Hiki ndicho kinachosababisha mgombea kuenguliwa

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa siasa, hamu ya kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, ni kama harakati za kudai nafasi ya kujenga jamii bora.

Lakini, kutimiza matakwa ya kiu yako ya kuwania uongozi huo, kunaambatana na masharti lukuki ambayo ndiyo msingi wa uadilifu na kipimo cha kutimiza matakwa yako.

Uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika,  chini ya kanuni zinazoweka masharti ya uteuzi wa wagombea na sababu za kuenguliwa.

Mgombea anayejitokeza kuwania nafasi za uenyekiti wa kijiji, ujumbe wa halmashauri ya kijiji, au uongozi wa kitongoji, lazima atimize masharti kadhaa ili kuthibitisha utayari wake wa kuwatumikia wananchi.

Lakini safari hii si nyepesi. Kanuni za Uchaguzi wa mwaka 2024 zinaweka wazi kuwa uadilifu, uaminifu na kujitolea ndio msingi wa sifa za mgombea.

Sheria hizi ni nguzo inayolinda haki za wananchi dhidi ya viongozi wanaoweza kutumia nafasi zao vibaya kwa maslahi binafsi.

Sifa kwa mgombea

Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) imeweka kanuni zinazozingatia sifa kadhaa kwa mgombea yeyote anayetaka kushika nafasi za uongozi wa kijiji, kitongoji, au halmashauri.

Kanuni ya 15 ya mwaka 2024 inatoa masharti kama uraia, ambao kila mgombea lazima awe raia wa Tanzania.

Kigezo kingine ni umri kwamba kila mgombea anapaswa kuwa na umri wa miaka 21 au zaidi, kadhalika awe na uwezo wa kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza.

Sifa nyingine ni mgombea anatakiwa kuwa na shughuli halali ya kumwezesha kuishi ili kuwa mfano wa kujitegemea kwa wananchi.

Pia, kanuni hiyo inataka mgombea lazima awe mwanachama wa chama cha siasa kinachotambulika na awe amedhaminiwa na chama hicho.

Kadhalika, mgombea anatakiwa kuwa na akili timamu ili kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Sababu mgombea kuenguliwa

Kinyume na matarajio ya wengi, si kila mgombea anayejiandaa kugombea huendelea hadi mwisho wa safari. Wapo ambao, kutokana na sababu mbalimbali, hujikuta wakiondolewa.

Mgombea anayekosa sifa zozote zilizotajwa katika kanuni ya 15, atakuwa hana haki ya kuendelea na mchakato wa kugombea.

Hii inahusisha wale ambao hawajafikisha umri unaohitajika, ambao si raia wa Tanzania au ambao hawajajiandikisha kama wapiga kura kwenye eneo husika.

Hii ni hatua ya awali ya kuhakikisha kuwa nafasi ya uongozi inashikiliwa na mtu aliyekidhi vigezo na mwenye sifa inayotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Kukosa sifa za msingi

Kanuni ya 16 (1)(a), inaweka wazi kuwa mgombea anayekosa sifa zozote zilizotajwa katika Kanuni ya 15 atakosa haki ya kuendelea na mchakato wa kugombea.

“Mtu hatakuwa na sifa za kugombea nafasi ya uenyekiti wa kijiji, ujumbe wa halmashauri ya kijiji au uenyekiti wa kitongoji endapo: amepoteza au hana sifa za mgombea zilizoainishwa katika kanuni ya 15,” kinaeleza kifungu cha 16 (1)(a) cha kanuni hiyo.

Hii inahusisha wasiofikisha umri unaohitajika, wasio raia wa Tanzania, au ambao si wakazi wa eneo la kitongoji husika.

Hii ni hatua ya awali ya kuhakikisha kuwa nafasi ya uongozi inashikiliwa na mtu aliyekidhi vigezo na mwenye sifa inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi.

Aidha, kifungu cha 16(1)(b), kinataja miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyomzuia mgombea kuendelea ni historia ya kihalifu.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, mgombea aliyewahi kuhukumiwa kifungo kinachozidi miezi sita gerezani, au aliyepatikana na hatia ya uhalifu mkubwa, hana haki ya kugombea.

“Amehukumiwa kifungo kinachozidi muda wa miezi sita gerezani au hukumu ya kifo na Mahakama za Tanzania,” kinaeleza kifungu cha 16(1)(b).

Mgongano wa maslahi ni sababu nyingine ya wagombea kuenguliwa kama inavyofafanuliwa katika kifungu cha 16(1)(c) cha kanuni hiyo.

Kanuni hiyo, inatambua umuhimu wa kuzuia migongano ya maslahi kwa wagombea.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mgombea yeyote mwenye maslahi ya kifedha katika kampuni inayofanya biashara na mamlaka ya serikali ya mitaa ambayo anataka kuiongoza, lazima afichue maslahi hayo kupitia matangazo rasmi.

Kama atashindwa kufanya hivyo, mgombea huyo huondolewa kama hatua ya kuzuia matumizi mabaya ya nafasi za umma kwa manufaa binafsi.

“Ana mkataba au maslahi kwenye kampuni ambayo ina mkataba na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambayo anagombea nafasi ya uongozi na hajatangaza kuwepo kwa mkataba au maslahi yake kupitia kwenye gazeti linalopatikana katika eneo husika au mbao za matangazo katika ofisi ya kijiji,” kinaeleza kifungu cha 16(1)(c).

Kukosa haki ya kupiga kura ni sababu nyingine inayomwondolea sifa mgombea kwa mujibu wa kifungu cha 16(1)(d) cha kanuni hiyo.

Kifungu hicho kinaeleza mgombea atapoteza sifa iwapo, “Amepoteza sifa ya kupiga kura chini ya kanuni hizi.”

Haki ya kupiga kura ni msingi wa kushiriki kwenye uchaguzi. Mgombea asiyejiandikisha au anayekosa sifa za mpiga kura, kama zilivyoainishwa kwenye kanuni, atakuwa hana haki ya kupiga kura.

Kuteuliwa au kuchaguliwa kwenye wadhifa mwingine ni sababu nyingine inayomwondolea sifa mgombea kama inavyoelezwa katika kifungu cha 16(1)(f).

Chini ya kifungu hicho, mgombea aliyeteuliwa au kuchaguliwa kushika nafasi yoyote ya utumishi wa umma au nafasi za juu kama vile udiwani, ubunge, au uspika hana sifa za kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa.

Hii ni hatua inayolenga kuzuia migongano ya kimaslahi na kujiepusha na mgombea anayeshikilia zaidi ya nafasi moja inayohusiana na utumishi wa umma.

Mgombea atapoteza sifa iwapo, ataajiriwa au kuteuliwa katika wadhifa wowote katika utumishi wa umma au kuchaguliwa katika nafasi ya udiwani, ubunge, uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imekuwa ikichukua hatua kali za kuhakikisha kuwa wagombea wote wanaohusishwa katika uchaguzi wa mwaka 2024 wanatimiza masharti ya msingi.

Wadau wa uchaguzi wanaeleza kuwa sheria hizi zimechangia kuongeza uwajibikaji kwa wagombea.

Hatua hiyo inalenga kuwa na mfumo unaolenga kuepusha utumizi mbaya wa rasilimali za umma na kuhakikisha kuwa viongozi wanaochaguliwa ni wale wanaotambua na kuheshimu sheria.

Wakati huo huo, baadhi ya wagombea walioondolewa wamelalamikia utaratibu huu, wakidai kuwa vigezo vingine ni vikali kupita kiasi na vinaweza kuwazuia wananchi wengi wenye nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi katika mitaa, vijiji na kata zao.

Hata hivyo, Tamisemi inasisitiza kuwa kanuni hizi ni muhimu kwa ajili ya ulinzi wa haki na uwajibikaji wa viongozi, ingawa ni muhimu haki na usawa uzingatiwe.

Kuenguliwa kwa mgombea si jambo la furaha kwa mgombea yeyote mwenye lengo la kushika nafasi za uongozi.

Hata hivyo, ni lazima ikubalike kuwa masharti haya yanachochea uadilifu na uwajibikaji katika uongozi wa serikali za mitaa.

Hatua hizi zinalenga kutoa nafasi kwa wagombea wenye sifa na kwa kufanya hivyo, zinalinda haki na matumaini ya wananchi ambao wanatarajia viongozi waaminifu na wacha Mungu.

Kwa wananchi, hiki ni kipindi cha kutafakari na kujiandaa kupiga kura kwa kigezo cha uadilifu.

Ni wajibu wa kila mpiga kura kuhakikisha anatoa nafasi kwa mgombea anayefuata maadili, na anayewajibika kwa jamii.

Ni kwa kufanya hivyo, tutaweza kujenga jamii yenye maadili mema na inayoongozwa kwa haki.

Kanuni hizi za uchaguzi, zilizopitishwa mwaka 2024, ni hatua muhimu kwa mustakabali wa demokrasia na maendeleo ya taifa letu.

Ni wito wa kujenga nchi inayojali maadili na kuwachagua viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.