
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara, Amani Golugwa amesema wapo tayari kufanya kazi na Dk Slaa akikubali kufuata itikadi na falsafa ya chama hicho ikiwamo kujibu maswali ya aliyoyasema wakati anajitenga na chama hicho mwaka 2015.
Msingi wa kauli ya Golugwa ni kile kilichoelezwa na Dk Willibrod Slaa kuwa atafanya kazi na Chadema kwa kufuata itikadi zao.
Golugwa amesema hayo alipozungumza na Mwananchi leo Machi mosi, 2025 kuhusu kauli ya Dk Slaa (76), kwamba yupo tayari kurejea Chadema, chama alichowahi kukitumikia.
Dk Slaa akiwa Katibu Mkuu wa Chadema wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, alitangaza kujiweka kando.
Akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kuachiwa huru kutokana na kesi dhidi yake kufutwa na Mahakama Februari 27, 2025, Dk Slaa alisema yupo tayari kurudi Chadema, akieleza mwanzo alikuwa mwanaharakati lakini sasa yupo tayari kurudi kwenye chama hicho.
“Kile tulichokipigania wamekiweka wazi, kile kilichoniondoa mwaka 2015 kimeshafutika, sasa hivi sina tatizo lolote kufanya kazi karibu zaidi na Chadema kwa utaratibu wa Chadema,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi, Golugwa amesema: “Hata mimi nimemsikia na niliongea naye Dk Slaa. Chadema ni chama cha watu, kipo tayari kufanya kazi na mtu yeyote anayeamini falsafa yetu, kukubaliana na itikadi pamoja na misimamo yake.
“Chadema kipo tayari kufanya kazi na Mtanzania yeyote bila ubaguzi ilimradi tukubaliane naye kwanza. Katika kumbukumbu zetu hatukuwahi kumfukuza Dk Slaa, kama yupo tayari akija kuna maswali tutamuuliza, kwamba wakati anaondoka kuna maneno yalizungumzwa ninaamini atakuwa na hayo majibu.”
Golugwa amesisitiza kuwa Chadema ni chama cha watu, kipo tayari kufanya kazi na mtu yeyote pasipo ubaguzi, akiwemo Dk Slaa.
Kufuatia msimamo huo, Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema ingawa ni vigumu kujua kilichomwondoa mwanasiasa huyo, lakini inakumbukwa alitofautiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuhusu Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Kulikuwa na mabishano yeye na mwenyekiti wake kuhusu mtu anayetakiwa kupeperusha bendera ya chama katika urais mwaka 2015. Dk Slaa alisema mtu ambaye walizunguka kumsema kama fisadi lakini leo anataka urais na wanatakiwa kumfanyia kampeni.
“Katika misingi ya kisiasa ni kama vile kula matapishi yako, sasa Dk Slaa alikuwa anaamini kwenye utu, hakuwa tayari kulifanya hilo, ndiyo maana aliondoka. Ni rahisi kusema kwamba kile kilichomfanya aondoke hakipo tena,” amesema Dk Mbunda.
Hata hivyo, zipo taarifa nyingine, kwamba njia ya Lowassa kwenda Chadema ilisafishwa na Askofu Josephat Gwajima, ambaye alifikisha taarifa hizo kwa Dk Slaa na kisha kwa Mbowe.
Hata hivyo, Dk Mbunda amesema ni kama vile Dk Slaa alishakubali kurudi CCM na kiasili katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema ni mwanasiasa.
“Kwa tathmini yangu inawezekana CCM imeshindwa kumtumia vizuri kwa hiyo anajiona yupo katikati, ndiyo maana akaamua kufanya siasa za upinzani hata kama alikuwa bado CCM,” amesema.
Kwa upande wake Dk Aviti Mushi, mhadhiri UDSM, mbali na kusema Dk Slaa aliondoka Chadema baada ya kutofautiana na Mbowe kuhusu ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho, amesema hata akirejea Chadema hawezi kuwa na ushawishi kama ilivyokuwa zamani kwa sababu muda wake umeshapita.
“Sidhani kama siasa za sasa ataziweza maana zimebadilika. Alishapoteza, hana tena ushawishi ni ni bora angekaa kando baada ya kutoka Chadema, lakini alipopewa wadhifa akaanza kuwaponda Chadema na kuwaharibia,” amesema.
Hata hivyo, Mwanasheria na mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema: ” Kama alitofautiana na mwenyekiti (Mbowe) ambaye hivi sasa hayupo, anaweza kwenda kwa sababu awali alionekana kumpigia debe Tundu Lissu (mwenyekiti mpya).
“Akiweza kurudisha imani anaweza kuwa na ushawishi tena, kikubwa ni kuonyesha kwa nini aliondoka Chadema. Lakini itategemea namna ambavyo atazichanga karata zake.
“Mwanzoni alionekana kama kujiingiza kwenye siasa za kiharakati, sasa ilikuwa vigumu kuingia Chadema kwa wakati huo ingawa walikuwa wanashirikiana kwenye baadhi ya harakati. Sasa ametumia nafasi hii kumuunga mkono Lissu ili iwe rahisi kurudi,” amesema.
Dk Kyauke amesisitiza kuwa bado Dk Slaa ana ushawishi katika siasa kwa sababu hakuondoka Chadema kwa kufanya kitu kibaya, bali walitofautiana na kiongozi mwenzake.