Hikma za Nahjul Balagha (68)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 68 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 68 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 60.

اللِّسَانُ سَبُعٌ، إِنْ خُلِّیَ عَنْهُ عَقَرَ

Ulimi ni mnyama hatari, ukiachwa huru hung’ata

Katika hikma hii ya 60 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatutahadharisha kuhusu hatari ya ulimi akisema, ulimi ni kama mnyama mkali na hatari ukiachwa bila ya kudhibitiwa hung’ata na kuangamiza.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba miongoni mwa neema kubwa ambazo Allah amempa mwanadamu na ambazo zinampambanua na viumbe wengine ni ulimi. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana baada ya Mwenyezi Mungu kuzungumzia neema za kuumbwa mwanadamu katika Suratur Rahmani ambayo inamkumbusha mwanadamu neema za Allah, – mara baada ya kutajwa neema ya kuumbwa mwanadamu – Allah ametaja moja kwa moja neema ya ulimi, ya kuweza kuzungumza na kubainisha mambo. Vilevile sehemu kubwa kupindukia ya elimu ya mwanadamu tangu kale hadi hivi sasa inabainishwa kwa ulimi kutoka kizazi hadi kizazi kingine. Lau kama si ulimi na uwezo wa kuzungumza na kubainisha mambo, mwanadamu asingekuwa na tofauti yoyote na wanyama.

Aidha kadiri neema inavyokuwa kubwa ndivyo jukumu lake linavyokuwa kubwa zaidi. Kadiri neema kubwa kama ulimi inavyotumiwa vibaya, ndivyo hatari zake zanavyokuwa kubwa zaidi. Hakuna kiungo chochote cha mwili wa mwanadamu kilicho hatari zaidi kushinda ulimi usiodhibitiwa na usio na breki. Baadhi ya wakati neno moja tu litamkwalo na ulimi huweza kusababisha vita vikubwa duniani, damu kumbwagwa, utulivu kupotea na jamii kutumbukia kwenye ukosefu mkubwa wa usalama. Ndio maana imepokewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW akisema, Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atauadhibu ulimi kwa adhabu kubwa ambayo hatokiadhibu kiungo kingine chochote cha mwanadamu. Ulimi utalalamika na kusema, Ewe Mola wangu, kwa nini mimi ulimi unaniadhibu kwa adhabu kubwa zaidi kuliko kiungo kingine chochote? Mwenyezi Mungu atasema, ni kwa sababu lilitoka neno kutoka kwako ambalo lilifika hadi mashariki mwa dunia na magharibi yake, likasababisha kumwagwa damu za haramu, zikaporwa mali za haramu na zikakanyagwa kiharamu haki za watu wengine. Naapa kwa dhati na utukufu Wangu, nitakuadhibu kwa adhabu ambayo sitokiadhibu kiungo chochote cha mwili wa mtu huyu.

Aidha na kama tunavyojua, sehemu kubwa ya madhambi makubwa yanayoitwa kabair na ya hatari sana, na ambayo yanakadiriwa kufikia madhambi 30, sehemu kubwa ya madhambi hayo yanasababishwa na ulimi usiodhibitiwa, ulimi usio na breki.

Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Baqir AS na ambayo inamnukuu Abu Dharr RA akisema: Ewe unayetafuta elimu, hakika ulimi huu ni ufunguo wa kheri kama ambavyo pia ni ufunguo wa shari, basi udhibiti, ulinde na upige kufuli kama unavyopigia kufuli dhahabu na dirhamu zako.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.