Hii ndio namna ya kucheza twisti kwa wanawake na wanaume

Dar es Salaam, Mwanzoni mwa miaka ya 60 vijana wa kizazi kipya wa nyakati zile wakaingiza mtindo mpya wa uchezaji dansi kutoka Marekani, mtindo huo uliitwa twisti. Uchezaji wa twisti ulikuwa ni kunengua kwa kuzungusha visigino tofauti sana na twisti inavyochezwa siku hizi ambapo kinachozungushwa ni kiuno. 

Lakini hata hivyo wazee wa miaka hiyo waliipiga vita sana twisti, kuna wanafunzi waliwahi kufukuzwa shule kwa kuonekana wanacheza twisti, mtindo ulioonekana kuwa ni ucheza wa kihuni. 

Bendi nazo zilianza kubuni mitindo yake na kuanza kugundua aina za uchezaji wake, ikazaliwa mitindo kama, Msondo, Mundo, Segere, Dondola, Kiweke na kadhalika. 

Katika kucheza mitindo hii mipya kulikuwa na tofauti ya uchezaji kati ya wanaume na wanawake. Wanaume walicheza zaidi wakitikisa vifua vyao kuonyesha kuwa wao ni wanaume.

Katika miaka ya sabini, utamaduni wa bendi kuwa na ‘wacheza show’ukaanza. Kwa vile utaratibu huu uliigwa kutoka bendi za Kongo.

Hata uchezaji wake uliiga sana uchezaji wa Kikongo, ingawaje kulikuwa na bendi ambazo wachezaji wake walikuwa wabunifu na kuanza kugundua uchezaji wao, na uchezaji huo ukawa unaigwa na wapenzi wa bendi hizo. 

Katika miaka ya karibuni kumekuwa kama hakuna tofauti kati ya uchezaji wa kiume na wa kike, unenguaji wa kiuno ambao zamani ilikuwa sifa hasa ya wachezaji wa kike, siku hizi si ajabu kabisa kukuta mwanaume akikatika kiuno kwa ufanisi  wa hali ya juu kuliko wanawake wenye asili yao. Na uchezaji huu wa kukata viuno kwa sasa  uko katika kila aina ya muziki kuanzia taarab, dansi, singeli mpaka  Bongo Fleva.