Hikma za Nahjul Balagha (69)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 69 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 69 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 61.

الْمَرْأَةُ عَقْرَبٌ، حُلْوَةُ اللَّسْبَةِ.

Mwanamke ni (mithili ya) nge, mng’ato wake ni mtamu.

Katika hikma hii ya 61 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anazungumzia uhakika mwingine kwenye maisha ya mwanadamu kwa kugusia moja ya sifa zenye mgongano za wanawake kwa kusema, mwanamke ni mithili ya nge, kung’ata kwake ni kutamu.

Wafasiri wa Nahjul Balagha wamekuja na tafsiri tofauti kuhusu hikma hiyo ya Imam Ali AS kiasi kwamba hata wametofautiana kuhusu matamshi ya neno la mwisho je linatamkwa lasba au lisba ambayo yana maana tofauti? Katika nakala ya Muhammad Abdul neno hilo limeandikwa kwa matamshi ya lisba kwa maana ya maingiliano na kuamiliana watu. Hivyo kwa mujibu wa nakala hiyo, maana ya hikma hiyo inabidi iwe hivi: Hata kama mwanamke ni mithili na nge, anang’ata na kutafuna na sumu yake ni hatari, lakini kuamiliana naye na kushirikiana naye katika maisha kuna faida na baraka nyingi nzuri na kule kung’ata kwake na zile sumu zake huwa zinafunikwa na mambo mengine mengi mazuri, hivyo inatakiwa kuwa karibu naye. Wanatolea ushahidi wa aya ya 21 ya Surat al Rum ambayo sehemu yake moja inasema:

وَمِنْ آیَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَکُمْ مِّنْ أَنفُسِکُمْ أَزْوَاجاً لِّتَسْکُنُوا إِلَیْهَا

Na katika Ishara Zake Allah ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao.

Vilevile sehemu moja ya aya ya 187 ya sura ya pili ya al Baqarah, Qur’ani Tukufu inasema:

هُنَّ لِبَاسٌ لَکُمْ وَأَنْتُمْ لِبَاسٌ لَهُنَّ

Wao (wanawake) ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao.

Yaani kimaumbile na kidhati, mwanamke na wamanamme ni viumbe wanaokamilishana, mmoja wao hakamiliki bila ya kuwepo mwenzake.

Lakini kwenye nakala nyingi zaidi za Nahjul Balagha neno hilo limeandikwa kwa matamshi ya labsa kwa maana hiyo ya kung’ata na kutafuna na maana hiyo inaonekana inaendana na neno nge na inaonekana ndiyo sahihi zaidi.

Lakini tunapojiuliza, ni vipi Imam Ali AS amemfananisha mwanamke na nge na vipi kung’ata kwake ni kutamu wakati kila mtu anajua mng’ato wa nge ni hatari sana, una sumu na huweza kusababisha kifo? Huenda makusudio hapo ni kwamba, hata kama mng’ato wa mwanamke baadhi ya wakati unakuwa kama sumu ya nge, lakini pembeni mwa mng’ato huo wa sumu kuna upulizaji mwingi mzuri, tiba na dawa nyingi kutoka kwa mwanamke, hivyo kung’ata kwake kunavumilika.

Aidha ni vyema tuseme pia kwamba, mbali na tafsiri hizo mbili, iko na tafsiri nyingine ya tatu ambayo imetolewa na marhum Ayatullah Khalil Kamarah’i ambaye amesema: Makusudio na hikma hiyo ya Imam Ali AS ni kuwaonya wanaume hasa vijana kwamba wachukue tahadhari kubwa na wajiepushe na kusuhubiana na wanawake waovu kwani hao ni nge, sumu zao zinaua na kuangamiza hata kama kijuujuu ung’ataji wao utaonekana kuwa ni mtamu. Wanaume hasa vijana hawapaswi kutekwa na kulaghai wa na uzuri wa nje wa wanawake kama hao kwani wana sumu kali ya kuangamiza.

Lakini tafsiri hiyo nayo inaonekana haiendani na siyaq na matini ya hikma yenyewe kwani lugha iliyotumiwa na Imam Ali AS katika hikma hiyo ya 61 si ya kuonya wala kutahadharisha, bali inazungumzia suala la kuvumiliana na kuishi kwa busara na wanawake. Hivyo tafsiri ya pili na ambayo ndiyo maarufu zaidi, ndiyo inayoonekana inaendana vizuri na matini na siyaq ya maneno hayo ya Imam Ali AS.     

Amma swali jingine linalojitokeza hapa ni kwamba, je, matamshi hayo ya Imam Ali AS yanawahusu wanawake wote? Tab’ani majibu ni hapana, si wanawake wote kwani wako wanawake wengi tu ambao wamepikika kiimani, kimalezi na kitabia kiasi kwamba kamwe hawawang’ati wala kuwatafuna waume zao. Hivyo makusudio hapa ni kuonesha kuwa iwapo mwanamke atapikika kwa imani, malezi mazuri na maadili bora, si tu hawi na sumu ya nge, bali huwa ni tulizo hasa la mume wake na huwa ni pambo la nyumba na kito adhimu kinachosimamia na kuiendesha vizuri familia kwa huruma na upole wake.

Tumalizie na kunukuu hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS ambaye amenukuliwa akisema: Moja ya haki za mwanamke kwa mumewe ni kwamba kama atafanya kosa, basi mumewe awe mwepesi wa kumsamehe yaani (وَاِنْ جَهِلَت غَفَرَ لَها).

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.