanyike kam ilivyotokea Jumamosi ni kuwepo kwa majanga ya asili. Labda msiba, ajali, Mafuriko na mengineyo. Mfano pambano la Barcelona na Osasuna lililokuwa lifanyike siku ile ile ya Simba na Yanga lilifutwa kwa sababu Barcelona ilipata msiba wa ghafla wa daktari wa timu hiyo ya Katalunya.

Hata hivyo, sisi tuna maamuzi yetu ya kuahirisha mechi baada ya kuona hali haijakaa vema. Hili liko wazi lakini tumeamua kulibeba na tutaendelea kulibeba kwa siku nyingi. Rafiki yangu Zaka Zakazi amening’ong’oneza kwamba hadi sasa Yanga wanaongoza katika orodha ya kukimbia mechi za Dabi.

Yanga amewahi kuchomoa mara nne wakati Simba amechomoa mara tatu. Tutegemee kwamba hali hii itaendelea kwa muda mrefu iwezekanavyo. Simba na Yanga ni madude makubwa na yenye nguvu kubwa. Ni kama dola fulani hivi iliyojitengeneza ndani ya nchi. Amini usiamini Yanga wanaweza wasicheze pambano lijalo kama busara ya simu ya usiku wa manane haitatumika. Tumeshazoea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *