Dar es Salaam. Wakati maandalizi ya kulifungua tena soko la Karikaoo yakiendelea, wafanyabiashara wameanza kupewa mikataba ya upangishwaji vizimba huku moja ya masharti ni kutakiwa kulipa kodi ya kizimba kuanzia Sh100,000 hadi Sh120,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh1.2 hadi Sh1.4 milioni kwa mwaka.
Soko hilo lilikuwa katika ukarabati tangu Januari 2022 baada ya kuungua mwaka 2021 na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara kwa mali zao kuteketea kwa moto.
Kutokana na hilo, Serikali ilitenga Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, ukarabati ambao ulienda sambamba na ujenzi mpya wa soko dogo litakalokuwa na ghorofa nane.
Katika kipindi chote cha ujenzi, wafanyabiashara hao walihamishwa masoko ya Kisutu, Machinga Compex na Karume ili kupisha ujenzi huo.
Katika urejeaji huo, kodi imeonekana kuwa tofauti na ilivyokuwa awali huku sababu ikitajwa kuwa na maboresho yalivyofanywa.
Kwani ukicha kodi hiyo, pia wafanyabiashara hao watapaswa kulipia huduma ya umeme, usafi, ulinzi na lifti ambavyo vyote hivi ni Sh10,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh120,000 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na baadhi ya wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda ambao wameshakabidhiwa mkataba huo, wiki mbili zilizopita, huku wakieleza ongezeko hilo na kueleza ni kubwa kwao ukilinganisha na biashara wanayoifanya.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Mei 6, 2025, Meneja wa Shirika la Masoko, Ashraph Abdulkarimu, amekiri kuwepo ongezeko la kodi hiyo.
Akifafanua sababu ya kupanda kwake ambayo awali ilikuwa ni Sh612,000 kwa mwaka, Abdulkarimu amesema ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika soko hilo.
“Zamani wafanyabiashara hawa walikuwa wakipanga bidhaa zao chini, lakini kutokana na maboresho ya ujenzi yaliyofanywa sasa watapanga kwenye vizimba juu na watakuwa na eneo pia la kuhifadhi bidhaa zao hivyo kodi haiwezi kuwa kama ya zamani,” amesema Meneja huyo.
Aidha amesema jambo hilo wafanyabiashara hao walikuwa wakilijua kwani walishaambiwa kwenye vikao mbalimbali walivyoketi na uongozi wa Mkoa ambao ndio ulikuwa ukisimamia ujenzi huo.
Walichosema wafanyabiashra
Hamza Abdallah, mmoja wa wafanyabiashara hao, amesema wakati wakiwa sokoni hapo kwa siku walikuwa wakilipa Sh1700 hivyo kwa mwezi walikuwa wakilipa Sh51,000 sawa na Sh612,000 kwa mwaka.
Hivyo kutokana na mkataba huo itabidi kwa siku walipe Sh4,000 ambayo kwa mwezi ni Sh120,000, wakati msingi wake ni Sh30,000.
Amesema katika biashara hiyo ya mbogamboga na matunda kwa siku faida yake haiwezi kuzidi kati ya Sh6,000 hadi Sh7,000, hivyo mkataba huo hawakubaliani nao licha ya kuwa wameusaini.
Alipoulizwa sababu ya kuusaini nini wakati hawakubaliani nao, Abdallah amesema wameamua kufanya hivyo huku wakiendelea kupaza sauti zao kwa kuwa wanahofia yote hayo yanafanyika malengo ikiwa ni kuondolewa sokoni hapo jambo ambalo hawapo tayari.

“Katika mambo kama haya huwezi kupambana na serikali, hivyo tumeamua kusaini mkataba huo huku tukiendelea kupambania haki yetu,” amesema Abdallah.
Hata hivyo walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa nia yake njema ya kuwajengea soko hilo lakini walimuomba kuyafanyia kazi malalamiko yao hayo.
Naye Mwenyekiti wa soko la Shimoni, Ramadhani Kakundilo, amesema katika upangaji wa bei hizo za kodi walitegema wangeshirikishwa ili nao kutoa maoni yao, lakini badala yake wamekutana nalo kwenye kusaini mkataba.
Kakundilo amesema suala hilo la ushirikishwaji, hawajui kwa nini limekuwa likikepwa na mamlaka tangu awali katika upangaji majina jambo linalozidi kuwapa wasiwasi namna watakavyoweza kufanya biashara chini ya Shirika hilo.
Rashid Salum, ambaye ni mjumbe pia wa soko la wazi, amesema yupo tangu mwaka 2009 sokoni hapo na hali ya biashara wanaijua huku akipendeeza mkataba huo urekebishwe walau walipe Sh1,500 kila siku.
Hussein Iddi, amesema ndani ya mkataba huo unasema ungeanza Mei 2025 lakini mpaka wanapozungumza sasa soko halijafunguliwa na hawajui itaanza kuchajiwa lini.
Lakini pia wapo baadhi waliopewa mkataba wakati hawajaonyeshwa vizimba jambo alilolifananisha ni sawa na kusainishwa mkataba wa kupangishwa nyumba ambayo hujawahi kuiona.
Akilijibia hilo, Meneja wa Shirika la Masoko, amesema matarajio ni soko hilo kufunguliwa muda wowote kuanzia sasa isipokuwa kuna vitu vidogovidogo klatika ujenzi vvimebakia na pia kuweza kukabidhiwa rasmi.
Kuhusu kutoonyeshwa vizimba kwa baadhi ya wafanyabiashara, amekiri ni kweli na kueleza kwamba mkandarasi wa ujenzi alishauri shughuli ya kuendelea kuwaonyesha watu vizimba iliyoanza kufanywa Aprili 10, 2025 kusitishwa kwani ingeweza kuathiri kazi yake na pia kulinda usalama wa wafanyabiashara hao.