Hii Ligi Kuu, ni mwendo wa namba tu

Jana Jumapili kulikuwa na mechi mbili za Ligi Kuu Bara ikiwa ni mzunguko wa 18 katika duru la pili.

Katikati ya wiki iliyopita zilipigwa mechi za raundi ya 17 zikianza kuchezwa Februari 5 hadi 7 huku ushindani ukiongezeka kwa baadhi ya timu wakati zingine zikibaki vilevile.

Ushindani ulioongezeka kwa baadhi ya timu umetoa majibu ya namna zilivyojiimarisha katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15 mwaka huu.

Mwananchi linakupitisha katika mambo mbalimbali kuhusu ligi hiyo hadi hapa ilipofika huku Yanga ikiwa kileleni na pointi 45 ikifuatiwa na Simba yenye 44.

KENGOLD MAJANGA

Licha ya kufanya usajili wa wachezaji zaidi ya 10, lakini KenGold kutoka Mbeya haijatibu tatizo la kuruhusu mabao mengi katika mechi moja zaidi tatizo limeongezeka.

KenGold ambayo inaendelea kuburuza mkia katika msimamo wa ligi kuu ikikusanya pointi 6 katika mechi 17, imetoka kufungwa 6-1 na Yanga huku jumla ikiruhusu mabao 35, yakiwa ni mengi zaidi ya timu zote shiriki.

Timu hiyo pia imekuwa na rekodi mbaya ya matokeo kwani ukiweka kando kichapo walichotoka kupokea, katika mechi tano za mwisho ndiyo timu pekee iliyopoteza zote. Haijaambulia hata sare.

Tangu mara ya mwisho Novemba 23, 2024 iambulie sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union, imepoteza mechi tano mfululizo dhidi ya Pamba Jiji (1-0), Namungo (3-2), Simba (2-0), Singida Black Stars (2-1) na Yanga (6-1). Kituo kinachofuata ni leo Jumatatu dhidi ya Fountain Gate.

Wakati KenGold ikipoteza mechi zote tano za mwisho, vinara wa ligi hiyo, Yanga ndiyo timu pekee iliyoshinda mechi zote tano zilizopita ikifunga mabao 23 na kuruhusu moja pekee.

Yanga katika mechi tano zilizopita imezifunga Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), Fountain GAte (5-0), Kagera Sugar (4-0) na KenGold (6-1).

Kocha Mkuu wa KenGold, Mserbia Vladislav Heric, ana kazi ya ziada kuhakikisha anaboresha maeneo yanayoonekana kuwa na changamoto ikiwemo ulinzi na ushambuliaji.

Ukiweka kando katika ulinzi ambapo inaonekana kuwa rahisi kupitika, timu hiyo imefunga mabao 12, ikiwa ni timu ya 10 kfunga mabao mengi sawa na Namungo na Kagera Sugar.

Timu yenye mabao machache zaidi kabla ya mechi za jana ni Pamba Jiji iliyofunga nane ikifuatiwa na Tanzania Prisons (9), KMC (11) na JKT Tanzania (11).

MATUMAINI YAMEIBUKA

Ukiangalia duru la kwanza na sasa, kuna timu zimeonekana kuwa na matumaini ya kuimarika kiuchezaji, hiyo inatokana na aina ya matokeo yao.

Tulishuhudia duru la kwanza Fountain Gate ikichapwa 4-0 na Simba, lakini duru la pili imekwenda sare ya 1-1 huku ikimaliza mchezo pungufu baada ya kipa wake, John Noble kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu ndani ya dakika tisa za nyongeza baada ya tisini kukamilika.

Hata Kagera Sugar nayo imeishangaza Singida Black Stars, timu iliyosajili wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa kulinganisha na wao. Sare ya mabao 2-2 ilikuwa nzuri kwa Kagera kwani duru la kwanza ilichapwa 1-0 nyumbani.

Tanzania Prisons chini ya kocha mpya, Amani Josiah, ameanza kazi vizuri kwa ushindi wa 2-1 nyumbani, kipimo cha kuimarika kwa timu hiyo kitaonekana zaidi kesho Jumanne pale timu hiyo itakapokuwa mgeni wa Simba ambapo mchezo wa duru la kwanza Wajelajela hao nyumbani walifungwa 1-0.

MOTO UNAWASHWA BALAA

Katika raundi ya 17 pekee, yamefungwa mabao 25, kwenye mechi nane. Ni raundi ambayo imezalisha mabao mengi zaidi kulinganisha na zilizopita ikifuatiwa na raundi ya 16 yalipofungwa mabao 24.

Raundi ambayo ilikuwa na mabao machache zaidi ni ya tatu ambapo yalifungwa 12. Kabla ya mechi mbili za jana, yamefungwa jumla ya mabao 298.

MZIZE APINDUA MEZA

Kwa muda mrefu, kinara wa ufungaji alikuwa mchezaji wa kigeni ambaye ni Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye mabao manane, akifuatiwa na wageni pia, lakini sasa mshambuliaji mzawa wa Yanga, Clement Mzize amekaa juu kwa mabao tisa.

Wakati Mzize akitamba na mabao, Feisal Salum wa Azam anaongoza kwa asisti, kabla ya mechi za jana alikuwa nazo 10 akiipiku rekodi ya aliyemaliza na asisti nyingi (9) msimu uliopita ambaye ni Kipre Junior aliyekuwa Azam.

VITA YA KILELENI

Simba na Yanga zinaonekana kuwa ndiyo zenye vita ya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Wakati duru la pili linaanza, Simba ilikuwa juu kwa pointi 40, Yanga ilikuwa nazo 39. Ilianza Yanga kushinda mechi yake ya 16 na kufikisha pointi 42, ikaishusha Simba iliyobaki nazo 40 lakini ilirejea baada ya siku moja kutokana na ushindi dhidi ya Tabora United na kukusanya pointi 43.

Yanga ikarejea tena kileleni ikiichapa KenGold 6-0 katika mchezo wa raundi ya 17, siku iliyofuatia   Simba ikalazimishwa sare ya 1-1 na Fountain Gate. Hivi sasa msimamo unaonyesha Yanga ipo juu kwa pointi 45, inafuatia Simba yenye 44.

Vita ya wawili hawa ni kubwa sana kwani ndiyo timu kongwe zinazobadilishana ubingwa wa ligi kwa muda mrefu sasa.

Tangu mwaka 2001 hadi 2024 ikiwa ni kipindi cha miaka 24, Yanga imebeba ubingwa wa ligi mara 13, ikifuatiwa na Simba 10, wakati Azam imechukua mara moja pekee msimu wa 2013-2014.

Akizungumzia kinachoendelea kwenye ligi, Kocha MKuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema: “Ligi bado ina mechi nyingi, kwa hiyo lolote linaweza kutokea, ngoja tuone mwisho wa safari itakuwaje.

“Suala la kufanya makosa kwenye mchezo wa mpira wa miguu kila mmoja linaweza kumtokea, kikubwa tunataka kurudi kwenye njia yetu ya ushindi.

“Simba itarudi kileleni na bado tuko hai kwenye mbio za ubingwa licha ya kufanya makosa ya kuangusha pointi mbili za kwanza ugenini msimu huu,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini,” amesema Fadlu.

Kwa upande wa kocha wa Yanga, Miloud Hamdi, amesema: “Kwa sasa hakuna muda wa kupoteza kwani ukiangalia ratiba kwa mwezi Februari imebanana sana, tuna mechi mfululizo tunazopaswa kucheza.

“Wachezaji wangu wapo timamu hivyo kazi yangu haitakuwa ngumu sana, napambana kuhakikisha nawajenga kiushindani ili kufikia malengo waliyojiwekea mwanzo wa msimu kutetea mataji.

“Hakuna kinachoshindikana, Yanga ina wachezaji wengi bora na wenye uzoefu mkubwa, mbinu imara itakuwa chachu ya wao kuisaidia timu kufikia malengo.”