Dar es Salaam. Imekuwa nadra kwa abiria wa mabasi ya mikoani kufanya safari zao bila kutazama movie za Abdallah Mzunda ‘Mkojani’ ndani ya vyombo hivyo vya usafiri.
Usipokutana nayo wakati wa kwenda basi unaweza kukutana nayo wakati wa kurudi. Na hichi ndicho kimeendelea kumfanya Mkojani kupendwa na kufuatiliwa na wengi.
Akizungumza na Mwananchi mchekeshaji huyo aliyeanza kufanya sanaa ya maigizo ya vichekesho mwaka 2004, amesema, kazi zake zinagusa hadhira yoyote ndiyo maana anapendwa na watu wa rika zote.

“Kuonekana mara kwa mara kwenye magari ya mkoani ni kwa sababu nafanya vitu ambavyo havibagui. Kwenye gari anaweza kupanda mtu na mkwewe, watoto au familia. Ninaangalia sana burudani yenye kuelimisha na kufurahisha,” anasema Mkojani.
Hata hivyo, anasema kwa sasa maigizo ya vichekesho ndiyo yanashika namba moja yakifuatiwa na Bongo Movie ambayo awali ilikuwa inatikisa.
“Tumepambana mpaka kuhakikisha komedi inakuwa namba moja kama vile Bongo Fleva inavyoongoza. Kwenye maigizo ipo wazi kabisa tumewatoa wenzetu miaka ya nyuma walikuwa namba moja sasa hivi wapo namba mbili,”anasema.
Anasema licha ya kushika namba moja kwa sanaa hiyo bado kuna changamoto ya uwekezaji ili kuiwezesha komedi ya Tanzania kwenda kimataifa.
“Komedi kuvuka mipaka inahitajika uwekezaji mkubwa, kwa sisi maprodyuza wadogo wa ndani hatuwezi kufanya kazi za kimataifa tutadanganyana. “Tutakuwa tunafanya hizi local movie ambazo zinaishia Afrika Mashariki.
“Lakini kwenda kimataifa ni kazi kubwa inahitaji mabilionea kwa hiyo wakitokea wawekezaji wakaamini katika kuwekeza tunaweza kwenda Kimataifa,” anasema.
Licha ya Mkojani kufanya kazi na wasanii wengi kama vile Samofi, Tin White, Masanja, Kingwendu na wengineo anasema kwenye upande wa wasanii wa Bongo Movie kiu yake kubwa ni kufanya kazi na mwigizaji Gabo Zigamba kwani yuko vizuri na mweledi kwenye kazi zake.
Hata hivyo, safari ya Mkojani kwenye sanaa unaweza kuifananisha na msemo usemwao “Ili dhaabu ing’ae lazima ipitishwe kwenye moto” hii ni kutokana na msoto aliopitia wakati akijitafuta kwenye sanaa.

“Matukio ni mengi sana nimekutana nayo kwenye safari yangu ya kujitafuta. Kuna manyanyaso, kutengwa , kutembea kwa mguu, kutafuta nafasi na kuzikosa.
“Familia pia inakuwa haikuamini miaka ya zamani watu walikuwa wanaaminiwa kwenda kwenye mambo ya gereji, ufundi na biashara usanii kwenye familia walikuwa hawaamini kama inaweza kuwa kazi tofauti na sasa familia zinaona umuhimu wake,” anasema.
Kama ilivyo kwa baadhi ya mastaa kukutana na hekaheka mbalimbali kutokana na umaarufu wao Mkojani anasema umaarufu unamgharimu katika kuishi licha ya kuwa faida zake ni nyingi zaidi kuliko hasara.
“Umaarufu unatugharimu katika kuishi unaweza ukafika sehemu wenzako kitu wanauziwa elfu 20 wewe ukauliza bei ukaambiwa elfu 60 ukimuuliza mtu anasema wewe una hela.
“Sijawahi kujuta kuwa maarufu na ndiyo maana sisi tunatumia mawinga kwenda kwenye masoko kwa sababu wakituona wanaamini sisi tuna pesa nyingi za kuuziwa vitu ambavyo siyo thamani yake,”anasema.
Anaongezea kuwa kwa mtu anayetamani kuwa kama yeye siyo rahisi lazima ajiongeze, awe mbunifu, kumshirikisha Mungu na kuacha dharau kwani safari ya umaarufu na mafanikio ina milima na mabonde.
Utakumbuka Mkojani anatamba na movie kama Cha 2000, Dingi Mtata, The Magic, Mazingaombwe, Tarehe 1 na nyinginezo
”Sipendi mnafiki, chuki roho mbaya msanii akiwa hivyo sipendi na ninamwambia mapema na sivipendi kwenye kazi nikimuona mtu wa hivyo huwa namwambia au namkataa yaani namuepuka.”