Dar es Salaam. Siku ya hivi karibuni nilikwenda kwenye shoo ya ‘stand up comedy’ inayoitwa All Stars ambayo iliandaliwa kama sehemu ya kujiandaa na Tuzo za Comedy Tanzania zilizotolewa Februari 22,2025. Nikiwa pale walipanda wasanii wengi, lakini nilifurahi alipopanda mchekeshaji Jolmaster sio kwa sababu ya kuchekesha tu, lakini kwa sababu ya mada aliyozungumzia.

Jolmaster alikuwa anazungumzia muziki wa Amapiano, akasema Amapiano ili iwe Amapiano inahitaji vitu vitatu tu – biti iliyochangamka, neno moja linalojirudiarudia na ‘dance challenge ya Tiktok’. Na ili kuthibitisha anachosema akiwa hapo hapo jukwaani Jolmaster alimuomba DJ amuwekee biti ya Amapiano iliyochangamka, akawekewa.

Kisha akatuuliza watazamaji aimbe neno gani? Mtazamaji mmoja akasema neno ‘Kimya’. Na ndani ya sekunde kadhaa Jolmaster akaanza kuimba neno kimyakimya huku akicheza na huwezi kuamini kilichotokea ilikuwa ni kama ngoma nyingi ambazo zinahiti mtaani kwa sasa.
Nilichofurahia ni kwamba alichosema Jolmaster ni kitu ambacho nimekuwa nikikizungumza sana, kwamba muziki wa Amapiano sio muziki ambao msanii anaweza kuutegemea. Na hapa naomba tuelewane wanangu sina maana kwamba wasanii wasiimbe Amapiano, hapana waendelee kuimba tu kwa sababu inaonekana huku mtaani watu wanaupenda huo muziki. Una vibe, unachezeka, ni muziki fulani unanoga ukiwa na furaha au maeneo ya kula bata.
Nachosema ni kwamba, Amapiano ni muziki rahisi sana kiasi kwamba kama msanii ametoka enzi za Amapiano na akaimba ngoma za Amapiano siku zote, asijidanganye kwamba naye ni msanii wa muziki. Ikiwezekana kwa sasa ajiite msanii wa Amapiano mpaka siku atakapopata ujasiri wa kufanya ngoma ambayo sio Amapiano na ikaenda mjini kama Amapiano zake.

Wasanii kama Chinno Kid ambao walianza kama madansa kisha Amapiano ilipoanza kubamba wakaanza kuimba. Watu kama Jaivah ambaye alikuwa mwanamuziki kitambo, lakini amehiti kipindi cha Amapiano kupitia Amapiano. Lukamba ambaye alikuwa ni mpigapicha wa Diamond alipoachana na shughuli hiyo na kujitosa kwenye muziki na kuimba Amapiano huu ni ujumbe wao.
Amapiano ni muziki rahisi sana mtu yeyote anaweza kuimba Amapiano watake wasitake ukweli ndiyo huo. Kinachofanya ngoma za Amapiano ziende ‘viral’ sio kwa sababu ni ngoma kali, bali kwa sababu ya vitu vingine kama vile staili nzuri za kucheza na mada inayoogelewa kwenye wimbo.

Lakini wakae wakijua kila aina ya muziki huja na kupotea. Kama ambavyo ilikuja Kwaito ikaondoka, kama ambavyo ilikuja Afro Pop ya Kinaijeria na kuondoka ndivyo ambavyo Amapiano itaondoka tena muda si mrefu. Kwa hiyo ni ama wasanii wa waliohiti na Amapiano waanze kujifunza miziki mingine ambayo inaonyesha nguvu zao za uimbaji au waanze kutafuta shughuli zingine za kufanya. Wakigoma kufanya hivyo maisha yao ya muziki yatakuwa mafupi sana.