Hikma za Nahjul Balagha (66) – (59)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 66 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 66 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 59.

مَنْ حَذَّرَکَ کَمَنْ بَشَّرَکَ

Anayekutahadharisha ni kama aliyekubashiria kheri.

Katika hikma hii ya 59 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS kama kawaida anabainisha uhakika mwingine muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku kwa kutumia maneno machache yenye balagha ya hali ya juu. Hapa anasema: مَنْ حَذَّرَکَ کَمَنْ بَشَّرَکَ yaani mtu anayekutahadharisha jambo huwa ni sawa na mtu aliyekubashiria jambo la kheri.

Neno hadharaka kwenye hikma hii chimbuko lake ni kuonya, kutahadharisha na kumtanabahisha mtu jambo ambalo lina maslahi kwake na kumuepusha na kupata madhara na hatari iliyoko mbele yake. Ndio maana hapa Imam anatufundisha kuwa, mtu anayekufanyia jambo hilo unapaswa umshukuru na si kumlaumu kwani huwa ni kama vile amekubashiria jambo jema lenye manufaa makubwa kwako.

Inabidi unapotahadharishwa jambo ufurahi kama unavyofurahi unapopata jambo zuri na inabidi mtu anayekutahadharisha umshukuru kwa kiwango kile kile unachomshukuru anayekufayia jambo jema kwani huwa amekuokoa usitumbukie kwenye hatari na jambo lenye madhara kwako.

Naam, tahdhir ni kwa maana ya kutoa onyo kuhusu hatari isiyoepukika au inayoweza kutokea usoni na tabshir ni kutoa bishara ya habari njema na nzuri iliyokaribia kutokea. Sasa kwa vile kuweza mtu kujiepusha na hatari ni ushindi mkubwa kwake, Imam katika hikma hii anasema mtu anayekupa tahadhari kuhusu hatari kubwa na madhara yaliyoko mbele yako ni sawa na mtu aliyekubashiria ushindi katika maisha yako. Ingawa watu wengi wanaona ushindi ni ule unaonekana kwa macho au kuhisika kwa hisia, lakini hapa Imam anatubainishia aina nyingine ya ushindi ambayo huenda tulikuwa hatujaifikiria wala kuitia maanani yaani ushindi unaotokana na kutahadharishwa na kuonywa jambo fulani.

Baadhi ya wakati kuhadharisha kitu kunakuwa na maana zaidi na kunakuwa ni muhimu zaidi kuliko kutoa bishara ya jambo fulani. Utaona Qur’ani Tukufu imelipa umuhimu mkubwa suala la al nudhur, yaani kuonya watu juu ya madhara ya kumuasi Mwenyezi Mungu. Mara nyingi utaona Mitume wa Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani wanawaambia watu wao, hakika mimi ni muonyaji, au mimi ni muonyaji aliye wazi, au nimetumwa kukuonyeni na vitu kama hivyo, hii yote inaonesha kuwa suala la kuonya na kutahadharisha ni muhimu mno kuliko hata kubashiri na kutoa habari njema, ingawa yote mawili ni muhimu. Imetokezea mara nyingine sana, onyo moja tu linabadilisha kabisa maisha ya mwanadamu na ya mataifa ya dunia.

Vile vile imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Baqir AS ndani ya kitabu cha al Kafi ambayo inasema:

 اِتَّبِعْ مَنْ یُبْکیکَ وهُو لَکَ ناصِحٌ وَلا تَتَّبِع مَن یُضحِکَکَ وَهو لَکَ غاشٍّ 

Mfuate anayekufanya ulie lakini akawa anakunasihi na kukutakia mema na jiepushe na mtu anayekufanya ucheke lakini ikawa ni tapeli, bazazi na hakwambii kweli.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.