Hili jipya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Uchaguzi ni njia pekee ya kidemokrasia inayotumiwa na kikundi cha watu, jamii, au Taifa kuchagua viongozi wanaoaminiwa kuwaongoza kwa kipindi kilichokubaliwa kwa mujibu wa katiba au makubaliano ya kisheria na kijamii, iwe kwa maandishi au kwa mdomo.

Hata hivyo, kuwepo kwa uchaguzi ni jambo moja na kuwa na uchaguzi huru na wa haki ni jambo lingine kabisa.

Mara nyingine watu hukubaliana kuhusu namna ya kuendesha uchaguzi, lakini utekelezaji wake unakuwa tofauti na makubaliano hayo.

Katiba ya Zanzibar inaeleza wazi kuwa uchaguzi ufanyike kwa siku moja. Lakini sheria iliyotungwa baadaye imeweka utaratibu wa uchaguzi kufanyika kwa siku mbili.

Baadhi ya wanasheria wanaona kuwa sheria yoyote inayokwenda kinyume na katiba ni batili.

Tunaambiwa kuwa hakuna tatizo kwa sababu mabadiliko hayo yalifanywa kwa “nia njema”, kana kwamba kuwa na nia njema kunawapa waliotekeleza mabadiliko hayo haki na mamlaka ya kufanya hivyo.

Kwa upande mwingine, wanaopinga mabadiliko hayo pia wana nia njema: wanataka Katiba iheshimiwe.

Uchaguzi ni mchakato mrefu na kipimo cha kuwa huru na wa haki hakiwezi kupimwa tu kwa siku ya kupiga kura.

Kuna vigezo vingi vinavyoathiri sifa hiyo, na kasoro yoyote huondoa uhalali wa uchaguzi kama doa kwenye nguo au kiraka kisicholingana.

Uchaguzi huru na wa haki huanza na misingi ya kisheria, ikiwemo kuwepo kwa Tume huru isiyotiliwa shaka.

Hali ilivyo sasa inatia mashaka, kwa sababu baadhi ya maofisa wanaotuhumiwa kuchafua uchaguzi wa 2020 ndio haohao waliorejeshwa kuusimamia uchaguzi ujao.

Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu watu, wakiwamo waliopiga kura katika chaguzi zilizopita, waliokuwa wabunge, wawakilishi, mawaziri, watoto wao na hata wale ambao hawajawahi kutoka Zanzibar, kunyimwa haki ya kujiandikisha.

Wakati huo huo, wapo watu wanaodaiwa kufika Zanzibar mwaka huu na tayari wamepatiwa haki hiyo.

Wakati viongozi wa Serikali wanahamasisha watu kujiandikisha kwa kusema ni haki yao, wapo kimya kabisa kuhusu wale wanaonyimwa haki hiyo.

Kura ya mtu ni siri, lakini hali halisi ya mazingira ya uchaguzi ujao inaashiria kuwa usiri huo unaweza kutoweka.

Katika chaguzi zilizopita, wafanyakazi wa vyombo vya Serikali, idara na mashirika ya umma walikuwa wakilazimishwa kuwasilisha kazini kadi zao za kupiga kura.

Ingawa awali jambo hili lilifanywa kwa siri, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Kitwana Mustafa, sasa ameamua kulitangaza hadharani.

Alipoitisha mkutano na waandishi wa habari, alitangaza kuwa kwa mamlaka aliyonayo ameagiza wafanyakazi wa Serikali na taasisi za umma wawasilishe kadi zao za kupiga kura ili kuhakikisha wamejiandikisha na kuonyesha imani kwa Serikali.

Swali: Je, Mkuu wa Mkoa Kitwana alipata wapi mamlaka hayo? Kisheria, kadi ya kupiga kura ni mali ya mpigakura na mamlaka ya kuidhibiti ni ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, si mtu mwingine.

Kauli ya Kitwana inaendelea kudhoofisha matumaini ya uchaguzi kuwa huru na wa haki.

Ni muhimu kufahamu kuwa Zanzibar haina sheria inayosema kujiandikisha kupiga kura ni lazima.

Ila tunachokifahamu Wazanzibari wote, uamuzi kupiga ama kutopiga kura ni wa mtu binafsi.

Hata mtu akijiandikisha, bado ana haki ya kuamua kupiga kura au kutopiga, au hata kuharibu kura kama ilivyotokea Pemba wakati wa kile kilichoitwa “uchaguzi wa kura za maruhani.”

Kwa bahati nzuri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetoa majibu na msimamo wake juu ya kauli ya mkuu huyo wa mkoa. Huo ni mwelekeo mzuri.

Hata hivyo, bado najiuliza kwa nini haya mambo ya ajabu kama uchaguzi wa siku mbili au viongozi kuhakiki kadi za kupiga kura hayafanyiki Tanzania Bara? Kuna nini kinachoendelea Visiwani?

Kama nia ya mkuu huyo wa mkoa ni kuhakikisha watu wengi wanajiandikisha, basi angeanza kwa kuwapatia haki waliodhulumiwa. Kisingizio cha “nia njema” kisitumike kuharibu uchaguzi.

Mwenendo huu unaweka shaka kubwa kuhusu sifa za uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki. Ni lazima sheria na katiba ziheshimiwe, na watu wapewe uhuru wa kupiga kura bila vitisho.

Mungu aijaalie Zanzibar ipite salama kwenye uchaguzi ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *