
Leo tutaongelea suala nyeti na tata kidogo ambalo wengi huwa hawaliongelei au wasingependa kuliongelea.
Hata hivyo, kama wahusika wataliongelea na kujua faida, ulazima, na umuhimu wake, wajitahidi kulifanyia kazi kwa faida na furaha ya ndoa zao.
Kabla ya kuzama, tuanze na maumbile ya binadamu. Kiasili, kila kilicho na uhai kina sifa ya uchafu wa kimwili. Hii ni kutokana na ulazima wa kupata lishe ili kuishi.
Hivyo, kiumbe alapo chakula au kunywa kinywaji kuondoa njaa na kiu mtawalia, lazima atatoa mabaki ya vitu hivi ambayo kiasili ni uchafu wenye kutoa hata harufu mbaya.
Japo binadamu hawalingani katika hili, wote hula na kutoa uchafu. Hivyo, huchafuka. Wengi wanaweza kujiuliza. Hili linahusianaje na ndoa. Lina uhusiano mkubwa tu.
Kwa wale ambao wamebahatika kusafiri katika baadhi ya nchi, watakubaliana nasi kuwa kuna nchi, ukiingia kwenye usafiri wa umma, unakutana na harufu mbaya iwe ni ya jasho au mengineyo.
Mwandishi wa Zimbabwe Tsitsi Dangarembga amewahi kuligusia hili japo kifasihi kwenye kitabu cha maarufu cha Nervous Conditions.
Hapa tunachomaanisha ni kwamba binadamu, sawa na viumbe wengine, ni wachafu hasa wasipojisafisha vilivyo na mara kwa mara.
Kwa siku, binadamu hula na kunywa na kutoa uchafu. Hivyo, uhitaji kujisafisha mara kwa mara. Hili lisipofanyika, husababisha baadhi ya watu kunuka.
Ni ushahidi kuwa hawafanyi usafi ipasavyo.
Je kama mtu baki unayepanda usafiri wa umma na kukutana na harufu kama hizo, hali ikoje kwa wanandoa wanaolala pamoja? Msijiruhusu kulala wachafu. Kwani, mtatengeneza tatizo katika uhusiano wenu.
Kwa wale wenye mazoea ya kulala bila kuoga au angalau kutawaza, kwa wale wasiofanya hivyo kutokana na kuishi kwenye sehemu za baridi, hakikisha angalau unatawadha kabla ya kulala.
Tuliwahi kuongelea kisa cha wanandoa fulani kutushangaa tulipokwenda kupiga mswaki wakati wa kwenda kulala.
Walisema wakipiga mswaki hawawezi kupata usingizi. Je hii ni kweli au imani tu? Huu ni ushahidi tosha kuwa kuna wanandoa wanaolala bila kuoga, kupiga mswaki, au kutawaza. Si tabia njema kiafya na kiuhusiano.
Hatutaki kuwafanya wasomaji wetu kuwa watoto wadogo kiasi cha kuwakumbusha mambo muhimu na ya msingi kama kupiga mswaki, kuoga au kutawaza kabla ya kulala.
Tusisitize. Usafi wa mwili ni muhimu kwa wanandoa sawa na watu wengine. Miili yetu, kiasili, ni michafu. Hivyo, uhitaji usafi wa mara kwa mara. Hapa lazima tuseme. Kuna mila nzuri kuiga. Mfano, Uislam, uhimiza usafi wa mara kwa mara kutokana na kuyajua maumbile ya binadamu.
Kwa jamii kama vile za kizungu zinazopenda kutumia karatasi (toilet tissues) kutawadhia, uwezekano wa watu kunuka ikilinganishwa na wale wanaotumia maji kwa shughuli hii.
Hivyo, bila aibu, tuseme wazi. Usijiruhusu hata siku moja kulala bila kutawadha. Hatutaki kuingia kwenye bailojia ya maumbile.
Kwa ufupi, itoshe kusema kuwa kupiga mswaki na kutawaza kabla ya kulala ni muhimu kuhakikisha mwili wako unakuwa safi.
Tafiti zimeonyesha kuwa wanandoa wasafi wana uwezekano mkubwa wa kuwa na uhusiano mzuri na yenye siha.
Jarida la Healthdor (Septemba, 2024) linaripoti kuwa usafi hujenga kujiamini na kujithamini.
Pia, jarida linaripoti kuwa kulala pamoja katika hali ya usafi huongeza upendo tokana na homoni ya mapenzi oxytocin ambayo huimarisha muunganiko wa hisia kwa wahusika.
Kwa upande wa pili, Jarida Healthdor linatahadharisha kuwa kutofanya uchafu kunaweza kusababisha maambukizi kwa wanandoa wanaolala pamoja.
Jarida la Huffington (Novemba, 2022) lilimkariri Dk. Karan Raj akisema kuwa unapooga maji ya uvuguvugu wakati wa kwenda kulala si unakuwa safi tu bali husababisha vasodilatation au kupanuka kwa mishipa ambako huwezesha damu kusafiri vizuri na hivyo, kuwa na usingizi mzuri.
Na hii inapotokea, unakuwa na uwezo wa kufanya yale wafanyayo wanandoa kama kushiriki chakula cha usiku vizuri.
Tuhitimishe kwa wale wenye utamaduni wa kuoga, kupiga mswaki, na kutawadha tunawashauri wasiache. Wawafundishe hata watoto wao.
Kwa wale wasiokuwa na utamaduni huu, tunawashauri waanze mara moja. Tutaomba maoni ya wahusika kama watakuwa tayari kufanya hivyo.